Wednesday, December 24, 2014

BEI ZA BIDHAA ZA VYAKULA HAZIJAPANDA X-MASS

Na John Gagarini, Kibaha
HUKU leo ikiwa ni sikukukuu ya kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo X-MASS ikiwa inaadhimishwa duniani kote wakazi wa wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wanasherehekea kwa furaha kutokana na bei za bidhaa za vyakula zikiwa hazijapanda kama inavyokuwa miaka ya nyuma.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa bei za bidhaa za vyakula hazijapanda kama miaka ya nyuma kwani nyingi ziko vilevile hali amabyo imefurahiwa na wananchi wengi.
Akizungumza na gazeti hili mjini Kibaha mkazi wa Maili Moja Kibena Mtoro alisema kuwa wanasherehekea sikukuu hii huku bei za bidhaa za vyakula zikiwa ni za kawaida.
“Miaka ya nyuma beiza bidhaa za vyakula zilikuwa zinapanda mara dufu lakini mwaka huu tunamshukuru Mungu kwani bei ni zilezile,” alisema Mtoro.
Mtoro alisema kipindi cha nyuma baadhi ya watu wenye kipato cha chini walikuwa hawaifurahii sikukuu kutokana na bei kuwa juu.
“Kutokana na hali ya kiuchumi kuwa mabaya na bei kuwa za kawaida ni dhahiri tunasherehekea sikuku hii kwa furaha kwani kila mtu anamudu kununua chakula,” alisema Mtoro.
Kwa upande wake katibu wa soko kuu la wilaya ya Kibaha Maili Moja, Muhsin Abdu alisema kuwa kwa mwaka huu bei hazijapanda kabisa.
Abdu alisema kuwa bei ya ndizi pekee ndiyo iliyopanda ambapo mkungu umepanda bei kutoka shilingi 20, 000 hadi 35,000 kwa mkungu pamoja na tanagawizi toka shilingi 3,000 kwa kilo hadi 4,500.
“Bei haijapanda kwa sababu mojawapo ni wakulima wengi kuleta bidhaa toka mashambani na kuja kuziuza mjini tofauti na kipindi cha nyuma ambapo wafanyabiashara walikuwa wakileta bidhaa na kuuza kwa bei kubwa,” alisema Muhsin.
Alisema kuwa wafanyabiashara ndiyo walikuwa wakipandisha bei kwa kuficha bidhaa ili wauze kwa bei kubwa wakitoa visingizio mbalimbali.
“Kipindi kile bei zilikuwa juu na zinakuwa adimu lakini safari hii vyakula vingi na bado vinakuja kwa wingi hata sisi tunafurahia hali kwani bei zikiwa juu hata uuzaji unakuwa mgumu,” alisema Abdu.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment