Na John Gagarini, Kibaha
ESTER Endrew (23) mkulima mkazi wa Tabata Jijini Dar es
Salaam anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Pwani kwa tuhuma za kumwua mwanae
Marko Elibariki (2) kwa kumnyonga kwa kutumia mikono.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini
Kibaha, kamanda wa polisi mkoani hapa Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo
linahusishwa na wivu wa kimapenzi.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 2
asubuhi eneo la Wipas mtaa wa mkoani B kata ya Tumbi wilayani Kibaha.
“Mtuhumiwa baada ya kutekeleza tukio hilo naye
alijichoma tumboni kwa kisu hali iliyosababisha apate majeraha,” alisema
Kamanda Matei.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya tukio baadhi ya
majirani waligundua kutokana na kulalamika huku damu zikimtoka.
“Alijijeruhi tumboni kwa kisu akitaka kujiua lakini hata
hivyo licha ya kujichoma hakufa na kuanza kupiga kelele ndipo majirani
walipotoa taarifa polisi na mtuhumiwa kuja kuchukuliwa ambapo ilibainika kuwa alikuwa akimlaumu mumewe kuwa na mke mwingine,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alisema mtuhumiwa amelazwa kwenye hospitali ya
Rufaa ya mkoa ya Tumbi kwa matibabu huku akiwa chini ya ulinzi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SHAMBA Malela (20) mkazi wa Nianjema wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupatikana na kete
136 za dawa aina ya Heroin.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kamanda wa polisi
mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi
waliokuwa doria.
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 22
mwaka huu majira ya saa 7:45 mchana huko Nianjema kata ya Magomeni wilaya ya
Bagamoyo.
“Mtuhumiwa baada ya kutiliwa mashaka alikwenda
kupekuliwa nyumbani kwake na kukutwa na dawa hizo ambazo zinadhaniwa kuwa ni za
Heroin ambapo hata hivyo thamanai yake haikuweza kufahamika mara moja.
Alisema kuwa jeshi hilo linafanya doria kwenye maeneo
mbalimbali ya wilaya za mkoa huo ili kukabiliana na matukio mbalimbali ya
uhalifu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment