Tuesday, November 18, 2014

WALIOUNGULIWA MOTO WASAIDIWA NA MKE WA MBUNGE ASAIDIA MSALABA MWEKUNDU

Na John Gagarini, Kibaha
WAFANYABIASHARA wa maduka ambayo yaliungua moto eneo la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wamepewa msaada wa mifuko 30 ya saruji yenye thamani ya shilingi 480,000 kwa ajili ya kujenga maduka yao.
Msaada huo ulitolewa na mdau huyo ambaye pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk David Nicas na kusema kuwa ameamua kujitolea ili kuwafariji wahanga hao ambao wamepata hasara kubwa.
Dk Nicas alisema kuwa wafanyabiashara hao walikuwa na mataratijio makubwa ya kuboresha biashara na maisha yao lakini ndoto zao zimekwenda kinyume.
“Janga la moto au lolote halina hodi wa taarifa linatokea wakati wowote bila ya kutegemea na linaleta umaskini kwani hawa waliamka na fedha lakini sasa hawana fedha tena na sisi ndiyo wa kuwasaidia ili kuwapa moyo, alisema Dk Nicas.
Aidha alisema kuwa moto huo umesababisha hasara ambayo haiwezi kulipika zaidi ya kuwasaidia na kuwafariji wafanyabiashara hao ambao bidhaa zao pamoja na fedha viliteketea kwa moto.
“Tunaimba serikali ya mkoa kuhakikisha inakuwa na gari lake la zimamoto badala ya kutegemea kutoka Jijini Dar es Salaam, licha ya kuwa wanalipa fedha kwa ajili ya huduma za zimamoto,” alisema Dk Nicas
Kwa upande wake mwakilishi wa wafanyabiashara hao Ally Gonzi alishukuru msaada huo na kusema kuwa umekuja wakati mwafaka na utawasaidia kukabiliana na gharama za ujenzi mpya wa maduka yao.
“Tunashukuru kwa msaada huu na tunawaomba wadau wengine nao wajitokeze kutusaidia ili angalau tuweze kurejesha biashara zetu kama ilivyokawaida,” alisema Gonzi.
Alisema kuwa gharama za hasara waliyoipata inakadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 700 ambapo katika tukio hilo mfanyabiashara mmoja alijeruhiwa na moto.
Mwisho.   
Na John Gagarini, Kibaha
MKE wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani Selina Koka ametoa hundi ya shilingi milioni moja kwa Chama Cha Msalaba Mwekundu tawi la Maili Moja ili wanunulie vifaa vya kutolea msaada wakati wa majanga.
Akizungumza mjini Kibaha wakati wa mkutano wa Chama na kusema kuwa amejitolea fedha hizo kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma kwa chama hicho kwenye jamii.
Koka alisema kuwa chama hicho ni muhimu ndani ya jamii kwani kimekuwa kikisaidia mara yanapotokea maafa mbalimbali katika jamii kama vile moto, ajali, mafuriko, kimbunga na majanga mengine.
“Nimesikia kwenye risala yenu kuwa mnaazima vifaa kwa ajili ya kutolea huduma naomba niwapatie fedha ili mnunue vifaa vyenu ili mfanye kazi zenu kwa uhakika bila ya kubahatisha,” alisema Koka.  
Aidha alisema kuwa chama hicho ni muhimu sana kwa jamii kwani kinajitolea kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali na dhana kuu ya chama ni kujitolea.
“Hawa wanajitolea kwenye shughuli mbalimbali hivyo tunaomba wadau wajitokeze kuwasaidia hawa ili waisaidie jamii yenye matatizo,” alisema Koka.
Naye mwenyekiti wa chama hicho tawi la Maili Moja Lazaro Kwiligwa alisema kuwa wanamshukuru mke wa Mbunge kwani vifaa ilikuwa ni changamoto kubwa kwao.
“Tulikuwa tunaazima vifaa jambo ambalo linatusababisha tushindwe kutoa huduma ipasavyo  lakini sasa tutafanya kazi zetu kwa uhuru,” alisema Kwiligwa.
Lazaro alisema kuwa tawi hilo lilianza mwaka 2013 na lina wanachama 280 huku hai wakiwa 168 ambapo aliwataka wanachama wote walipe ada zao ili wawe hai.
Mwisho.




Picha 3831 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka kushoto akimkabidhi jora la kushonea sare, mwenyekiti wa tawi la Maili Moja la chama cha msalaba mwekundu Lazaro Kwiligwa.
Picha 3830 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka kushoto akimkabidhi kizibao mwenyekiti wa chama cha msalaba mwekundu tawi la Maili Moja Lazaro Kwiligwa.
Picha 3829 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka akionyesha moja ya vizibao ambavyo alivitoa kwa chama cha msalaba mwekundu tawi la maili Moja, kulia mwenyekiti wa tawi hilo Lazaro Kwiligwa na katikati ni msaidizi wa Mbunge Method Mselewa.
Picha 3784 Mdau wa Maendeleo wa maili Moja wilayani Kibaha Dk David Nicas kushoto akimkabidhi mfuko wa sementi moja ya wafanyabiashara ambao maduka yao yaliteketea kwa moto Ally Gonzi kulia
Picha Na John Gagarini



No comments:

Post a Comment