Na John Gagarini, Kibaha
TIMU ya soka ya wanawake ya mkoa wa Pwani imeingia kambini kwenye
shule ya sekondari ya Baden Powell iliyopo wilayani Bagamoyo kujiandaa na
mchezo wake na timu ya mkoa wa Morogoro utakaochezwa Desemba 28 mwaka huu.
Mchezo huo ambao utapigwa kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi
wilayani Kibaha wa kuwania kombe la Taifa kwa wanawake.
Akizungumza na gazeti hili mjini Kibaha, katibu wa chama cha soka
la Wanawake (TWFA) mkoa wa Pwani Florence Ambonisye alisema kuwa maandalizi ya
mchezo huo yanaendelea vizuri.
Ambonisye alisema kuwa timu hiyo inanolewa na mchezaji wa timu ya
Taifa ya Wanawake Hilda Masanche iliingia kambini wiki iliyopita.
“Timu inatarajiwa kurejea Desemba 26 wilayani Kibaha ambapo
itaingia kambini kwenye kambi ya Ruvu JKT Mlandizi siku mbili kabla ya mchezo
huo,” alisema Ambonisye.
Aidha alisema kuwa timu hiyo itaongezewa wachezaji wanne mara
itakaporudi Kibaha ili kuipa nguvu timu hiyo inayoundwa na wachezaji wengi vijana
ambao ni wanafunzi shule za sekondari.
“Changamoto kubwa inayoikabili timu hiyo ni ukosefu wa vifaa kwani
wachezaji wanatumia vifaa vyao binafsi walivyoendanavyo kambini,” alisema Ambonisye.
Alibainisha kuwa wanatarajia kushinda mchezo huo kwani timu yao
imejiandaa vyema na mchezo huo licha ya kuwa wapinzani wao nao wako vizuri na
wana uhakika wa kuingia 16 bora.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment