SERIKALI Kuu imeupatia Mkoa wa Pwani kiasi cha shilingi trilioni 1.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imeainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamesemwa na Kamisaa ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge wakati akiwasilisha taarifa ya miradi iliyotekelezwa mkoani humo katika kipindi cha Machi 2021 hadi Juni 2023 kwenye kikao cha Kamati kuu ya Chama hicho mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kwa Mfipa wilayani Kibaha.
Kunenge amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, nishati, maji na miundombinu ya barabara.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amesema chama kimeridhika na miradi iliyotekelezwa na serikali imetimiza matakwa yaliyopo kwenye Ilani ya CCM katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani Benard Ghatty amesema hadi sasa serikali imefikisha asilimia 98 ya utekelezaji wa miradi na kwamba sehemu iliyosalia ni ndogo ambapo wanaamini ifikapo mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu miradi yote itakamilika.
No comments:
Post a Comment