Tuesday, December 2, 2014

JENGENI BARABARA ZA LAMI

Na John Gagarini, Kibaha
HALMASHAURI za wilaya mkoani Pwani zimetakiwa kuwa na ubunifu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kujenga barabara badala ya kuisubiri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Kutokana na kutokuwa na ubunifu baadhi ya wilaya hazina hata kilomita moja ya barabara ya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.
Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza, wakati wa kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo.
Mahiza alisema kuwa inashangaza kuona kuwa hakuna jitihada zozote zikifanyika za kuhakikisha kunakuwa na ujenzi wa barabara za lami.
“Kaeni na wadau wenu jengeni barabara za lami hata kilomita moja moja mfano mzuri ni Halmashauri ya Mji wa Kibaha imejenga lami kidogo kidogo kwenye baadhi ya maeno lakini zingine hazifanyi jitihada kama hizo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kama halamashauri hazina uwezo zinaweza kuingia mikataba na wajenzi wa barabara ili baadaye wawalipe.
“Mji wa Kibaha ulikopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zake kwa kiwango cha lami kwa hiyo na Halmashauri nyingine ziige mfano huu kwani kikubwa ni ubunifu msikubali kukaa tu,” alisema Mahiza.
Alibainisha kuwa kuna Halmashauri zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kuwasaidia katika kufanikisha ujenzi huo kwani haipendezi kutokuwa na lami ambayo inapendeza na inapunguza ukarabati wa mara kwa mara unaotumia fedha nyingi.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Injinia Tumaini Sarakikya alisema uwezo wao siyo mkubwa kutokana na kutokuwa na fedha nyingi kwani wanategemea kutoka serikalini.
Injinia Sarakikya alisema kuwa wao wataendelea kuboresha barabara pamoja na miundombinu yake ikiwemo madaraja, makalavati na shughuli nyingine zinazohusiana na masuala mazima ya barabara.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment