Na John Gagarini,
Kibaha
CHANGAMOTO ya maji
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani huenda ikawa historia baada ya serikali ya India
kutoa kiasi cha bilioni 800 kwa ajili ya mradi wa maji wa Wami Chalinze.
Akizungumza na
waandishi wa habari mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa
fedha hizo zitasaidia kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa likiwasumbua
wananchi wa wilaya hiyo.
Ridhiwani alisema kuwa
fedha hizo ambazo ni sehemu ya mkopo baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa nchi ya
India alipotembelea nchini hivi karibuni.
“Fedha hizi zitasaidia
kwa kiasi kikubwa kukamilisha mradi huo ambao umekwama kwa baadhi ya maeneo
kutokana na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kutotengeneza miundombinu kwa
kiwango kinachotakiwa,” alisema Ridhiwani.
Alisema mbali ya
kujenga miuondombinu ya kufika kwenye vijiji mbalimbali pia fedha hizo
zitatumika kwa ajili ya kujenga mabwawa ya muda kwa ajili ya kuhifadhi maji na
kuchujia maji.
“Wakati mwingine maji
yamekuwa yakitoka machafu kutokana na maji kuingiwa na tope hasa pale mvua inaponyesha
hivyo tunatarajia kuwe na matanki ambayo yatachuja maji kwani yaliyopo ni
machache,” alisema Ridhiwani.
Aidha alisema pia
kutajengwa vioski na matenki kwenye vitongoji na vijiji 20 kwani baadhi viko umbali
mdogo kwenye baadhi ya matenki lakini
havipati maji.
Alibainisha kuwa Jimbo
la Chalinze baada ya muda mfupi itaepukana na adha ya maji kwani watakuwa na
uhakika wa kupata maji safi na salama kupitia mradi huo kama baadhi ya maeneo.
Na John Gagarini,
Kibaha
WILAYA ya Kibaha mkoani
Pwani imefikia asilimia 80 ya ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na
inatarajia kukamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa mujibu wa mkuu wa
wilaya ya Kibaha Halima Kihemba alisema kuwa wilaya hiyo imeweza kujenga
maabara 53 katika kipindi cha miezi miwili cha agizo la Rais Dk Jakaya Kikwete.
Kihemba alisema kuwa
kulikuwa na changamoto kubwa ambazo zimechangia ujenzi huo kushindwa kukamilika
kwa asilimia 100 ambapo kwa sasa zimebakia maabara 10.
“Changamoto kubwa
ilikuwa ni wenyeviti wa mitaa na viji kujiuzulu kabla ya uchaguzi kwani wao
ndiyo wahamasishaji wakuu wa kukusanya michango pia mwitikio wa wananchi
kuchangia kuwa mdogo na suala la akaunti ya Tegeta Escrow kushusha uchangiaji
kutokana na wapinzani kutumia sababu ya wananchi wasichangie,” alisema Kihemba.
Alisema kuwa wilaya
yetu ina jumla ya shule 21 ambapo kila shule inatakiwa kujenga maabara 3 hivyo
kufanya wilaya kuhitaji maabara 63 na thamani ya kila maabara ni shilingi
milioni 60.
“Tunawashukuru wadau
wetu mbalimbali wa maendeleo na wananchi ambao walitusaidia fedha kwa ajili ya
kufanikisha ujenzi wa maabara hizi na tunaendelea kuwaomba watusaidie ili
tuweze kukamilisha ujenzi huo kama tulivyopanga,” alisema Kihemba.
Mkuu huyo wa wilaya ya
Kibaha alisema kuwa anamshukuru Rais kwa kuwapa msukumo wa ujenzi wa maabara
kwani kwa kipindi kifupi maabara nyingi zimejengwa ambazo zitakuwa na manufaa
makubwa kwa wanafunzi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment