Saturday, October 14, 2023

WATAKA JITIHADA ZIONGEZWE WATU KUKUA KUSOMA KUHESABU NA KUANDIKA

IMEELEZWA kuwa watu wanaojua kusoma kuandika na kuhesabu nchini kwa sasa ni asilimia 77.8 ikilinganishwa na mwaka 1980 ambapo watu hao ilikuwa ni asilimia 9.6.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Profesa Michael Ng'umbi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Nchini wakati wa ufunguzi wa Kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya juma la elimu ya watu wazima kitaifa.

Ng'umbi alisema kuwa mwaka 1980 Tanzania iliweza kufikia kiwango cha juu cha kufuta ujinga kwa watu wasiojua kuandika kuhesabu na kusoma na kufikia asilimia hiyo.

Akifungua mafunzo hayo kaimu mkurugenzi elimu msingi wizara ya elimu sayansi na teknolojia Josephat Luoga alisema kuwa mafunzo hayo yatawezesha kuamsha hamasa ya kutafakuri kuwa tunakwenda wapi katika utoaji elimu.

Luoga alisema kuwa mfumo wa elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi utaweza kubadilisha mtizamo juu ya uendeshaji na usimamizi na tathmini ili kuendana na dira ya maendeleo ya 2025 pamoja na mpango wa maendeleo endelevu 2030.

PROFESA MKENDA AFURAHISHWA TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZIMA INAVYOBORESHA MFUMO HUO

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha elimu ya watu wazima nchini.

Mkenda aliyasema hayo wakati wa kufunga Kongamano la maadhimisho ya kitaifa ya juma la elimu ya watu wazima kitaifa lililofanyika Wilayani Kibaha.

Alisema kuwa serikali itaendelea kujenga uwezo na watendaji kwenye Halmashauri kwenye mikoa zitoe kipaumbele kwa program zote za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dk Charles Msonde alisema kuwa moja ya mkazo uliowekwa ni kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza wanajua kusoma kuandika na kuhesabu.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Profesa Caroline Nombo alisema kuwa jumla ya wanafunzi milioni 5.7 walidahiliwa kwenye elimu changamani kwenye vituo 405.

Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema kuwa baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya program ni pamoja na walimu wa kujitolea kutokuwa na mafunzo ufinyu wa bajeti, upungufu wa vitendea kazi na kushindwa kulipa wa wezeshaji.


Mwisho.

MKUU WA MKOA WA PWANI KUNENGE ATAKA VIONGOZI WALIOHUSIKA UUZAJI VIWANJA ENEO LA MITAMBA WAKAMATWE

KUFUATIA viongozi 24 kujihisisha kuwatapeli watu na kuwauzia eneo la shamba la Mitamba mali ya Wizara ya mifugo na uvuvi Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa  siku 14  kukamatwa viongozi hao.

Aidha viongozi hao ni pamoja na mabalozi, wenyeviti wa mitaa, watendaji  walioshirikiana na madalali  waliohusika kuwauzia  wananchi viwanja katika eneo la shamba hilo lililopo Halmashauri ya Mji Kibaha.

Kunenge alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Pangani uliowahusisha watalaam kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha na mkoa kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya makazi.

Alisema orodha na majina ya viongozi hao na madalali  waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na serikali na kwamba anayakabidhi kwa Taasisi ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru pamoja na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Naye Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha Aron Shushu alisema kuwa kiwanja hicho kilipimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na kwamba  mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.

Shushu alisema kuwa jitihada za kuwakataza wazanchi hao ziliendelea huku baadhi wakionekana kuendelea na shughuli za ujenzi   na kukaidi na walipokea mapendekezo kutoa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Alisema kuwa kuhusu upimaji wa eneo hilo hekta 150 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania (TVLA) hekta 188 kwa ajili ya matumizi ya Taasisi za  Umma, 486  uwekezaji wa viwanda na 200  makazi.


Tuesday, October 10, 2023

DC OKASHI ATAKA WAHUJUMU WAFICHULIWE MIRADI YA MAJI RUWASA BAGAMOYO

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi amewataka wananchi kuwafichua watu wanaohujumu miradi ya maji ambayo serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya uboreshaji wa  huduma ya upatikanaji maji kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Ameyasema hayo Wilayani Bagamoyo wakati alipokuwa akifungua mkutano na wadau wa maji kwenye wilaya hiyo ambayo inaundwa na Halmashauri mbili za Bagamoyo na Chalinze. 

Okashi amesema kuwa serikali imetoa fedha hizo kwa lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa ili huduma ya maji safi na salama inapatikana kwa wananchi vijijini kwa umbali usiozidi mita 400.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bagamoyo James Kionaumela amesema kuwa Wilaya ina vyanzo vikuu viwili vya maji ambavyo ni chini ya ardhi kupitia visima vya kuchimba virefu na vifupi kukiwa na visima 215.

Kionaumela amesema kuwa chanzo cha pili ni maji ya juu inayojumuisha maji ya mito, mabwawa na chemichemi na wilaya hiyo ina vyombo vya watoa huduma 17 ambapo imevipunguza na kufikia vyombo vitano.

Naye mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu amesema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya uboreshaji upatikanaji huduma ya maji.

Diwani wa Kata ya Kibindu na makam mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhan Mkufya amesema kuwa Vijiji viwili vya Kwa Msanja na Kwa Konje ndiko kuna changamoto ya maji.

Mwentekiti wa vyombo vya watumiaji maji Wilaya ya Bagamoyo Jitihada Mwinyimkuu ameiomba serikali kuvihudumia vyombo hivyo kwani vingine vinashindwa kufanya kazi kutokana na vifaa kufa na kushindwa kuvikarabati.


Mwisho.

Sunday, October 8, 2023

WAFANYABIASHARA WAZITAKA MAMLAKA KUBORESHA MIUNDOMBINU

WAFANYABIASHARA wa Tengeru Mkoani Arusha wamewataka baadhi ya viongozi wa mamlaka mbalimbali za Serikali Wilayani humo kuboresha miundombinu ili kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye dhamira njema kwa wafanyabiashara.

Hayo yamesemwa leo na wafanyabiashara wa Tengeru wakati wa Mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) na wafanyabiashara wa eneo hilo uliofanyika kwa lengo ikiwa ni kupokea, kuchakata na kutolea ufafanuzi wa kero, changamoto na maoni ya wafanyabiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara hao Aloyce Mallya amebainisha ukosefu wa soko katika eneo hilo na hata eneo ambalo linatumika kama soko lina miundombinu mibovu ikiwemo huduma za vyoo pamoja na barabara hali inayohatarisha afya za wafanyabiashara na watumiaji wengine wa eneo hilo.

Wamesema kuwa hata hivyo eneo wanalofanyia biashara ni finyu kwa biashara siku za minada hivyo wanaiomba serikali kuwapa eneo ambalo litatumika kufanyia biashara zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa  nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kutatua kero zote za wafanyabiashara nchini hivyo kero hizo zote wanazifikisha sehemu husika kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.

Awali  Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Abdalla Salim amewataka wafanyabiashara wawe wazi kusema kero zao ili kupata ufafanuzi na ufumbuzi wa kero zao na kuwahimiza kujaza fomu ili wasajiliwe na kupata vitambulisho kwani kila Sekta duniani ina utambulisho wake. 

Pia kupitia vitambulisho  hivyo vitawasaidia kutatuliwa changamoto zao na viongozi wa Jumuiya kwa kushirikiana na Mamlaka husika kutatua changamoto hizo.

Naye  Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Ismail Masoud amesema kuwa Rais Samia anawapenda wafanyabiashara ndiyo maana ametoa fursa ya kufanya mikutano nchi nzima ili wafanyabiashara waweze kuwasilisha changamoto na kero zao na amewasisitiza wafanyabiashara kutumia Jumuiya kama chombo cha utatuzi wa kero zao.

*WAZIRI KAIRUKI AIPONGEZA TAWA KWA USIMAMIZI BORA WA WANYAMAPORI NCHINI*

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa jitihada za dhati katika kuleta maendeleo ya uhifadhi nchini ikiwa ni pamoja na Usimamizi mzuri wa Wanyamapori 

Mhe. Kairuki ametoa pongezi hizo Oktoba 7, 2023 alipotembelea bustani ya Wanyamapori hai katika maonesho ya Saba ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo - SITE yanayofanyika Mlimani City Jijini Dar es Salaam

".. niwashukuru wote lakini zaidi niwashukuru TAWA kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya kwa ajili ya maendeleo ya uhifadhi pamoja na kuendelea kusimamia hifadhi zetu mbalimbali na kuhakikisha pia kunakuwa na Utalii ambap ni endelevu unaozingatia masuala mazima ya uhifadhi" alisema Mhe. Kairuki

Aidha Waziri Kairuki amesema Wizara yake kupitia TAWA imepeleka bustani ya Wanyamapori hai katika maonesho hayo ili kuendelea kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na kuvitumia na kuona rasilimali tulizonazo kama Taifa.

Maonesho haya  yanafikia tamati leo Oktoba 8, 2023.

JUMUIYA WAZAZI PWANI YATAKA MAMLAKA USIMAMIZI KUSHIRIKIANA


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani amezitaka mamlaka za usimamizi kushirikiana katika utoaji wa vibali ili kuondoa muingiliano wa kimamlaka.

Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa Wazazi mkoa wa Pwani Jackso Kituka wakati wa kikao cha Baraza la Wazazi Mkoa kilichoganyika Mjini Kibaha.

Kituka amesema kuwa baadhi ya mamlaka zimekuwa zikitofautiana kimaamuzi ambapo moja inaweza ikawa inakataa huku nyingine ikiruhusu kuhusu suala fulani.

"Mfano kama vile Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) linakataza upigaji wa muziki wenye kelele ambapo ni uchafuzi wa mazingira lakini ofisi ya utamaduni inaruhusu upigaji wa muziki kwenye kumbi za starehe,"amesema Kituka.

Naye ofisa mazingira kutoka NEMC Joseph Rugatiri akijibu baadhi ya maswali kuhusu mazingira amesema kuwa vibali vya uchimbaji mchanga hutolewa na halmashauri kama taratibu za uchimbaji mchanga zinakiukwa wananchi wanapaswa kutia malalamiko kwenye ofisi za mitaa na kama hakuna marekebisho taarifa zipelekwe kwao ili wachukue hatua na kuhusu kelele za muziki alisema kila eneo lina kiwango cha sauti.