Na John Gagarini,
Kibaha
KUFUATIA maduka
kadhaa kungua moto eneo la Maili Moja wilayani Kibaha wafanyabiashara mkoani Pwani wameshauriwa
kukatia bima biashara zao ili kukabiliana na hasara zinazoweza kujitokeza
kutokana na majanga kama hayo.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mara baada ya kuwakabidhi msaada wa fedha
kiasi cha shilingi 810,000 wahanga wa moto huo mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoa wa Pwani, Abdala Ndauka alisema kuwa moto
huo umewapa hasara kubwa wafanyabiashara hao.
Ndauka alisema kuwa
imefika wakati sasa kwa wafanyabiashara kukata bima za biashara zao ili mara
wapatapo majanga kama ya moto au wizi bima itawafidia na wataweza kuendelea
vizuri na biashara bila ya kuyumba.
“Ule moto umesababisha
hasara kubwa kwa wafanyabiashara wenzetu kwani hawakuweza kuokoa bidhaa zote
ziliteketea kwa moto hivyo umuhimu wa bima umeonekana kwani wangekuwa nayo
wangelipwa,” alisema Ndauka.
Akizungumzia juu ya
msaada huo alisema kuwa baada ya wenzao kupata tatizo hilo walichanga fedha
hizo kama pole kwa wenzao watatu ambao walipata tatizo hilo la kuunguliwa
maduka yao ya biashara mbalimbali.
Aidha alisema fedha
hizo zimechangwa na sehemu ya wafanyabiashara wanachama wa JWT ambao ni zaidi
ya 300 kati ya 800 wanaounda umoja huo.
“Kutokana na
tukio hili tumeazimia kuanzisha mfuko wa
maafa ili tuweze kusaidiana mara yanapotokea matatizo kama haya na fedha
zitakazopatikana ziweze kuwasaidia waathirika,” alisema Ndauka.
Naye Ally Gonzi
moja ya waathirika wa moto huo aliwashukuru wanajumuiya hiyo kwa msaada walioutoa
na kusema kuwa serikali inapaswa kuhakikisha mkoa huo unakuwa na huduma ya
zimamoto kwani moto ulipotokea hawakuweza kupata huduma hiyo licha ya kuwa
wanalipia huduma hiyo.
Gonzi alisema kuwa endapo
mkoa huo ungekuwa na gari la zimamoto basi mali zilizoteketea zingeweza
kuokolewa hasa ikizingatiwa ofisi za kikosi
hicho ziko jirani kabisa na tukio lilipotokea ambapo waathirika wengine ni
Urisha Mwembamba na Adam Mwasha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment