Thursday, October 5, 2023

NSSF YAPIGA VITA VITENDO VYA RUSHWA

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoani Pwani, imetoa rai kwa Mtumishi ama Mtendaji yeyote anaejihusisha na vitendo vya rushwa kuacha mara moja vitendo hivyo kwani vinachangia kuzorotesha utoaji wa huduma kwa wateja.

Akifungua maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kimkoa, Meneja wa NSSF Mkoani Pwani, Witness Patrick ,amesema wanashirikiana na Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU) kudhibiti mazingira ya vitendo vya rushwa kwenye maeneo ya kazi.

Amewaasa ,kila mmoja kujitathmini na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kudumisha imani kwa wanachama na wadau.

Witness ameeleza kuwa, mfuko hautamvumilia mtendaji yeyote atakaeshindwa kuendana na viwango na kasi ambayo mfuko unatarajia kuifikia.

Anasema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inapinga rushwa kwa vitendo, na Nssf inaunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kukemea masuala yote ya rushwa.

Vilevile Witness amewahimiza ,watumishi na wananchi wema kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyotendeka katika maeneo yao ya kazi kwani kutokutoa taarifa ni kushiriki rushwa.

Halikadhalika," anawasihi kutumia mfumo mpya wa NISS katika kuandikisha wanachama wengi zaidi wa mfumo wa kujichangia kwa hiari ili kuongeza wigo wa kinga ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi.

Naye mwanachama wa Nssf Kibaha, Vicent Ndumbili ameipongeza Nssf kwa kujali wateja wake.

Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi kimataifa mwaka 1984 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja ambapo mwaka huu 2023 yanaanza octoba 2-octoba 6 kilele.


Mwisho

No comments:

Post a Comment