Friday, December 19, 2014

HABARI ZA PWANI

Na John Gagarini, Chalinze
KATIKA kutekeleza mpango wa Matokeo ya haraka (BRN) Wizara ya Afya imesema kuwa iko katika maongeza na wafadhili kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali badala ya kutegemea kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Asilimia 80 ya dawa zinaotumika zinaagizwa toka nje ya nchi na kuifanya nchi kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kuagiza dawa hizo ambapo endapo kutakuwa na viwanda vingi kutasaidia kupunguza gharama.
Hayo yalisemwa na katibu mkuu wa Wizara ya Afya Donan Mmbando, kwenye Kijiji cha Msoga alipotembelea ujenzi wa kituo cha afya cha kijiji hicho na kusema kuwa dawa bado ni changamoto kubwa.
“Mpango huu kama ulivyo kwenye sekta nyingine utatupima kwa kipindi cha miaka mitatu kutuona je temeweza kufikia malengo ambapo kati ya malengo hayo ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa, upatikanaji wa vifaa tiba na mambo mengine,” alisema Mmbando.
Alisema BRN itafanikiwa endapo kutakuwa hakuna tatizo la upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba ambavyo vimeonekana kuwa ni changamoto kubwa.
“Mbali ya changamoto ya upatikanaji wa dawa pia kuna baadhi ya watumishi wanaojihusisha na wizi wa dawa hawa sasa tutawakamata na kuwatangaza kwenye vyombo vya habari,” alisema Mmbando.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa ujenzi wa Kituo hicho cha afya ambacho ni cha kisasa ni ukombozi kwa watu wa Jimbo hilo ambao hutegemea kuwapeleka wagonjwa kwenye hospitali ya Tumbi.
Ridhiwani alisema kuwa pia majeruhi wa ajali ambao walikuwa wakipelekwa Tumbi sasa watapata huduma hapo ambapo wanatarajia kituo hicho kufunguliwa mwezi Machi mwakani.
Naye diwani wa kata ya Msoga Hussein Mzimba alisema kuwa kituo hicho kinajengwa kwa nguvu ya wananchi, serikali pamoja na wadau wa maendeleo wa kata na wilaya hiyo.
Mwisho.

19,Des
Na John Gagarinii, Chalinze
KITUO cha Afya cha Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kinakabiliwa na ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa kwa kipindi cha miezi mine jambo ambalo linasababisha wagonjwa kukodisha magari kwa ajili ya kupelekwa kwenye hospitali kubwa ikiwemo ya Tumbi.
Hayo yalisemwa na Mganga mkuu mfawidhi wa kituo hicho, Dk Victor Bamba wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete alipotembelea kituo hicho na kuangalia changamoto zinazoikabili sekta ya afya.
“Changamoto hii imetokana na imetokana na gari la wagonjwa lililopo kuwa kwenye matengenezo kwa muda wote huo,” alisema Dk Bamba.
Kwa upande wake Ridhiwani alisema kuwa tayari kuna mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo na magari ya kubebea wagonjwa matatu mkakati utakaotekelezwa mapema mwaka ujao.
“Magari hayo yatagawiwa katika kituo cha afya Chalinze, Miono na kituo cha afya Msoga ambacho kinatarajia kukamilika hivi karibuni,” alisema Ridhiwani.
Kituo cha afya Chalinze kinakabiliwa na changamotombalimbali ikiwa ni pamoja na uhaba wa madawa, chumba cha kuhifadhia maiti, vifaa vya kujifungulia mama wajawazito ambapo kwa miezi 12 sasa havijasambazwa katika kituo hicho.
Mwisho.


Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa ajali kwa sasa zinaonekana kama ugonjwa usioambukiza ambao unaua watu wengi kwa sasa hapa nchini.
Hayo yalisemwa jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa Elimu Mafunzo na Uenezi wa kamati ya usalama Barabarani Taifa Henry Bantu, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani mkoani Pwani.
Alisema kuwa ajali kwa sasa zinaelekea kuwa ugonjwa unaoua kuliko magonjwa mengine kwani mwelekeo ndiyo unaoonekana.
“Endapo jitihada za kuzuia ajali hazitafanyika ajali ndiyo zitakuwa ni ugonjwa usioambukiza unaoua watu wengi nchini kwa sasa lakini hata hivyo baraza linajitahidi kuhakikisha ajali zinapungua,” alisema Bantu.
Bantu alisema kuwa madereva wanapaswa kuwa makini katika uendeshaji wa magari ili kupunguza ajali zisizo za lazima.
“Ajali nyingi siyo bahati mbaya kama wanavyosema watu bali ajali zinatokana na uzembe na si mpango wa Mungu hivyo umakini unatakiwa kuwepo,” alisema Bantu.
Awali akisoma risala ya kamati ya usalama barabarani mkoa Shaban Nkindwa alisema kuwa katika kipindi cha Januari Mosi hadi Novemba 30 jumla ya watu 556 walifariki dunia.
Nkindwa alisema kuwa ajali kwa jumla zilikuwa 1,859 za vifo zilikuwa 424 huku zilizojeruhi zikiwa 1,126 na watu waliojeruhiwa walikuwa 2,601.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limekusanya kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili kutokana na makosa madogo madogo ya usalama barabarani yaliyotokea kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka huu.
Akisoma risala ya kamati ya usalama barabarani mkoa wa Pwani, wakati wa kilele cha siku ya usalama barabarani zilizofanyika jana mjini Kibaha, Shaban Nkwinda alisema kuwa fedha hizo zilitokana na makosa yaliyotokana na makosa yaliyofanywa na madereva.
Nkwinda alisema kuwa makosa yaliyokamatwa yalikuwa 80,786 ambapo ni ongezeko la ajali 23,839 sawa na asilimia 41.8 ikilinganishwa na mwaka jana.
“Makosa yaliyolipiwa yalikuwa 80,259 ikiwa ni ongezeko la ajali 24,293 sawa na asilimia 43.4 ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema Nkwinda.
Alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka jana mkoa uliweza kukusanya kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni moja kutokana na makosa 56,946 kutokana na makosa yaliyolipiwa na 55,966.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment