Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Zuberi Samataba ambaye aliongoza ujumbe wa viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China akiongea |
Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Zuberi Samataba akielezea jambo kulia ni mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo |
Baadhi ya washiriki wakijadili baada ya kupokea taarifa ya baadhi ya viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China |
Na John Gagarini, Kibaha
WATAKA kuwekwa wataalamu wa uwekezaji kwenye kila Halmashauri mkoani humo ili kuwawekea mazingira mazuri ya mawasiliano na wawekezaji.
Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huo wakati wa kupokea taarifa toka kwa timu ya wataalamu na viongozi wa mkoa na Halmasahuri ya wilaya ya Kibaha waliokwenda nchini China.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga alisema kuwa wataalamu hao wakiajiriwa itasaidia kurahisisha wawekezaji kuwa na mtu maalumu ambaye atakuwa anawajibika kwa wawekezaji wanaokuja mkoani humo.
“Kukiwa na dawati maalumu kwa ajili ya wawekezaji itasaidia kupunguza usumbufu wa mwekezaji kuzungushwa wakati wa kupata vibali mbalimbali vya uwekezaji,” alisema Sanga.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happynes Seneda alisema kuwa mtaalamu huyo atakuwa akiwajibika na suala la wawekezaji kwani kwa sasa nchi imehamasisha ujengwaji wa viwanda hivyo kutakuwa na wageni wengi toka nje ya nchi kwa ajili ya uwekezaji.
Seneda alisema kuwa mtaalamu atajua masuala mbalimbali yanayohusiana na uwekezaji kuanzia masuala ya ardhi, upatikanaji wa vibali mbalimbali na kuwa na mawasiliano na sekta wezeshi kwa ajili ya kutatua changamoto kwa wawekezaji.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa madawati ya wataalamu wa uwekezaji kwenye Halmashauri pia sekta wezeshi zinapaswa kuwa na wtu watakaokuwa wanahusika na wawekezaji.
Ndikilo alisema kuwa sekta wezeshi kama vile TANESCO, CHALIWASA, DAWASCO, TARURA, TRA, Polisi na Uhamiaji lazima inakuwa na watu wanaofanya kazi ya kushughulikia wageni.
“Tukiwa na wataalamu wa kudili na wageni itakuwa rahisi kutoa huduma kwa haraka na kwa wakati pia itasaidia kuondoa urasimu wakati wa kuwahudumia wawekezaji ili waweze kutekeleza majukumu yao,” alisema Ndikilo.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment