Na John Gagarini,
Kibaha
MTU mmoja
aliyefahamika kwa jina la Juma Abdala (65) mkulima wa Kitongoji cha Kwa Mwaleni
kijiji cha Mbwewe kata ya Mbwewe wilayani Bagamoyo mkoani Pwani amekufa kwa
kuchomwa kwa visu na watu wasiofahamika.
Kwa mujibu wa
mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mzee huyo aliitwa na vijana wawili
waliofika nyumbani kwake na kumwita pembezoni mwa nyumba yake kisha
kumshambulia na kumwua.
Akizungumza kwa njia
ya simu na mwandishi wa habari hizi ofisa mtendaji wa kijiji cha Mbwewe Ramadhan
Mwanaagonile alisema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 6 mwaka huu majira ya
saa 1:30 usiku Kitongojini hapo.
Mwanaagonile alisema
kuwa siku ya tukio vijana hao ambao hawafahamiki walifika nyumbani kwa marehemu
na kumtaka waongee naye wakati huo marehemu alikwenda kwenye kibanda jirani kwa
ajili ya kunywa kahawa.
“Watu hao
walipomuulizia marehemu walijibiwa kuwa hayupo walitaka aitwe ili waongee naye
ndipo alipoitwa na kumtaka wakazungumze pembeni na ndipo walipokwenda kwenye ua
wa nyumba yake na kuanza kuongea,” alisema Mwanaagonile.
Alisema baada ya muda
walisikia marehemu akipiga kelele kuomba msaada huku akisema kuwa anakufa na
walipokwenda walikutwa kachomwa kisu kitovuni na kifuani na mkononi.
“Marehemu alijaribu
kukimbia kwenda waliko watu lakini alishindwa na kuanguka na watu walipofika
walimkuta akiwa anatokwa na damu nyingi ambazo zilisababisha kifo chake huku
wale watu wakiwa hawaonekani kwani walikimbia kusikojulikana,” alisema Mwanaagonile.
Aidha alisema taarifa
zilitolewa kituo cha Polisi cha Mbwewe ambao walifika na kuuchukua mwili wa
marehemu na baadaye mwili ulichunguzwa na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa
ajili ya mazishi.
“Tulijaribu kuwatafuta
vijana hao bila ya mafanikio na hatukukuta chochote pale palikotokea tukio watu
hao hawakumchukulia kitu chochote kwnai alikuwa na simu na vitu vingine lakini
waliviacha,” alisema Mwanaagonile.
Kwa upande wake
kamanda wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo
alisema bado halijafikishwa ofisini kwake na kusema kuwa atafuatilia na
kulitolea taarifa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment