Saturday, December 6, 2014

WANAFUNZI WALIOPATA UJAUZITO WANENA

Na John Gagarini, Rufiji
BAADHI ya wanafunzi walioacha masomo baada ya kupata ujauzito  Wilayani Rufiji mkoani Pwani wameonyesha kujutia makosa hayo na kumuomba mkuu wa wilaya kuwasaidia warudi shuleni.
Wanafunzi hao ambao walifika kituo cha polisi cha wilaya ya Rufiji kufuatia agizo la mkuu wa Nurdin Babu kuwataka wafike kwenye kituo hapo na kutakiwa  kuwataja wale waliowapa mimba ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo zoezi la kuwataja wahusika wa mimba hizo lilikuwa gumu kutokana na kubainika kuwa wenye watoto hao baadhi yao walikuwa ni wajenzi wa barabara ya kuelekea mikoa ya Kusini.
Wakizungumza na waandishi wa habari wanafunzi hao ambao walikuwa wakisoma kidato cha pili shule ya sekondari ya Kazamoyo walifika kituoni hapo wakiwa na wazazi na walezi wao huku wakiwa na watoto wao mgongoni wamesema wako tayari kurudi shuleni na kuendelea na masomo.
Semeni Ismail aliyekuwa akisoma kidato cha pili mwaka huu alikuwa akisoma shule ya sekondari Kazamoyo alisema kuwa yeye alipata ujauzito baada ya kukosa huduma muhimu ya shuleni hali ambayo ilimfanya aache shule na kuwa mitaani kwani alikuwa akiishi na mama yake ambaye wakati huo hakuwepo nyumbani kwani alikuwa akiumwa.
“Maisha yalikuwa magumu chakula cha shida ada na mahitaji mengine nilikuwa nikiyapata kwa shida sana kwani baba aliashafariki na mama alikuwa mgonjwa sana, ndipo nilipokutana na huyo mwanaume ambaye alikuwa fundi wa ujenzi kwenye barabara ya Kusini na baada ya ujauzito alinikataa hadi sasa hakuna mawasiliano yoyote,” alisema Semeni.
Kwa upande wake Hafsa Twalibu alisema kuwa yeye alifukuzwa shule baada ya kufanya makosa ikiwa ni pamoja na kuchana barua ya kumsimamisha masomo kwa makosa mbalimbali.
“Nilifanya makosa na mlezi wangu alipokwenda shule kuusihi uongozi wa shule unisamehe ikiwa ni pamoja na kufanya adhabu ambazo nilikataa kuzifanya walikataa na kusema labda nihamishiwe shule nyingine lakini siyo pale tena na waligoma kabisa mimi kuendelea kusoma pale ndipo alipoacha shule na kujihusisha na masuala ya kimapenzi na kupata ujauzito huo,”  alisema Hafsa.
Wanafunzi hao walisema kuwa wanaomba msamaha kwa makosa waliyo yafanya na kusema kuwa wako tayari kuendelea na masomo kama walivyo wenzao na kusema hawatarudia tena.
Naye moja ya wazazi Sauda Said alisema kuwa walikuwa wakijitahidi kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao ili wasome lakini kumbe walikuwa wakijihusisha na masuala ya kimapenzi hata hivyo wanapoulizwa waliowapa mimba hawataki kuwataja.
Mkuu wa wilaya ya Rufiji Babu alisema kuwa kwa kuwa wanafunzi hao wameomba msamaha na kusema kuwa wataendelea na masomo atawaombea wanafunzi hao ili ikiwezekana Januari mwaka 2015 waendelee na masomo yao.
Jumla ya wanafunzi 26 wa shule za sekondari kwenye wilaya ya Rufiji walipata mimba wakiwa vidato mbalimbali hali iliyosababisha washindwe kuendelea na masomo yao ambapo wawili kati yao walifanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu.
Mwisho.



No comments:

Post a Comment