Na John Gagarini,
Rufiji
MKUU wa Wilaya ya
Rufiji mkoani Pwani Nurdin Babu amesema atawachukulia hatua kali baadhi ya
madaktari watakaobainika kuiba dawa na kuziuza kwenye maduka ya dawa.
Aliyasema hayo
kwenye Kijiji cha Nyambili-Bungu wilayani humo wakati akielezea umuhimu wa
wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Babu alisema kuwa
baadhi ya madaktari kwenye zahanati vijijini wamekuwa wakiiba dawa muhimu kisha
kuziuza kwenye maduka hayo na kuacha maboksi matupu wakidai kuwa zimetumiwa na
kuisha.
“Dawa hizi si
sukari kusema watu wanalamba kila wakati lakini ni baadhi ya madaktari
wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakiziuza dawa hizo na kila wananchi wanapoandikiwa
dawa wanaambiwa zimekwisha je zinakwishaje wakati wagonjwa hawajapewa
tutawashughulikia nyie tupeni taarifa,” alisema Babu.
Alisema kutokana na
hali hiyo anaacha namba yake ya simu ili apewe taarifa za madaktari wanaofanya
mchezo huo ili akabiliane nao na kuwataka wananchi kutoa taarifa.
Kwa upande wake
mganga mkuu wa wilaya ya Rufiji Dk Michael Michael alisema njia rahisi ya
kupata matibabu ni kujiunga na mfuko huo ambapo familia ya watu sita inalipa
10,000 kwa mwaka lakini kwa wasiojiunga wanalipa 3,000 kila wanapomwona
daktari.
“Uzuri wa sasa ni
kwamba kutakuwa na kamati ya Kijiji ya afya ambayo itakuwa na uwezo wa kununua
dawa wanazoona zimekwisha au zinazohitaji kutokana na tatizo la eneo husika,”
alisema Dk Molel.
Aidha alisema kuwa
wataingia mikataba na wamiliki wa maduka ili dawa zinapokwisha wawe wanawapa
wagonjwa ili kuondoa kero na kusema kuwa mfumo huu utaondoa changamoto ya dawa.
Naye mratibu wa CHF
wilaya hiyo Rashid Mihuka alisema kuwa kutaanzishwa madirisha ya dawa kwa ajili
ya wanachama wa mfuko huo ili kuboresha huduma kwa wateja wa mfuko huo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment