Na John Gagarini,
Rufiji
BAADHI ya wanafunzi walioacha
masomo baada ya kupata ujauzito Wilayani
Rufiji mkoani Pwani wameonyesha kujutia makosa hayo na kumuomba mkuu wa wilaya
kuwasaidia warudi shuleni.
Wanafunzi hao ambao
walifika kituo cha polisi cha wilaya ya Rufiji kufuatia agizo la mkuu wa Nurdin
Babu kuwataka wafike kwenye kituo hapo na kutakiwa kuwataja wale waliowapa mimba ili hatua za
kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo zoezi la
kuwataja wahusika wa mimba hizo lilikuwa gumu kutokana na kubainika kuwa wenye
watoto hao baadhi yao walikuwa ni wajenzi wa barabara ya kuelekea mikoa ya
Kusini.
Wakizungumza na
waandishi wa habari wanafunzi hao ambao walikuwa wakisoma kidato cha pili shule
ya sekondari ya Kazamoyo walifika kituoni hapo wakiwa na wazazi na walezi wao huku
wakiwa na watoto wao mgongoni wamesema wako tayari kurudi shuleni na kuendelea
na masomo.
Semeni Ismail aliyekuwa
akisoma kidato cha pili mwaka huu alikuwa akisoma shule ya sekondari Kazamoyo alisema
kuwa yeye alipata ujauzito baada ya kukosa huduma muhimu ya shuleni hali ambayo
ilimfanya aache shule na kuwa mitaani kwani alikuwa akiishi na mama yake ambaye
wakati huo hakuwepo nyumbani kwani alikuwa akiumwa.
“Maisha yalikuwa
magumu chakula cha shida ada na mahitaji mengine nilikuwa nikiyapata kwa shida
sana kwani baba aliashafariki na mama alikuwa mgonjwa sana, ndipo nilipokutana
na huyo mwanaume ambaye alikuwa fundi wa ujenzi kwenye barabara ya Kusini na
baada ya ujauzito alinikataa hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote,” alisema
Semeni.
Kwa upande wake Hafsa
Twalibu alisema kuwa yeye alifukuzwa shule baada ya kufanya makosa ikiwa ni
pamoja na kuchana barua ya kumsimamisha masomo kwa makosa mbalimbali.
“Nilifanya makosa na
mlezi wangu alipokwenda shule kuusihi uongozi wa shule unisamehe ikiwa ni
pamoja na kufanya adhabu ambazo nilikataa kuzifanya walikataa na kusema labda
nihamishiwe shule nyingine lakini siyo pale tena na waligoma kabisa mimi
kuendelea kusoma pale ndipo alipoacha shule na kujihusisha na masuala ya
kimapenzi na kupata ujauzito huo,” alisema Hafsa.
Wanafunzi hao walisema
kuwa wanaomba msamaha kwa makosa waliyo yafanya na kusema kuwa wako tayari
kuendelea na masomo kama walivyo wenzao na kusema hawatarudia tena.
Naye moja ya wazazi Sauda
Said alisema kuwa walikuwa wakijitahidi kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao
ili wasome lakini kumbe walikuwa wakijihusisha na masuala ya kimapenzi hata
hivyo wanapoulizwa waliowapa mimba hawataki kuwataja.
Mkuu wa wilaya ya
Rufiji Babu alisema kuwa kwa kuwa wanafunzi hao wameomba msamaha na kusema kuwa
wataendelea na masomo atawaombea wanafunzi hao ili ikiwezekana Januari mwaka
2015 waendelee na masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 26 wa
shule za sekondari kwenye wilaya ya Rufiji walipata mimba wakiwa vidato
mbalimbali hali iliyosababisha washindwe kuendelea na masomo yao ambapo wawili kati
yao walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Mwisho.