Wednesday, December 24, 2014

PWANIYAONGEZA UFAULU DARASA LA SABA

Na John Gagarini, Kibaha
MKOA wa Pwani umeongeza ufaulu kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa darasa la saba ambapo jumla wanafunzi 13,242 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule mbalimbali za sekondari.
Akitangaza matokeo hayo mjini Kibaha katibu tawala wa mkoa huo Mgeni Baruani na kusema kuwa wanafunzi wote waliofaulu wamepata nafasi ya kujiunga na shule za sekondari.
Mgeni alisema kuwa Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 23,562 waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, ambapo idadi ya waliofaulu wasichana walikuwa ni 6,851 na wavulana ni 6,391 huku idadi ya wanafunzi wasichana ikionekana kuwa juu.
“Kwa mwaka huu mkoa umeweza kuongeza kiwango cha ufaulu kwa asilimia 56.2 kutoka asilimia 54 ya mwaka 2013 hivyo kushika nafasi ya 13 kitaifa na kuwa moja ya mikoa iliyofanya vizuri,” alisema Mgeni.
Aidha alisema kuwa kupatikana kwa nafasi kwa wanafunzi hao kumetokana na mpango madhubuti uliowekwa na sekretarieti ya mkoa kwa kushirikiana na halmashauri mpango wa kuongeza vyumba vya madarasa katika shule zote za sekondari.
“Shule mpya zimejengwa ambazo zilisaidia kuondoa tatizo la wanafunzi kukosa nafasi katika shule za serikali na tunawaomba wazazi na walezi ambao watoto wao wameichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanawaandikisha watoto hao na kuhudhuria shuleni pasipo visingizio mbalimbali hali inayosababisha kuwakosesha haki yao ya msingi kielimu,” alisema Mgeni.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa wa Pwani Yusuph Kipengele alisema changamoto kubwa inayojitokeza kwa sasa ni baadhi ya wanafunzi wanaosoma shule za binafsi kutokwenda kuripoti katika shule wanazopangiwa.
“Wanafunzi hao wanaosoma shule za binafsi unakuta wanapata nafasi za juu lakini wanaokwenda kuripoti shule za sekondari wanzochaguliwa ni wachache labda wakipangiwa shule za sekondari za  Kibaha zinazomilikiwa na shirika la elimu Kibaha hivyo kuipa shida sana idara yetu”alisema Kipengele.
Kipengele alieleza kuwa wanafunzi hao wasioripoti katika shule za sekondari wanazopangiwa wanawanyima nafasi wanafunzi wengine ambao wangepata fursa ya kwenda kwenye shule hizo.
Mwisho

No comments:

Post a Comment