Wednesday, November 22, 2023

JAMII MKOANI PWANI YATAKIWA KUWALINDA WATOTO

JAMII Mkoani Pwani imetakiwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto kwa kumuondolea vikwazo na kutoa taarifa kwa wanaofanya vitendo vya ukatili ili mtoto aweze kutimiza ndoto zake.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta alipokuwa akizindua mradi wa Usalama wa Watoto (UWAWA) awamu ya pili unaosimamiwa na Christian Social Services Commission (CSSC).  

Mchatta amesema watoto wanakabiliwa na changamoto nyingi ambapo jamii inatakiwa kuwalinda kwani nao wana ndoto zao za kuwa nani katika jamii mara wamalizapo masomo yao.

"Mradi wa uwawa una lengo la kuimarisha usalama wa watoto utasaidia kuanzishwa dawati la kushughulikia changamoto za watoto kukabiliana na ukatili kwa watoto shuleni na sehemu yoyote wawapo watoto,"amesema Mchatta. 

Naye Ofisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto wakati mwingine vinatokana na utandawazi na baadhi wanafanyiwa na wazazi wa kuwazaa kama kuwanyima chakula na watoto hujikuta wakifanya vibarua ili wapate fedha.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki wa (CSSC) Makoye Wangeleja amesema kuwa wanaushukuru mkoa kwa kutoa ushirikiano kwani vita hiyo siyo lelemama kwani watu wanaowafanyia vitendo hivyo ni watu ambao huwezi kuwafikiri na inabidi kujipanga ili kukabili vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto na watafuata taratibu ili kuweka misingi mizuri ya kuwalinda watoto.







No comments:

Post a Comment