CHAMA Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kimetoa siku mbili hadi
Desemba 10 kwa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) Kibaha kuwarejesha wagombea wa nafasi
mbalimbali kupitia chama hicho na endapo hatawarejesha watafanya maandamano
kushinikiza warudishwe kuwania nafasi hizo.
Jumla ya wagombea 16
wa chama hicho wameondolewa kwenye kinyanganyiro cha kuwania nafasi za uongozi
kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Deemba 14 mwaka
huu, wakiwemo wenyeviti na wajumbe, kutokana na sababu mbalimbali za kukiuka
sheria za uchaguzi.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Kibaha
Mjini Mohamed Mnembwe alisema kuwa wametoa siku mbili Jumatatu na Jumanne
ambapo Jumatano wataandamana kama endapo DAS hatawarejesha wagombea hao kwenye
kinyanganyiro hicho.
Mnembwe alisema kuwa
maandamano hayo watayafanya kuanzia kwenye ofisi za chama kwenda kwa DAS kudai
haki za wagombea wao.
“Kuandamana ni haki ya
kikatiba na si kuvunja sheria ni kutaka wagombea wetu warejeshwe kwani wameondolewa
kwa uonevu na hawakutendewa haki kwani sababu zenyewe za kuwaengua si za halali,”
alisema Mnembwe.
Alisema wagombea wao
hawakupewa nafasi ya kupeleka ushahidi kwani wengi walienguliwa kwa madai kuwa
si wakazi wa maeneo waliyoomba uongozi na kukosea kujaza fomu ikiwa ni pamoja
na mtaa na mahali wanapoishi.
“Wengi waliwekewa
pingamizi kuwa si wakazi wa maeneo hayo lakini wangethibitisha kwa kuwaita
wahusika wakiwemo wenye nyumba kwani kusema kuwa balozi hamtambui si sawa kwani
sisi pia tuna mabalozi wetu kikubwa wangepata ushahidi kama kweli si wakazi wa
maeneo hayo, kwa upande wa ujazaji wa fomu ni mahali unapoishi na mtaa ndiyo
walivyokosea na majina yao kuondolewa,” alisema Mnembwe.
Aidha alisema kuwa wao
wanachotaka ni wagombea wao kurejeshwa kwenye nafasi za kuwania nafasi hizo na
endapo DAS atafanya hivyo hawatafanya maandamano kwani wanataka uchaguzi huo
ufanyike kwa amani na utulivu.
“Tunajua muda umeisha
ila wakirejeshwa tunauhakika wa kushinda kwenye uchaguzi huo na tutatoa taarifa
polisi ili kuomba ulinzi kwani maandamano yetu ni ya amani na hatuna nia ya
kufanya vurugu kikubwa tunachotaka ni haki kutendeka,” alisema Mnembwe.
Mwenyekiti huyo wa
CHADEMA Jimbo la Kibaha alitaja maeneo ambako wagombea wake wameondolewa kuwa
ni Maili Moja 2, Kongowe 6, Visiga 3, Vikawe Shuleni 1,Miswe Chini 1 na
Miwaleni 3.
Hivi karibuni DAS Sozi
Ngate alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo alisema kuwa kama wanaona
wameonewa waende mahakamani kudai haki yao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment