KATIKA kuadhimisha siku ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (Watoto Njiti) Duniani Tasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na baadhi ya wadau imetoa misaada kwa watoto njiti kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila.
Aidha imetoa misaada kwenye sekta ya elimu ili kuboresha mazingira ya usomaji na vifaa kwa wanafunzi wa baadhi ya shule Wilayani Kibaha.
Misaada hiyo ambayo ni saruji, sabuni, mafuta ya watoto na mavazi ya michezo vimetolewa leo mbali ya Hospitali ya Mloganzila ni pamoja na Shule ya Msingi Kambarage na Mlandizi.
Katibu wa Taasisi hiyo ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Omary Punzi amesema kuwa wamefikia hatua hiyo ili kuendelea kutimiza malengo ya Taasisi hiyo ambayo ni mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na uamsikini.
Punzi amesema kuwa mbali na hilo pia hatua hiyo inalenga kuikumbusha jamii ili kutambua kuwa bado tatizo la watoto njiti lipo na linaendelea kuwaandama wajawazito wengi hivyo ni vema likapewa kipaumbele na kuongeza nguvu katika kukabiliana nalo.
Amesema kuwa Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza malengo yake kwa kujiweka karibu na jamii ambapo katika msaada huo imeshirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki wanathamini wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi huduma za tiba wa Hospital ya Mloganzila Dk Faraja Chiwanga amesema kuwa sababu mbalimbali zinatajwa kuchangia hali hiyo ni pamoja na magonjwa yasiyoambukiza na ukosefu wa lishe bora.
Naye mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Kambarage Happynes Tesha amesema kuwa msaaada wa mifuko 50 ya saruji iliyotolewa na taasisi hiyo itaongeza nguvu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment