Saturday, October 7, 2017

CCM WILAYA YA BAGAMOYO YAPATA MWENYEKITI MPYA










Na John Gagarini, Bagamoyo

ABDUL Zahoro Sharifu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani baada ya kumshinda aliyekuwa mwenyekiti Alimasi Masukuzi.

Uchaguzi huo ambao ulifanyika Msata wilayani humo Sharifu alimshinda mpinzani wake kwa kupata kura 711 dhidi ya kura 383 za Masukuzi huku Tariq Kafuku akipata kura 185 na nafasi ya Katibu Mwenezi ilikwenda kwa John Francis maarufu kama Bolizozo aliyepata kura 112 akimshinda Hassan Sharifu aliyepata kura 4.

Kutokana na ushindi huo Sharifu amesema kuwa chama ndiyo kilichoshinda na siyo yeye na kuwataka wagombe na wanachama kuwa kitu kimoja ili kukijenga chama kwa ajili ya kuendelea kushika dola.

“Kuanzia sasa hakuna makundi makundi yamekwisha baada ya uchaguzi na kila mtu anahaki ya kuwa na mgombea anayempenda lakini kwa kuwa mshindi kashapatikana hakuna sababu ya kuwa na makundi,” alisema Sharifu.
Alisema kuwa baada ya uchaguzi kwisha malengo yake ni kujenga chama kwa kuanzisha vitega uchumi na kuachana na tabia ya kutegemea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za chama.

“Furaha yangu ni kuona chama kinajitegemea chenyewe kwa kujiendesha kwani kina miradi mingi na endapo itasimamiwa vizuri itakiletea manufaa chama,” alisema Sharifu.

Kwa upande wake Bolizozo alisema kuwa kwa kutumia nafasi yake atahakikisha anashirikiana na viongozi na wanachama kuleta maenedeleo ya chama ili kiweze kwenye chaguzi kuanzia ya serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment