Monday, November 20, 2023

MAOFISA TARAFA NA WATENDAJI KATA PWANI WATAKIWA KUWA WABUNIFU KULETA MAENDELEO KWA WANANCHI

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka Maofisa Tarafa na Watendaji Kata kuwa wabunifu kwa kutafuta suluhisho la kutatua changamoto za wananchi.

Ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ili kuboresha utendaji kwa maofisa hao kutoka Halmashauri tisa za mkoa huo.

Kunenge amesema kuwa kazi kubwa ya kiongozi ni kutatua changamoto ili kuwaletea wananchi maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa moyo pia kujua jamii inataka nini.

"Inashangaza kuona Rais anapelekewa malalamiko kutoka kwa wananchi na sisi tupo ambapo tungeweza kutatua changamoto husika lazima tuwe na ubunifu na kufanya kazi kwa weledi,"amesema Kunenge.

Naye Mkurugenzi msaidizi idara ya serikali za mitaa Ibrahim Minja amesema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwaendeleza kiuwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, kuwajengea uwezo na ufanisi na kujua na kuzifuata taratibu  kanuni, sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Minja amesema kuwa yanawahusisha maofisa hao 160 ambapo waliofika ni 152 ambapo ni ya awamu ya pili kwa Kanda ya Mashariki Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara awamu ya kwanza yalifanyika kwenye mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Katavi na timu nyingine ikifanya kwenye mikoa ya Singida, Tabora na Shinyanga.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo Jane Mwanamtwa ofisa Mtendaji kata ya Kawawa wilaya ya Kibaha amesema yana umuhimu kwa sababu wanakumbushwa wajibu wao pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo kukamilika kwa wakati pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wananchi wanaowahudumia.



No comments:

Post a Comment