Na John Gagarini,
Kibaha
JUMLA ya Wazee zaidi
ya 300 kati ya wazee 2,500 kwenye kata ya Kibaha katika halmashauri ya mji wa
Kibaha mkoani Pwani wamepatiwa matibabu ya maradhi mbalimbali.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msamaria Mwema Huduma
za Jamii (GSSST), Elisha Sibale alipozungumza na waandishi wa habari juu ya
huduma walizotoa kwa wazee.
Sibale alisema kuwa
wazee hao ambao wanahudumiwa na shirika lake ni wale wenye umri kuanzia miaka
60 walitibiwa magonjwa mbalimbali kama vile Kisukari, Macho, Wingi wa damu,
Uoni hafifu na ugonjwa wa Ukimwi.
“Lengo la mradi huu ni
kuwawezesha wazee kupata matibabu kwa wakati kwani wengi wao wamekuwa hawapati
huduma hizo kutokana na jamii kutowathamini hivyo kujikuta wakiwa na changamoto
za kuumwa maradhi mengi,” alisema Sibale.
Naye mtaalamu wa
maabara kwenye zahanati ya Mwendapole Hans Amon alisema kuwa wazee hao wameanza
kujiamini kwenda kupata matibabu ambapo awali walikuwa na woga kutokana na
jamii kutowapeleka hospitali na kuwaacha.
Kwa upande wake moja
ya wazee walionufaika na mradi huo Hadija Mbwambo alisema kuwa wameweza kujua
afya zao na kujitambua na kuona umuhimu wa kuwahi kupata matibabu.
Mradi huo wa miaka miwili unatekelezwa kwenye
mitaa ya Kwa Mfipa, Simbani, Mwendapole A na B kwa Kibaha Mjini na Kibaha
Vijijini Mwanabwito na Kikongo na matibabu hayo yalifadhiliwa na shirika hilo
kwa kushirikiana na Help Age International na Pfizer Pharmaceuticals kuanzia
Oktoba Mosi siku ya wazee duniani hadi Desemba mwaka jana na litakuwa endelevu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment