Na John Gagarini,
Kibaha
CHAMA Cha
Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha
mkoani Pwani kimesema kuwa kitadai haki za wanachama wake kwa kukaa mezani na
si kwa kufanya migomo au maandamano.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Tawi la Kibaha Mji, Adolf Masawa wakati wa
kufunga mafunzo ya viongozi wapya wa matawi kwenye halmashauri hiyo
Masawa alisema kuwa
baadhi ya vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikidai haki zao kwa kufanya migomo na
maandamano jambo ambalo linasababisha utoaji huduma kuwa mbaya.
“Sisi tutafuata
taratibu na sheria katika kudai haki na hatutakuwa tayari kuwatetea wanachama
ambao hawawajibiki kwani haki inakwenda sambamba na uwajibikaji,” alisema
Masawa.
Aidha alisema kuwa
wao hawana ushabiki na ndiyo sababu chama chao huwa hakifuati mkumbo katika
kudai haki zao kama ilivyo kwa baadhi ya vyama hali ambayo inasababisha
usumbufu kwa wateja wanaowahudumia.
Kwa upande wake
katibu wa TALGWU wa mkoa wa Pwani Amina Darabu alisema kuwa chama chao kina
lengo la kuwaunganisha wafanyakazi ili waweze kuwa na mahusiano mazuri na
mwajiri wao ili kuboresha huduma kwa wateja.
“Tuna sisitiza
umoja ujshirikiano na upendo baina ya wanachama pamoja na mwajiri na wateja
wanaowahudumia kwani kwa pamoja huduma zitakuwa bora mahali pa kazi,” alisema Darabu.
Awali akifungua
mafunzo hayo mwenyekiti wa mkoa Mohamed Mahingika alisema kuwa mafunzo hayo
yatawasaidia viongozi hao wapya kujua wajibu na majukumu yao kwa wanachama.
Mahingika aliwataka
viongozi hao kuhamasisha watumishi wa serikali za mitaa kujiunga na chama hicho
ili kuwa na nguvu ya pamoja katika kuboresha utendaji kazi wao.
Mafunzo hayo ya
siku moja yaliwahusisha viongozi kutoka matawi ya Kituo cha Afya Mkoani sasa Hospitali ya Wilaya ya Kibaha,
Kituo cha Afya Mwendapole na kata Kibaha.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment