Sunday, November 26, 2017

KIFO MTOTO KUUWAWA SERIKALI KUFANYA UCHUNGUZI



 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lukenge kwenye mkutano maalumu

 Mke wa mtuhumiwa Zena Manoza

 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Lukenge waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kibaha hayupo pichani

 Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akiangalia nyumba lilipotokea tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa risasi,kushoto ni matundu ya risasi

Na John Gagarini, Magindu

WAKAZI wa Kijiji cha Lukenge kata ya Magindu wilayani Kibaha wametakiwa kuendelea na shughuli zao na kuishi kwa amani huku serikali ikiendelea na uchunguzi juu ya tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa na bunduki na baba yake mdogo Ally Sakalawe (43) wakati akijibizana na polisi walipokwenda kukagua silaha.

Akizungumza kwenye mkutano mkuu maalumu wa Kijiji hicho mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa serikali inaendelea na uchunguzi na itatoa taarifa ili kuondoa utata ambao umegubika tukio hilo kwa baadhi ya ndugu na wakazi wa kijiji hicho kudai kuwa polisi ndiyo walimwua mtoto huyo aitwaye Mark Joel Modest (15).

Mshama alisema kuwa anajua kuwa tukio hilo limewaumiza sana wakazi hao pamoja na familia husika lakini hawana budi kuwa na subira juu ya uchunguzi ili kubaini ukweili juu ya tukio hilo.

“Nawaomba muishi kwa amani na msiwe na wasiwasi serikali inaendelea na uchunguzi na mtapewa majibu mara uchunguzi huo utakapokamilika watu wanaosema kuwa hawaishi majumbani kuhofia kukamatwa wasiogope kama si wahalifu hawana haja ya kuogopa,” alisema Mshama.

Alisema kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake na haki itatolewa kwani jambo hili linasikitisha sana kwani mtoto kapoteza uhai na alikuwa hausiki kwa lolote.

“Tunamasikitiko makubwa ya kumpotez amtoto huyu ambaye hakuwa na hatia lakini ninachowaomba muwe na imani na serikali kwani inalifanyia kazi suala hili ili kuweza kujua ukweli hivyo nanyi mnapaswa kuwa na imani na endeleeni na shughuli zenu za uzalishaji mali msiishi kwa hofu,” alisema Mshama.

Aidha alisema kuwa wananchi hao pia wawe makini katika kumiliki silaha ambapo mtuhumiwa licha ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji pia alibainika kuwa alikuwa akimiliki gobore bila ya kibali pia alikutwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaleta maswali mengi juu ya matumizi ya silaha hiyo.

“Lazima tujiulize licha ya kifo cha mtoto huyo lakini mtuhumiwa ambaye anashikiliwa na polisi alikutwa na bunduki mbili aina ya gobore, risasi ya mark 4, vipande vya nondo na gololi vyote vikitumika kama risasi hivyo lazima tujiulize matumizi ya silaha hizi,” alisema Mshama.

Awali akielezea juu ya tukio hilo mke wa mtuhumiwa Zaina Manoza alisema kuwa siku ya tukio hilo walikuwa wamelala ndani majira ya saa 8 kwenda saa 9 usiku askari walifika na kuanza kupiga bunduki na wao kuanza kupiga kelele wakiomba msaada kwa majirani.

Manoza alisema kuwa walitakiwa kutoka nje na kuambiwa watoke nje na kujitambulisha kwa majina lakini yeye akawaambia katika hao mtoto mmoja hayupo wakamwambia akamwangalie chumba kingine ambapo alipokwenda alimkuta mtoto huyo akiwa anavuja damu ubavuni.

“Baada ya hapo walinitaka nikamwite mwenyekiti wa kitongoji na alipofika wakawaambia wampeleke mtoto akapate tiba na kunitaka niongozane na huyo mtoto na mwanangu mwingine tukiwa tumembeba nikaona kama hali ni mbaya nikajua tayari kafa,” alisema Manoza.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi wa wilaya Caster Ngonyani alisema kuwa wananchi wanapaswa kuishi kwa amani na hawatakiwi kuwa na woga na hawakwenda kwa ajili ya kuwatisha wananchi na wanafanya kazi kwa kufuata sheria.

Ngonyani alisema kuwa ripoti aliyopewa juu ya tukio hilo ilisema kuwa polisi walikwenda kwenye nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna silaha aina ya gobore bila ya kibali ambapo taarifa hizo walizipata kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ndipo walipokwenda kwa ajili ya kuzikamata.

“Kulikuwa na wamiliki wawili wa hizo silaha ambao ni Ally Sakalawe na Robinus Almas na hawakutoa taarifa kwa uongozi kwa hofu taarifa kuvuja na walipofika waligonga na kushindwa kuingia ndani baada ya mtuhumiwa kukataa kufungua mlango na kuanza kurusha hewani,” alisema Ngonyani.

Alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi mbele ya baba Mzazi Modest na Anna Raphael mama mzazi

“Ndani ya tumbo walikuta kipande cha chuma ambacho ni kipande cha nondo kwenye tumbo la marehemu hali ambayo inaonyesh silaha iliyotumika ni gobore na silaha ya polisi haitumii chuma inatumia risasi na zingekutwa tungejua kuwa polisi walihusika,” alisema Ngonyani.

Aidha alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo ni dhahiri kuwa mtoto huyo alipigwa na mtuhumiwa kwani tumboni kilikutwa kipande cha nondo ambazo zimekatwa na hutumika kama risasi kwenye magobore hayo ambapo vipande vingine 10 vilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 28 mwaka huu wakati polisi walipokwenda kufanya upekuzi juu ya uwepo wa silaha hizo aina ya magobore ambaye yalikuwa yakitumika kwa uhalifu na uwindaji haramu ambapo licha ya mtuhumiwa wa kwanza kukutwa na silaha hizo pia walimkamata Robson Almas naye akiwa na magobore mawili yakiwa hayana vibali vya umiliki.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment