WAFANYABIASHARA wa Tengeru Mkoani Arusha wamewataka baadhi ya viongozi wa mamlaka mbalimbali za Serikali Wilayani humo kuboresha miundombinu ili kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye dhamira njema kwa wafanyabiashara.
Hayo yamesemwa leo na wafanyabiashara wa Tengeru wakati wa Mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) na wafanyabiashara wa eneo hilo uliofanyika kwa lengo ikiwa ni kupokea, kuchakata na kutolea ufafanuzi wa kero, changamoto na maoni ya wafanyabiashara.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Aloyce Mallya amebainisha ukosefu wa soko katika eneo hilo na hata eneo ambalo linatumika kama soko lina miundombinu mibovu ikiwemo huduma za vyoo pamoja na barabara hali inayohatarisha afya za wafanyabiashara na watumiaji wengine wa eneo hilo.
Wamesema kuwa hata hivyo eneo wanalofanyia biashara ni finyu kwa biashara siku za minada hivyo wanaiomba serikali kuwapa eneo ambalo litatumika kufanyia biashara zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa nia ya Serikali ya awamu ya sita ni kutatua kero zote za wafanyabiashara nchini hivyo kero hizo zote wanazifikisha sehemu husika kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi.
Awali Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Abdalla Salim amewataka wafanyabiashara wawe wazi kusema kero zao ili kupata ufafanuzi na ufumbuzi wa kero zao na kuwahimiza kujaza fomu ili wasajiliwe na kupata vitambulisho kwani kila Sekta duniani ina utambulisho wake.
Pia kupitia vitambulisho hivyo vitawasaidia kutatuliwa changamoto zao na viongozi wa Jumuiya kwa kushirikiana na Mamlaka husika kutatua changamoto hizo.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Ismail Masoud amesema kuwa Rais Samia anawapenda wafanyabiashara ndiyo maana ametoa fursa ya kufanya mikutano nchi nzima ili wafanyabiashara waweze kuwasilisha changamoto na kero zao na amewasisitiza wafanyabiashara kutumia Jumuiya kama chombo cha utatuzi wa kero zao.
No comments:
Post a Comment