Saturday, October 14, 2023

LIONS CLUB YATOA MISAADA YA VIFAA VYA SHULE


KLABU ya Lions ya Jijini Dar es Salaam imetoa vifaa kwa Shule 15 za Msingi na Sekondari Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilayani Bagamoyo zenye thamani ya zaidi ya milioni sita ili kukabiliana na uhaba wa vifaa kwenye shule hizo.

Hayo yalisemwa kwenye  shule ya msingi Ruvu Darajani kata ya Vigwaza na Rais wa zamani wa klabu hiyo Muntazir Bharwani wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa shule ambapo ziliwakilishwa na walimu wakuu wa shule hizo.

Bharwani amesema kuwa klabu yao inajihusisha na kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kwenye sekta za elimu, afya na maji na masuala mengine ya kimaendeleo.

"Tumetoa vifaa vikiwemo vitabu vya walimu kwa ajili ya kufundishia, madaftari pamoja na mipira kwa ajili ya kuwaweka wanafunzi kwenye utimamu wa akili,"amesema Bharwani.

Akipokea misaada hiyo ofisa elimu msingi na awali wa Halmashauri ya Chalinze Miriam Kihiyo ameishukuru klabu hiyo na kuomba iendelee kusaidia kwenye sekta hiyo.

Kihiyo amesema kuwa mahitaji kwenye sekta ya elimu ni kubwa kutokana na kuwa na wanafunzi wengi na kuomba wadau wengine waendelee kujitolea misaada mbalimbali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Vigwaza Musa Gama amesema kuwa anashukuru kwa misaada hiyo ambayo itasaidia kupunguza sehemu ya baadhi ya changamoto.

Gama amesema kuwa msaada huo ni motisha kwa walimu na wanafunzi katika kuhakikisha elimu inaboreka na kuwataka wananchi wawasimamie watoto wao ili wapate elimu ipasavyo.

No comments:

Post a Comment