WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kulipa kodi kwa hiyari ili wawe huru kufanyabiashara na kuchangia mapato ya serikali ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Taifa Hamis Livembe alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wa Wilaya ya Kibaha wakati wa ziara yake kutembelea Mkoa wa Pwani.
Livembe alisema kuwa kila upande una wajibu kwa mwenzake ambapo serikali inaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na kwa wafanyabiashara kazi yao ni kulipa kodi.
"Naombeni wafanyabiashara mlipe kodi kwa hiyari kwani serikali imeweka mazingira mazuri ya sisi kufanya biashara na hata kama kuna changamoto imeacha milango wazi kwa ajili ya majadiliano kama kuna kero kuhusiana na kodi,"alisema Livembe.
Alisema kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameamua kufungua milango ya biashara ili wafanyabiashara wafanye biashara zao kwa uhuru na hataki kuona wanabughudhiwa.
"Tumuunge mkono jitihada za Rais anazo zifanya kwa wafanyabiashara kwa kutatua kero zetu hivyo tukilipa kodi vizuri nchi itasonga mbele kwenye suala la maendeleo na nchi itafunguka,"alisema Livembe.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta alisema kuwa Jumuiya hiyo inafanya kazi kubwa ya kizalendo kwani nchi inapokusanya vizuri mapato yanarudi kwa wananchi kwa kutoa huduma kwa ufanisi.
Mchatta alisema kuwa wajibu wa kulipa kodi ni muhimu na kama kuna changamoto watashirikiana na wafanyabiashara kuzitatua kwa pamoja ili mazingira ya biashara yawe rafiki.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) Mkoa wa Pwani Abdala Ndauka alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kutatua baadhi ya changamoto za wafanyabiashara.
Ndauka alisema kuwa changamoto zao zikitatuliwa watafanyabiashara kwa uhuru na kuwezesha biashara kukua hivyo kulipa kodi kwa hiyari na kuleta maendeleo ya nchi.
Moja ya wafanyabiashara ambaye ni mwanachama wa Jumuiya hiyo Mkoani humo Hassan Msemo alisema kuwa moja ya changamoto wanazozipata ni baadhi ya viwanda kutokuwa na stoo za kuuzia bidhaa wanazozizalisha ambapo nyingi ziko Jijini Dar es Salaam hivyo kuwagharimu kuzifuata.
Msemo alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo husababisha kuzifuata Jijini Dar es Salaam hivyo gharama kuwa kubwa na hata bei za kuuzia nazo zinakuwa juu.
No comments:
Post a Comment