Sunday, December 28, 2014

MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA YAWA TISHIO NA WAZEE WAFURAHIA HUDUMA ZA AFYA

Na John Gagarini, Bagamoyo
WATANZANIA wametakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula na ufanyaji wa mazoezi ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yanasababisha vifo vya watu wengi hapa nchini.
Hayo yamesemwa hivi karibu kwenye Kijiji cha Msoga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na katibu mkuu wa Wizara ya Afya Dk Donan Mmbando alipotembelea kukagua ujenzi wa kituo cha afya cha kisasa cha Kijiji hicho.
Dk Mmbando amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na ushindani mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza na yale yanayoambukiza katika kusababisha vifo hivyo jamii inapaswa kuangalia njia za kujikinga na magonjwa hayo.
Amesema kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na presha na mengineyo ya namna hiyo yanasababisha vifo vingi hapa nchini kwa sasa ambapo serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kuyadhibiti
Ametoa mfano wa baadhi ya nchi zilizoendelea zimekuwa zikitenga hadi kufikia asilimia 15 ya bajeti katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kupunguza vifo.
Amebainisha baadhi ya vitu vinavyochangia magonjwa hayo kuongezeka ni pamoja na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe na kutofanya mazoezi ni baadhi ya mambo yanayochangia kuongezeka kwa magonjwa hayo. 
Aidha amesema kuwa wao kama wizara wanasisistiza kinga zaidi ili kukabilina na magonjwa hayo na ndiyo maana wamekuwa wakitoa chanjo za kinga za magonjwa mbalimbali hasa kwa watoto ili kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Katibu mkkuu huyo wa wizara ya Afya amesema wamekuwa wakihamasisha ulaji wa chakula kwa mpangilio kwani chakula nacho kimekuwa ni changamoto ya ongezeko la magonjwa hayo kutokana na ulaji usiofaa, na wamekuwa wakikabili magonjwa hayo kwa kuzingatia taratibu za afya kupunguza vifo.
Amewataka wananchi kupata tiba sahihi ya magonjwa ili kupunguza madhara yatokanayo na magonjwa kuwa sugu pia wajiunge na mifuko ya afya ili kupunguza mzigo wa malipo kwa ajili ya matibabu.

Na John Gagarini, Kibaha
WAZEE wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wameipongeza serikali kwa kuwatengea kitengo maalumu kwa ajili ya kuwahudumia.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwenyikiti wa wazee Mlandizi Mohamed Pongwe wakati wa mafunzo ya kuwahudumia wazee majumbani alisema kuwa kwa sasa huduma zao zimeboreshwa tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Pongwe alisema kuwa huduma kwa wazee kwenye kituo cha Afya cha Mlandizi na sehemu nyingine za huduma za afya zilikuwa ni mbaya kutokana na wazee kutopewa kipaumbele wakati wa kupata matibabu.
“Kwa sasa tunaishukuru serikali ya wilaya kwa kutuwekea kitengo chetu dirisha malumu kwa ajili ya kuwapatiwa huduma za matibabu kwenye kituo hicho cha afya cha Mlandizi kwani tunahudumiwa vizuri,” alisema Pongwe.
Alisema kuwa kama unavyojua wazee wana matatizo mengi hasa ya kiafya lakini walikuwa wakipuuzwa kwenye suala la afya hali iliyokuwa ikisababisha waishi katika hali mbaya za kiafya.
“Tunakwenda hospitali tukiwa hautna wasiwasi wa matibabu kwani tuna dirisha letu maaalumu tunapata huduma kwa upendo kutoka kwa wahudumu wa afya kwa kweli hata afya zetu zinaridhisha,” alisema Pongwe.
Kwa upande wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Elizabeth Sekaya ambaye ni muuguzi wagonjwa majumbani na huduma kwa wazee kutoka halmashauri ya wilaya alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wazee waweze kuwasaidia wenzao kwenye huduma za afya wakiwa majumbani.
“Tumekuwa tukiwapatia mafunzo haya mara kwa mara na tumeona mafanikio kwani sasa wameweza kuyakabili baadhi ya magonjwa wakiwa nyumbani ikiwa ni pamoja na ufanyaji wa mazoezi na lishe bora,” alisema Sekaya.
Sekaya alsiema kuwa wazee wanachangamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na maumivu ya mwili na kingine ni ususaji wa chakula endapo wanaudhiwa hivyo tunawajengea uwezo wa kujiamini na kukabilina na changamoto mbalimbali.
Mwisho.

  


No comments:

Post a Comment