Mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga |
Na
John Gagarini, Kibaha
WATU
walioko kwenye mahusiano ya kimapenzi wametakiwa kufunga ndoa kisheria ili
waweze kutambulika badala ya kuishi kwenye dhana ya ndoa ambayo imesababisha
migogoro mingi mara mahusiano yanapovunjika huku watoto ndiyo wakiwa waathirika
wakuu.
Hayo
yalisemwa mjini Kibaha na mwenyekiti wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Kibaha
(KPC) Catherine Mlenga wakati wa mafunzo ya utoaji wa elimu juu ya masuala
mbalimbali ya Kisehria yaliyoandaliwa na kituo hicho kwa viongozi wa serikali
za Mitaa na Kata ya Kibaha.
Mlenga
alisema kuwa dhana ya ndoa imekuwa ni tatizo sana ambapo mwanamke anaishi na
mwanaume bila ya kufunga ndoa kisheria na kujiita mume na mke lakini mara
inapotokea watu hawa wamechoka kuishi pamoja mwanamke hukosa haki zake za
msingi.
“Watu
wengi wamekuwa wakiishi kwa dhana ya ndoa ambayo haiwatambui kisheria watu hao
kama ni wanandoa na kusababishia mara wanapotaka kutengana mwanamke hunyimwa
mali ambayo waliichuma katika kipindi walipokuwa wakiishi hivyo ni vema
wakafunga ndoa kisheria ili haki ipatikane,” alisema Mlenga.
Alisema
kuwa kama watu wanataka kuwa wanandoa kwanini waishi bila ya ndoa kwani hali
hii husababisha migogoro mingi ya ndoa hizo ambazo haziko kisheria kwa watu
kuchukuana tu na kuishi kama mke na mume.
“Endapo
kutakuwa na ndoa iliyo kisheria itasaidia kupunguza migogoro kwani hata kama
mahusiano ya kindoa yamekwisha kila mtu atapata haki yake kuanzia mume, mke na
watoto lakini watu wakiishi kwa dhana ya ndoa kuna upande ambao hautapata haki
licha ya kwamba watakuwa wamfanya maendeleo muda walioishi pamoja,” alisema
Mlenga.
Aidha
alisema dhana ya ndoa pia husababisha wanandoa kutowajibika lakini kama
wamefunga ndoa sheria inawataka kuwajibika na endapo mmoja atashindwa
kuwajibika mwanandoa anaweze kumshtaki na mhusika kuwajibishwa.
Kwa
upande wake diwani wa Kata ya Kibaha Omary Bula alisema kuwa ndoa nyingi
zinaingia kwenye migogoro kutokana na wanandoa hasa wanawake kutojua haki zao
za msingi hivyo kujikuta wakinyanyasika.
Bula
alisema kuwa ili ndoa iweze kudumu ni kila upande kuwajibika kwa mwenzake kwa
kupeana haki zote ndani ya ndoa na kutawaka wadau mbalimbali waendelee kutoa
elimu ya sheria mbalimbali si za ndoa tu kwa wananchi kama kilivyofanya kituo
hicho.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment