Wednesday, October 25, 2023

RC KUNENGE ATAKA UJENZI WA MALL YA HALMASHAURI YA MJI UKAMILIKE NDANI YA SIKU 14


MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa siku 14 kwa Mkandarasi anayejenga Maduka Makubwa (Mall) inayomilikiwa na Halmashauri ya Mji Kibaha kukamilisha ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni nane.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri hiyo ambapo mradi huo uko kwenye kitovu cha mji karibu na stendi mpya ya Maili Moja Kibaha.

Kunenge amesema kuwa mradi huo ni mkubwa ambao utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni nane hivyo lazima ukamilike ndani ya muda huo ambapo matarajio ni kuingiza kiasi cha shilingi milioni 450 kwa mwaka.

"Nataka mkandarasi Elray asizidishe zaidi ya wiki mbili ahakikishe anakamilisha ndani ya muda huo tunachotaka akamilishe mradi huu ili biashara zianze kufanyika na Halmashauri ianze kupata mapato,"amesema Kunenge.

Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Brighton Kisheo amesema kuwa Halmashauri hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni nane mwaka 2018-2019 kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambapo wafanyabiashara 253 watapata fursa za biashara na litahudumia watu zaidi 2,000 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Naye mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Pwani Filemon Maliga amesema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuwapatia eneo jirani na Mall hiyo ili wafanye biashara zao na wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kulirasimisha kundi lao ambapo sasa wanatambulika na wanapata fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo.

Miradi mingine aliyoitembelea mkuu huyo wa mkoa ni barabara, ujenzi wa madarasa ya sekondari kata ya Mkuza na maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji wa mitungi ya gesi ya kampuni ya Taifa Gas.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment