DODOMA.
IMEELEZWA kuwa shughuli za kijamii na kiuchumi, mwenendo na mifumo ya maisha na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kumekuwa na ongezeko la magonjwa yanayoibuka kutokana na mwingiliano uliopo baina ya binadamu, wanyama na mazingira.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu ( Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama , wakati akifungua kongamano la kitaifa la Afya Moja ambapo amesema kuwa duniani kote takriban visa bilioni 1 vya ugonjwa na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Aidha amezisihi Wizara za Kisekta kuwa na mipango ya kutekeleza na kuimarisha ushirikiano wa kisekta kwa kutumia mbinu ya Afya Moja na kila sekta kushiriki kikamilifu katika tafiti kuhusu magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, utunzaji wa mazingira, usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, usalama wa chakula na lishe na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Nao baadhi ya washiriki wa kongamano hilo wamesema kuwa dhana ya Afya moja faida yake ni njia inayowaleta pamoja na sekta mbalimbali ambapo ni afya, mifugo na wanyamapori ili kukabiliana na changamoto zinazohusiana na afya.
Kila ifikapo Novemba 3 ya kila mwaka wadau mbalimbali huadhimisha siku ya Afya Moja kwa lengo la kuimarisha uratibu na utendaji uliopo baina ya sekta katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na majanga ya milipuko ya magonjwa ya binadamu, wanyama na mimea ambapo kauli mbiu mwaka huu inasema “Afya Moja: Mbinu ya Pamoja kuboresha afya ya binadamu, wanyama, mimea na mfumo wa ikolojia kwa ustahimilivu wa maafa.
No comments:
Post a Comment