Saturday, October 14, 2023

MKUU WA MKOA WA PWANI KUNENGE ATAKA VIONGOZI WALIOHUSIKA UUZAJI VIWANJA ENEO LA MITAMBA WAKAMATWE

KUFUATIA viongozi 24 kujihisisha kuwatapeli watu na kuwauzia eneo la shamba la Mitamba mali ya Wizara ya mifugo na uvuvi Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa  siku 14  kukamatwa viongozi hao.

Aidha viongozi hao ni pamoja na mabalozi, wenyeviti wa mitaa, watendaji  walioshirikiana na madalali  waliohusika kuwauzia  wananchi viwanja katika eneo la shamba hilo lililopo Halmashauri ya Mji Kibaha.

Kunenge alitoa maagizo hayo wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Pangani uliowahusisha watalaam kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha na mkoa kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya makazi.

Alisema orodha na majina ya viongozi hao na madalali  waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na serikali na kwamba anayakabidhi kwa Taasisi ya  Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru pamoja na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Naye Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha Aron Shushu alisema kuwa kiwanja hicho kilipimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na kwamba  mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.

Shushu alisema kuwa jitihada za kuwakataza wazanchi hao ziliendelea huku baadhi wakionekana kuendelea na shughuli za ujenzi   na kukaidi na walipokea mapendekezo kutoa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Alisema kuwa kuhusu upimaji wa eneo hilo hekta 150 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania (TVLA) hekta 188 kwa ajili ya matumizi ya Taasisi za  Umma, 486  uwekezaji wa viwanda na 200  makazi.


No comments:

Post a Comment