Na John Gagarini,
Kibaha
MFANYABIASHARA mmoja wa duka la bidhaa mbalimbali Maili Moja
wilayani Kibaha mkoani Pwani Urisha Mwembamba amenusurika kifo baada ya
kujeruhiwa na moto ambao uliteketeza duka lake na mengine matano.
Moto huo ambao
unadaiwa ulitokana na shoti ya umeme ulianzia kwenye jokufu la kuhifadhia
vinywaji baridi ambavyo alikuwa akiuza pamoja na bidhaa nyingine viliteketea
kabisa.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi mmoja wa wahanga wa tukio hilo Ally Gonzi alisema kuwa
tukio hilo lilitokea juzi Novemba 10 majira ya saa 2 usiku
Gonzi alisema kuwa
moto huo ulianza majira ya saa 2 usiku na ulianzia kwenye duka hilo na kusambaa
kwenye maduka mengine baada ya kushindwa kuudhibiti.
“Moto ulianzia
kwenye duka la Mwembamba kwenye jokofu na wakati moto unaanza alikuwepo kwani
aliingia kwa mlango wa dharura lakini alishindwa kutoka akiwa hajui nini cha
kufanya huku moto ukiendelea ndipo wasamaria wema wakaingia na kumtoa ambapo
alijeruhiwa na moto miguuni,” alisema Gonzi
Alisema kuwa moto
ulipokuwa ukiendelea watu walifika na kuanza kujaribu kuzima lakini ulikuwa
mkali sana kwani kuna pipa kubwa la maji kama lita 15,000 wakawasha mashine
lakini moto huo haukuzimika.
“Dada wa Mwembamba aitwaye
Nasra alipopata taarifa akaja kutoka Mbezi naye akazimia kutokana na tukio hilo
ambapo wote walikimbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa ajili ya
matibabu hata hivyo gari la zimamoto lilifika saa moja na nusu baada ya moto
kutokea hata hivyo walifika moto huo ukiwa tayari umedhibitiwa na wananchi,”
alisema Gonzi.
Aidha alisema
waliwasiliana na kikosi cha zimamoto lakini waliambiwa hakuna gari na askari
wakuzuia ghasia FFU walifika na kuzuia wizi lakini hata hivyo watu waliiba vitu
walipokuwa wakijidai kuokoa.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa
jumla ya maduka sita yaliathirika na moto huo na mtu mmoja alijeruhiwa.
“Polisi ilibidi
watumie mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu ambapo baadhi yao walikuwa ni
vibaka waliokuwa wakijaribu kuiba mali kwenye maduka mengine ya jirani,”
alisema Kamanda Matei.
Kamanda Matei alisema
kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana wala thamani ya mali zilizoteketea
bado hakujafahamika na uchunguzi unaendelea aliwataka wananchi kutotumia fursa
kuiba yanapotokea majanga kama hayo badala yake watoe msaada.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment