Tuesday, October 31, 2023

TAKUKURU PWANI YAFANIKISHA MTENDAJI KUREJESHA MILIONI 4 ZA KIJIJI ALIZOZICHUKUA ZA MAUZO YA ARDHI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kurejesha kiasi cha shilingi milioni nne za Kijiji cha Kanga zilifanyiwa ubadhirifu na kaimu mtendaji wa Kata ya Kanga wilayani Mafia.

Aidha fedha hizo ambazo ni asilimia tano ni tozo ya mauzo ya kiwanja cha Kijiji hicho ambacho kiko ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Sadiki Alli akitoa taarifa ya miezi mitatu ya utendaji kazi kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu. 

Alli amsema kuwa mtuhumiwa huyo jina linahifadhiwa fedha hizo hakuziwasilisha ofisini wala kuzipeleka benki kwenye akaunti ya kijiji.

Amesema mtuhumiwa huyo ambaye pia ni ofisa mazingira wa kata alibainika kwenye mkutano wa Takukuru Rafiki ambapo wananchi waliibua kero hiyo na ndipo walipofanya uchunguzi juu ya tukio hilo na kufanya ufuatiliaji.

"Baada ya uchunguzi tulibaini kuwa tukio hilo ni la kweli na alirejesha fedha hizo na tumemwandikia mwajiri wake ili achukuliwe hatua zaidi za kisheria kuhusu tukio hilo,"amesema Alli.

Amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na mkutano wa Takukuru Rafiki na kuwataka wananchi watumie mikutano hiyo ili kutoa kero zao juu ya vitendo vya rushwa.

"Wananchi watoe kero zao za rushwa kupitia mikutano tunayoiandaa kupitia Takukuru Rafiki kwani hapo ni moja ya sehemu wanazoweza kutoa taarifa kama watashindwa kutuletea taarifa ofisini,"amesema Alli.

Katika hatua nyingine amesema kuwa jumla ya matukio 126 ambapo 92 yalihusu masuala ya rushwa huku 34 hayakuhusu rushwa na 27 wahusika walipewa ushauri manne yalifungwa na matatu yalihamishiwa idara nyingine.

Ameanisha idara ambazo zinaongoza kwa malalamiko kuwa ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) yenye malalamiko 44, na elimu 17, ardhi 15, ushirika sita, binafsi tano na polisi nne.

Ameongeza kuwa idara nyingine ni afya na kilimo tatu, bandari, fedha, madini, maji, misitu na utawala malalamiko mawili kila moja, idara ya biashara, ofisi ya mkuu wa wilaya, mifugo, maendeleo ya jamii, Mamlaka ya Mapato TRA, uchukuzi, ujenzi, Tanesco, utalii na viwanda lalamiko moja moja kila idara.

No comments:

Post a Comment