Friday, November 7, 2014

MAHIZA AKIMBIA OFISI KUKAMILISHA UJENZI WA MAABARA NA KUKU MILIONI 20 KUNUSURIKA NA KIFO

> Na John Gagarini, Bagamoyo
>
> SUALA la Maabara kwa shule za Sekondari za Kata limeingia kwenye hatua
> nzito baada ya mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza kuiacha ofisi yake na
> kuhamia Wilaya ya Bagamoyo ili kuhakikisha agizo la Rais Dk Jakaya Kikwete
> la kila wilaya iwe imekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu.
>
> Sambamba na hilo mkuu huyo amewataka wakuu wa idara wa Wilaya hiyo kila
> mmoja kutokaa ofisini na kuchagua kata ya kwenda ili kusimamia ujenzi huo
> hadi ujenzi wa maabara ukamilike.
>
> Akizungumza juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika mjini
> Bagamoyo Mahiza alisema kuwa ujenzi wa maabara kwenye wilaya hiyo bado
> zoezi hilo haliko vizuri hivyo lazima itumike nguvu ya ziada kufanikisha
> zoezi hilo.
>
> “Kuanzia sasa najua nitaanzia kata gani lakini nahamia Bagamoyo na wakuu wa
> idara kila mmoja tukitoka hapa ataniambia atakuwa kata gani ili tuanze
> usimamizi kwani bila ya kufanya hivi muda utaisha na mambo yatakuwa
> magumu,” alisema Mahiza.
>
> “Kuanzia sasa vikao vya madiwani havitakuwepo kilichobaki wote tuende
> kwenye ujenzi wa maabara na kama mtu anaona hawezi kuwajibika aondoke
> mapema asije akatuharibia mipango yetu ya maendeleo kwani watoto ni wetu,”
> alisema Mahiza.
>
> Mahiza alisema kuanzia sasa hivi hakuna cha mahafali wala sherehe wimbo
> uliopo ni maabara kwa shule zetu za sekondari kwani baadhi ndo wako kwenye
> msingi je ujenzi utakamilika kwa wakati jambo ambalo linatia mashaka.
>
> “Baadhi ya watendaji hawana haraka na kusababisha shughuli kwenda taratibu
> kuanzia sasa hapa ni mwendo wa kufanya kazi kwani tusipokuwa makini muda
> utaisha hatujakamilisha itakuwa haipendezi,” alisema Mahiza.
>
> Aidha alisema kuwa wakuu wa wilaya na mikoa waliitwa Dodoma na Rais na
> kutakiwa wawe wamekamilisha ujenzi huo ifikapo Novemba 30 mwaka huu na wao
> walimwahidi kuwa watakamilisha ujenzi kipindi hicho.
>
> Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo Shukuru Mbato alisema
> kuwa agizo hilo wamelipokea na watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa
> maabara hizo kwa muda uliopangwa.
>
> Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

> CHANJO mpya ya ugonjwa wa Mdondo kwa kuku ya ITA NEW itasaidia kupunguza
> vifo vya kuku wa kienyeji zaidi ya milioni 20 wanaokufa kwa mwaka kutokana
> na ugonjwa huo.
>
> Tayari dawa hiyo imeshapitishwa na mamlaka ya vyakula na dawa (TFDA) kwa
> ajili ya matumizi kwa kuku ambapo Tanzania ina jumla ya kuku wapatao
> milioni 60.
>
> Akizungumza mjini Kibaha makamu mwenyekiti wa chama cha waganga waisidizi
> wa mifugo kitaifa (TAVEPA) ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya madawa ya
> Laprovet Tanzania Ephrahim Massawe alisema kuwa chanjo hiyo ni ya muda
> mrefu.
>
> “Chanjo hiyo inawakinga kuku kwa kipindi cha mwaka mmoja tofauti na chanjo
> nyingine ambazo huisha nguvu kila baada ya miezi mitatu kabla ya kuchanjwa
> chanjo nyingine,” alisema Massawe.
>
> Alisema kuwa ugonjwa huo ni mbaya kwa kuku ambao unaua kuku kwa muda mfupi
> na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji lakini kutokana na kupatikana
> chanjo hii itasaidia kupunguza vifo vya kuku kutokana na ugonjwa huo
> maarufu kama Kideri
>
> “Ugonjwa huo ambao hutokea kwa misimu ya mvua zinapoanza na zinapoishia
> ulikuwa ni tishio kubwa kwa wafugaji kwani ulifikia hatua ya kuua hata nusu
> ya idadi ya kuku wa kienyeji hapa nchini,” alisema Massawe.
>
> Aidha alisema kuwa kupatikana kwa chanjo hiyo kutasaidia kuongeza pato,
> lishe na kukuza uchumi wa kaya ambazo zifafuga kuku hasa vijijini ambapo
> mikoa inayoongoza kwa ufugaji wa kuku hao ni Singida, Dodoma, Shinyanga na
> Morogoro.
>
> Mwisho.
>

No comments:

Post a Comment