Wednesday, November 22, 2017

TANESCO WATAKIWA WATUMIE NGUZO ZA ZEGE

 Waziri wa Nishati Merdard Kalemani akifurahia jambo wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo kwa kutumia zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo 

 Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo kwa kutumia zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo

 Waziri wa Nishati Dk Merdard Kalemani katikati akipata maelezo juu ya uzalishaji wa nguzo kutumia zege


Baadhi ya nguzo zinazozalishwa na kiwanda chaEast Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo

Na John Gagarini, Bagamoyo

SERIKALI imelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza kutumia nguzo za umeme za zege kwenye miradi yake mikubwa ukiwemo ule wa Stieglers Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani ambao mara utakapokamilika utazalisha megawati 2,100 ikiwa ni uzalishaji wa megawati nyingi tangu mwaka 1930 uzalishaji ni megawati 1,451 hadi hivi sasa.

Aidha ifikapo Agosti mwakani nchi itaweza kuzalisha megawati 240 kutoka kwenye mradi wa chanzo cha umeme cha Kinyerezi namba mbili ambapo kuanzia Desemba mwaka huu megawati 30 zitakuwa zinaunganishwa kwenye greti ya Taifa kupitia mradi huo na kutosheleza kwa ajili ya viwanda vilivyopo.

Hayo yalisemwa wilayani Bagamoyo na Waziri wa Nishati Dk Merdard Kalemani alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo kujionea uzalishaji wa nguzo hizo.

Dk Kalemani alisema kuwa baada ya serikali kupiga marufuku uingizwaji wa nguzo za umeme toka nje na kuruhusu wawekezaji kutengeneza umefika wakati shirika hilo lianze kutumia nguzo za zege kuanzia Desemba mwaka huu kwa kuanzia kewenye mradi huo wa Stiglers Gorge.

“Mradi huo unatarajia kutumia nguzo kati ya 500 hadi 600 na kutokana na ukubwa wa mradi huo lazima tutumie nguzo imara ambazo zinauwezo wa kudumu kwa miaka 70 kuliko kutumia nguzo za miti ambazo zinadumu kwa miaka mitatu kwani ni gharama kubwa ukilinganisha na nguzo za zege,” alisema Dk Kalemani.

“Huwezi kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kutegemea malighafi toka nje ya nchi lazima tutegemee vitu vionavyotengenezwa hapa nchini na mmetekeleza agizo la serikali la awamu ya tano kuanzisha viwanda vyetu kwa kutengeneza malighafi wenywe hakuna sababu ya kuagiza vifaa toka nje manufaa yameanza kuonekana tulipozuia wananchi wengi waliomba kuunganishiwa umeme wengine miaka miwili kisa kukosekana nguzo lakini kwa sasa shida hiyo haipo,” alisema Dk Kalemani.

Alisema kuwa walipozuia nguzo zisitoke nje kulikuwa na watu 29,000 walikuhawajaunganishiwa lakioni baada ya hapo watu 20,000 waliunganishiwa umeme na kama kuna mteja hajaunganishiwa umeme zaidi ya mwezi meneja hajafanya hivyo atachukuliwa hatua changamoto kuchelewesha kuunganishiwa hilo ni tatizo la meneja na atachukuliwa hatua kwani hilo ni tatizo lake.

“Utumiaji wa nguzo zinazotumia miti madhara ni kuharibu vyanzo vya maji na mazingira hivyo kaeni na kamapuni hii mshirikiane ili mradi wa Rufiji utakapoanza kutekelezwa zitumike nguzo za zege ambapo kilometa 36 zitatumia nguzo hizo kwani maeneo ya mbugani huwezi kutumia nguzo za miti au kupitisha umeme chini ya ardhi kwani lengo langu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme,” alisema Dk Kalemani.

Awali akielezea juu ya kiwanda hicho mmiliki wake Otieno Igogo ambaye anashirikiana na Wachina katika uzalishaji wa nguzo hizo alisema teknolojia hiyo ni ya kisasa kwa umeme na mawasiliano ambayo inadumu kwa zaidi ya miaka 70 hivyo kupunguza gharama za kuweka nyingine kama ilivyo kwa zile za miti.

Igogo alisema kuwa gharama za ujenzi wa kiwanda hicho ni kiasi cha shilingi ni bilioni 13 ambapo changamoto inayowakabili ni kukosa soko kwenye sekta za umma na binafsi na kuiomba serikali kuwaunga mkono kwa kutumia nguzo hizo kwenye miradi mbalimbali ya mawasiliano na umeme.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kuendelea kufanikisha upatikanaji wa umeme hasa ikizingatiwa mkoa huo ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi hapa nchini.

Mwanga alisema kuwa wilaya ya Bagamoyo na mkoa una mahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuwa na uwekezaji mkubwa hasa kwenye sekta ya viwanda ambayo ina mahitaji makubwa ya umeme na kusema mipango mbalimbali ya uzalishaji umeme itasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo Mbunge wa Jimbo hilo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo ule wa REA ni miradi muhimu sana ambayo inakwenda kuondoa kabisa tataizo la umeme.

Dk Kawambwa alisema kuwa anampongeza Rais wa awamu ya tano Dk John Magufuli kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji wa umeme ambapo kwa miaka mingi kumekuwa na tataizo la upungufu wa umeme na baadhi ya maeneo kutokuwa na huduma hiyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment