Na John Gagarini,
Kibaha
CHUO Kikuu Huria
Tanzania (OUT) kimepata fedha kiasi cha dola za Kimarekani milioni 50 kutoka
benki ya dunia kwa ajili ya kuwajengea uwezo walimu wa masomo ya Sayansi na
Hisabati hapa nchini.
Aidha fedha hizo pia
zitatumika kwa ajili ya kujenga maabara mchanganyiko, mabweni na ofisi za
walimu kwa lengo la kuboresha ufundishaji wa masomo chuoni hapo.
Hayo yalibainishwa na
mgeni rasmi kwenye mahafali ya kwanza ya OUT kituo cha mkoa wa Pwani, Naibu
Makamu Mkuu wa chuo hicho kitengo cha Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za
Mikoa Profesa Modest Varisanga.
Prof. Varisanga
alisema kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo hivyo wameamua kuwekeza
kwenye masomo hayo kwani ndiyo msingi wa kupata wataalamu mbalimbali.
“Chuo kinaendelea
kujiimarisha kwenye maeneo mbalimbali pamoja na kuhakikisha tunazalisha
wataalamu na msingi ni masomo ya Sayansi ndiyo sababu ya kuweka mkakati wa makusudi
wa kuwawezesha na kuwajengea uwezo walimu hao wanaosoma kwenye chuo chetu,”
alisema Prof Varisanga.
Alisema kuwa fedha
hizo pia zitatumika kujenga maabara mabweni na ofisi za walimu ili kuboresha
utoaji elimu kwa wanachuo ambao hupata masomo yao kwa elimu ya masafa.
Katika hatua nyingine
alisema kuwa wameiomba serikali kuvibadili vyuo hivyo kutoka vituo hadi kuwa
vyuo vya mikoa ambapo maombi hayo yamefikishwa kwenye baraza la Mawaziri na
yamekubaliwa huku kwa sasa mchakato ukiwa unaendelea.
Kwa upande wake
mkurugenzi wa kituo cha mkoa wa Pwani Abdala Alli alisema kuwa elimu ya masafa
ambayo inatolewa na chuo hicho imekuwa suluhisho la elimu hapa nchini wakiwemo
wanawake.
Alli alisema kuwa
elimu ya masafa ndiyo elimu bora kwa sasa kwani inatolewa huku kwa wale
watumishi wakiendelea kufanyakazi bila ya kuathiri utendaji kazi tofauti na
elimu ya moja kwa moja ambayo humtaka mwanachuo kukaa darasani pamoja na kuwa
kwenye bweni ambapo gharama zake ni kubwa.
Akisoma risala ya
wahitimu Stella Mapunda alisema kuwa kituo chao kinakabiliwa na uhaba wa walimu
pamoja na kumbi za mikutano na mihadhara kwa ajili ywa wanachuo kujadiliana na
kujifunzia.
Mapunda alisema kwa
sasa wanatumia majengo ya Shirika la Elimu Kibaha ambayo hayatoshelezi mahitaji
ya wanachuo ambapo kumekuwa na ongezeko la udahili wa wanachuo wapya kila
mwaka.
Jumla ya wahitimu 98 toka
kituo cha mkoa wa Pwani walihitimu na kutunukiwa vyeti ngazi mbalimbali kwenye
mahafali ya Kitaifa yaliyofanyika kwenye makao makuu ya chuo hicho yaliyopo
Bungo wilayani Kibaha wiki iliyopita.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment