KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imetembelea mradi wa Maji wa Wami awamu ya tatu kwenye chanzo Mto Wami na kufurahishwa na jitihada za Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha huduma ya upatikanaji maji inakuwa ya uhakika.
Hayo yamesemwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Deus Sangu wakati wa ziara iliyofanywa kutembelea mradi huo kuangalia maendeleo ya mradi huo ambao kwa awamu zote umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 160.
Sangu amesema kuwa wameridhishwa na jitihada za Dawasa na kuahidi kuendelea kuipambania ili iweze kukabili changamoto za upungufu wa maji na kupitia Bunge kati ya maazimio 14 mawili ni ya kuisaidia mamlaka hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa upatikanaji wa maji kwa mkoa huo ni asilimia 86 ambapo aliomba miradi itekelezwe vizuri ikizingatiwa ni mkoa wa uwekezaji wa viwanda na mahitaji ya maji kwa sasa ni makubwa kwani kuna ongezeko la watu na uwekezaji mkubwa ambapo bila ya maji hakuna uwekezaji.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete ameishukuru kamati hiyo kwa kupambani Chalinze kupata maji kwani kwenye mikutano yake hakuna jambo ambalo lilikuwa kero kwa wananchi kuhitaji maji ambapo kwa sasa changamoto ya maji imepungua kwa kiasi kikubwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa awamu ya tatu Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa Kiula Kingu amesema kuwa maji yatazalishwa kutoka lita milioni saba hadi lita milioni 21 ambapo mabomba yatatandazwa kwa kilometa 124 na matenki 18 na kutakuwa na vituo vikubwa vya maji Miono, Msoga na Mboga.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment