Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imetakiwa iendee kudhibiti uingizaji mifugo kutoka nje ya nchi ili kuepuka magonjwa ambayo yakiingia yataathiri soko la nje ambalo linapato kubwa.
Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na Mwenyekiti wa Chama Cha Waganga Wasaidizi wa Mifugo Tanzania (TAVEPA) Salim Mselem wakati wa mkutano wa kamati kuu ya chama hicho na kusema kuwa lazima kuwe na udhibiti wa magonjwa.
Mselem alisema kuwa suala la udhibiti wa magonjwa ni mgumu sana lakini serikali kwa kushirirkrana na wataalamu wake wanapaswa kudhibiti uingizwaji wa mifugo hapa nchini.
“Hivi karibuni serikali ilivichoma moto vifaranga ambavyo viliingizwa kwenye mpaka wa Namanga ambapo wahusika hawakufuata taratibu za uingizaji mifugo na hizo ndiyo sheria hata kwenye mataifa mengine,” alisema Mselem.
Alisema kuwa ili kudhibiti magonjwa lazima mifugo inayoingia nchini lazima ikaguliwe ili kuangalia kama imepata chanjo na kama haijapata chanjo lazima uharibiwe.
“Magonjwa mengine ni ya hatari sana licha ya kuathiri soko la nje ambapo endapo itabainika mifugo yetu ina maganjwa haitaruhusiwa kwenye nchi za nje hata kwa afya za walaji pia ni hatari sana na hatutakubali nchi yetu kuwa sehemu ya kuuzwa vitu vibaya,” alisema Mselem.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TAVEPA Ephrahim Masawe alisema kuwa kitengo cha ukaguzi wa uingizwaji mifugo kinapaswa kuwa makini ili kuepuka uingizwaji wa mifugo ambayo haijachanjwa.
Masawe alisema kuwa mifugo inayo ingizwa bila ya kuchanjwa ina hatari ya kuingiza magonjwa ambayo ni ya hatari kwa mifugo pamoja na afya za walaji.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment