Sunday, November 26, 2017

UJUMBE WA WAWEKEZAJI TOKA NCHI YA CHINA WATUA PWANI

 Baadhi ya wawekezaji toka nchini China wakiwa wanamsikiliza mkuu wa mkoa wa Pwani hayuko pichani walipomtembelea ofisini kwake Mjini Kibaha

 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza na ugeni wa wawekezaji toka nchini China waliomtembelea ofisini kwake kulia ni katibu Tawala wa mkoa huo Zuberi Samataba na kushoto mwakilishi wa wawekezaji toka China Liv Ming

 Mkuu wa mkoa katikati waliokaa akiwa na ugeni toka nchi ya China walipomtembelea ofisini kwake mjini Kibaha 

 Mkuu wa mkoa wa Pwani na mgeni wake na katibu tawala wa mkoa wakiwa wanafuatialia mazungumzo

 Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimkabidhi zawadi mwakilishi wa wawekezaji toka nchi ya China
Wataalamu wa mkoa
Wataalamu wa mkoa 

 Mkuu wa mkoa wa Pwani akimkabidhi zawadi moja ya wawakilishi wa wawekezaji toka nchi ya China

Na John Gagarini, Kibaha

WAWAKILISHI wa makampuni toka nchi ya China wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani Pwani baada ya kuonyeshwa fursa za uwekezaji kwenye mkoa huo.

Wakizungumza baada ya kumtembelea mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wawakilishi hao baada ya kuonyeshwa maeneo hayo ya uwekezaji kwa njia ya video waliahidi kuwatuma wataalamu ili waone wawekeze kwenye masuala gani.

Mwakilishi wa wawekezaji hao Liv Ming alisema kuwa wamefurahishwa na nchi ya Tanzania na kikubwa ni uhusiano mzuri uliokuwepo tangu enzi za marais Julius Nyerere na Mao Tse Sung.

“Tumeona fursa nyingi za uwekezaji na tunatarajia kuwatuma wataalamu wetu kujua kuangalia na kutupa ushauri lakini baadhi ya vitu ni uwekezaji kwenye sekta ya umeme, vipuri vya magari na uhifadhi wa mazao,” alisema Ming.

Alisema kuwa wameona maeneo mbalimbali kwa njia ya video ambayo wanaweza kuwekeza na wataendelea kufanya mawasiliano na mkoa kwa ajili ya masuala ya uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.

“Tumevutiwa na mambo mengi pia kuna baadhi ya makampuni ya wenzetu kutoka China wamewekeza viwanda mengine yanazaidi ya miaka 20 hivyo tutaendelea kuhamasisha wenzetu nao waje kuwekeza,” alisema Ming.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa ujio wa wageni hao ni faraja kwa mkoa pamoja na nchi kwa ujumla kwani itasaidia azma ya serikali ya kuwa nchi ya viwanda.

Ndikilo alisema kuwa mkoa utaendelea kuhamasisha wawekezaji wa nje na ndani ya nchi ili wawekeze kwenye sekta mbalimbali ikiwemo viwanda ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya nchi ya viwanda na uchumi wa kati.

Ujio wa wawekezaji hao ni kufuatia ziara ya wiki mbili iliyofanywa na timu ya mkoa wa Pwani ya Viongozi pamoja na wataalamu walioifanya mwezi Oktoba mwaka huu ambapo waliweza kuzungumza na makampuni 106 na 30 kukubali kuja mkoani Pwani kwa ajili ya kuja kuangalia maeneo ya uwekezaji.


Mwisho.

Wednesday, November 22, 2017

TANESCO WATAKIWA WATUMIE NGUZO ZA ZEGE

 Waziri wa Nishati Merdard Kalemani akifurahia jambo wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Bagamoyo na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo kwa kutumia zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo 

 Mkurugenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo kwa kutumia zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo

 Waziri wa Nishati Dk Merdard Kalemani katikati akipata maelezo juu ya uzalishaji wa nguzo kutumia zege


Baadhi ya nguzo zinazozalishwa na kiwanda chaEast Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo

Na John Gagarini, Bagamoyo

SERIKALI imelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza kutumia nguzo za umeme za zege kwenye miradi yake mikubwa ukiwemo ule wa Stieglers Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani ambao mara utakapokamilika utazalisha megawati 2,100 ikiwa ni uzalishaji wa megawati nyingi tangu mwaka 1930 uzalishaji ni megawati 1,451 hadi hivi sasa.

Aidha ifikapo Agosti mwakani nchi itaweza kuzalisha megawati 240 kutoka kwenye mradi wa chanzo cha umeme cha Kinyerezi namba mbili ambapo kuanzia Desemba mwaka huu megawati 30 zitakuwa zinaunganishwa kwenye greti ya Taifa kupitia mradi huo na kutosheleza kwa ajili ya viwanda vilivyopo.

Hayo yalisemwa wilayani Bagamoyo na Waziri wa Nishati Dk Merdard Kalemani alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha East Africa Infrastructure Engineering Ltd kilichopo Kidomole kata ya Fukayosi wilayani Bagamoyo kujionea uzalishaji wa nguzo hizo.

Dk Kalemani alisema kuwa baada ya serikali kupiga marufuku uingizwaji wa nguzo za umeme toka nje na kuruhusu wawekezaji kutengeneza umefika wakati shirika hilo lianze kutumia nguzo za zege kuanzia Desemba mwaka huu kwa kuanzia kewenye mradi huo wa Stiglers Gorge.

“Mradi huo unatarajia kutumia nguzo kati ya 500 hadi 600 na kutokana na ukubwa wa mradi huo lazima tutumie nguzo imara ambazo zinauwezo wa kudumu kwa miaka 70 kuliko kutumia nguzo za miti ambazo zinadumu kwa miaka mitatu kwani ni gharama kubwa ukilinganisha na nguzo za zege,” alisema Dk Kalemani.

“Huwezi kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kutegemea malighafi toka nje ya nchi lazima tutegemee vitu vionavyotengenezwa hapa nchini na mmetekeleza agizo la serikali la awamu ya tano kuanzisha viwanda vyetu kwa kutengeneza malighafi wenywe hakuna sababu ya kuagiza vifaa toka nje manufaa yameanza kuonekana tulipozuia wananchi wengi waliomba kuunganishiwa umeme wengine miaka miwili kisa kukosekana nguzo lakini kwa sasa shida hiyo haipo,” alisema Dk Kalemani.

Alisema kuwa walipozuia nguzo zisitoke nje kulikuwa na watu 29,000 walikuhawajaunganishiwa lakioni baada ya hapo watu 20,000 waliunganishiwa umeme na kama kuna mteja hajaunganishiwa umeme zaidi ya mwezi meneja hajafanya hivyo atachukuliwa hatua changamoto kuchelewesha kuunganishiwa hilo ni tatizo la meneja na atachukuliwa hatua kwani hilo ni tatizo lake.

“Utumiaji wa nguzo zinazotumia miti madhara ni kuharibu vyanzo vya maji na mazingira hivyo kaeni na kamapuni hii mshirikiane ili mradi wa Rufiji utakapoanza kutekelezwa zitumike nguzo za zege ambapo kilometa 36 zitatumia nguzo hizo kwani maeneo ya mbugani huwezi kutumia nguzo za miti au kupitisha umeme chini ya ardhi kwani lengo langu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme,” alisema Dk Kalemani.

Awali akielezea juu ya kiwanda hicho mmiliki wake Otieno Igogo ambaye anashirikiana na Wachina katika uzalishaji wa nguzo hizo alisema teknolojia hiyo ni ya kisasa kwa umeme na mawasiliano ambayo inadumu kwa zaidi ya miaka 70 hivyo kupunguza gharama za kuweka nyingine kama ilivyo kwa zile za miti.

Igogo alisema kuwa gharama za ujenzi wa kiwanda hicho ni kiasi cha shilingi ni bilioni 13 ambapo changamoto inayowakabili ni kukosa soko kwenye sekta za umma na binafsi na kuiomba serikali kuwaunga mkono kwa kutumia nguzo hizo kwenye miradi mbalimbali ya mawasiliano na umeme.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kuendelea kufanikisha upatikanaji wa umeme hasa ikizingatiwa mkoa huo ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi hapa nchini.

Mwanga alisema kuwa wilaya ya Bagamoyo na mkoa una mahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuwa na uwekezaji mkubwa hasa kwenye sekta ya viwanda ambayo ina mahitaji makubwa ya umeme na kusema mipango mbalimbali ya uzalishaji umeme itasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo Mbunge wa Jimbo hilo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo ule wa REA ni miradi muhimu sana ambayo inakwenda kuondoa kabisa tataizo la umeme.

Dk Kawambwa alisema kuwa anampongeza Rais wa awamu ya tano Dk John Magufuli kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji wa umeme ambapo kwa miaka mingi kumekuwa na tataizo la upungufu wa umeme na baadhi ya maeneo kutokuwa na huduma hiyo.
Mwisho.

PWANI WATAKA WATAALAMU WA UWEKEZAJI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Zuberi Samataba ambaye aliongoza ujumbe wa viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China akiongea

Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Zuberi Samataba akielezea jambo kulia ni mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo  


 Baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Pwani kuanzia kushoto Gulmahusein Kifu wilaya ya Kibiti anayefuata Happyness Seneda wilaya ya Kisarawe, Juma Njwayo wilaya ya Rufiji  na Majid Mwanga wilaya ya Bagamoyo

 Baadhi ya washiriki wakijadili baada ya kupokea taarifa ya baadhi ya viongozi na wataalamu waliotembelea nchi ya China 

Na John Gagarini, Kibaha

WATAKA kuwekwa wataalamu wa uwekezaji kwenye kila Halmashauri mkoani humo ili kuwawekea mazingira mazuri ya mawasiliano na wawekezaji.

Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huo wakati wa kupokea taarifa toka kwa timu ya wataalamu na viongozi wa mkoa na Halmasahuri ya wilaya ya Kibaha waliokwenda nchini China.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga alisema kuwa wataalamu hao wakiajiriwa itasaidia kurahisisha wawekezaji kuwa na mtu maalumu ambaye atakuwa anawajibika kwa wawekezaji wanaokuja mkoani humo.

“Kukiwa na dawati maalumu kwa ajili ya wawekezaji itasaidia kupunguza usumbufu wa mwekezaji kuzungushwa wakati wa kupata vibali mbalimbali vya uwekezaji,” alisema Sanga.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kisarawe Happynes Seneda alisema kuwa mtaalamu huyo atakuwa akiwajibika na suala la wawekezaji kwani kwa sasa nchi imehamasisha ujengwaji wa viwanda hivyo kutakuwa na wageni wengi toka nje ya nchi kwa ajili ya uwekezaji.

Seneda alisema kuwa mtaalamu atajua masuala mbalimbali yanayohusiana na uwekezaji kuanzia masuala ya ardhi, upatikanaji wa vibali mbalimbali na kuwa na mawasiliano na sekta wezeshi kwa ajili ya kutatua changamoto kwa wawekezaji.      

Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa madawati ya wataalamu wa uwekezaji kwenye Halmashauri pia sekta wezeshi zinapaswa kuwa na wtu watakaokuwa wanahusika na wawekezaji.

Ndikilo alisema kuwa sekta wezeshi kama vile TANESCO, CHALIWASA, DAWASCO, TARURA, TRA, Polisi na Uhamiaji lazima inakuwa na watu wanaofanya kazi ya kushughulikia wageni.

“Tukiwa na wataalamu wa kudili na wageni itakuwa rahisi kutoa huduma kwa haraka na kwa wakati pia itasaidia kuondoa urasimu wakati wa kuwahudumia wawekezaji ili waweze kutekeleza majukumu yao,” alisema Ndikilo.


Mwisho.

Thursday, November 16, 2017

WENGI WAMWAGA ALBERT NGWADA




Katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Anastazia Amas akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Albert Ngwada kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini.

 Baadhi ya waombolezaji wakiaga mwili wa Ngwada



 Baadhi ya waombolezaji wakiangua vilo baada ya kuuaga mwili wa Ngwada

Vijana wa CCM wakiwa wamebeba jeneza lililokuwa na mwili wa Ngwada 


 Mama wa Marehemu katikati akiwa anabembelezwa wakati wa kuaga mwili wa mwanae kwenda mkoani Iringa kwa ajaili ya mazishi.
 Katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu akitoa taarifa fupi ya marehemu wakati wa kuaga kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini 
Na John Gagarini, Kibaha

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani Anastazia Amas juzi aliwaongoza wanachama na wananchi wa wilaya ya Kibaha kuaga mwili wa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa wa Pwani kuwakilisha Kata ya Pangani Albert Ngwada kwa ajili ya mazishi mkoani Iringa ambaye alifariki dunia Novemba 13 mwaka huu.

Akiongea wakati wa kuaga mwili wa marehemu Ngwada kwenye ofisi za CCM Kibaha Mjini Amas alisema kuwa chama kimepata pigo kutokana na kifo hicho cha mjumbe wa CCM.

Amas alisema kuwa ili kumkumbuka marehemu wanachama wanapaswa kufanya kazi za chama kwa uaminifu na uadilifu ili kuleta maendeleo ndani ya chama na kwa wananchi wa Kibaha kama alivyokuwa Ngwada.

“Natoa pole kwa ndugu na wote walioguswa na msiba huu ambao umewagusa watu wengi na ndiyo maana watu wamejaa hii yote inaonyesha jinsi gani mlivyokuwa mnamkubali kutokana na utendaji wake kikubwa ni kuenzi utendaji wake,” alisema Amas.  

Awali akitoa maelezo mafupi juu ya marehemu katibu wa CCM Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa kutokana na utendaji wake kazi mzuri marehemu alipandishwa cheo kutoka Katibu msadizi wa kata ya Pangani na kuwa kaimu katibu msaidizi wa CCM Kibaha Mjini mwaka 2015

Mdimu alisema kuwa marehemu alitumikia nafasi hiyo kama msiadizi wake hadi mwaka 2017 baada ya kuletwa katibu msaidizi toka Magu ambapo Aprili alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa toka kata ya Pangani nafasi aliyokuwa nayo hadi anafariki dunia.

Awali marehemu alianza kukitumikia chama mwaka 2007 hadi mwaka 2012 alipochaguliwa kuwa katibu kata Pangani hadi 2017 Juni 2015 alipanda daraja na kuwa Kaimu katibu Msaidizi hadi Aprili 2017.

Alisema kuwa mwaka huu mwezi Mei alichaguliwa kuwa Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa kupitia kata ya Pangani  na tarehe 4 Oktoba alipata ajali ya Pikipiki huko eneo la Kidimu majira ya saa 1:30 usiku na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani ya Tumbi na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aidha marehemu alifariki dunia wakati akiendelea na kliniki baada ya kutolewa Hospitali na alitarajiwa kuzikwa jana kwao mkoani Iringa na alizaliwa mwaka 1982.

Mwisho.
















UINGIZAJI MIFUGO TOKA NJE YA NCHI SERIKALI YASHAURIWA






Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imetakiwa iendee kudhibiti uingizaji mifugo kutoka nje ya nchi ili kuepuka magonjwa ambayo yakiingia yataathiri soko la nje ambalo linapato kubwa.

Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na Mwenyekiti wa Chama Cha Waganga Wasaidizi wa Mifugo Tanzania (TAVEPA) Salim Mselem wakati wa mkutano wa kamati kuu ya chama hicho na kusema kuwa lazima kuwe na udhibiti wa magonjwa.

Mselem alisema kuwa suala la udhibiti wa magonjwa ni mgumu sana lakini serikali kwa kushirirkrana na wataalamu wake wanapaswa kudhibiti uingizwaji wa mifugo hapa nchini.

“Hivi karibuni serikali ilivichoma moto vifaranga ambavyo viliingizwa kwenye mpaka wa Namanga ambapo wahusika hawakufuata taratibu za uingizaji mifugo na hizo ndiyo sheria hata kwenye mataifa mengine,” alisema Mselem.

Alisema kuwa ili kudhibiti magonjwa lazima mifugo inayoingia nchini lazima ikaguliwe ili kuangalia kama imepata chanjo na kama haijapata chanjo lazima uharibiwe.

“Magonjwa mengine ni ya hatari sana licha ya kuathiri soko la nje ambapo endapo itabainika mifugo yetu ina maganjwa haitaruhusiwa kwenye nchi za nje hata kwa afya za walaji pia ni hatari sana na hatutakubali nchi yetu kuwa sehemu ya kuuzwa vitu vibaya,” alisema Mselem.

Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa TAVEPA Ephrahim Masawe alisema kuwa kitengo cha ukaguzi wa uingizwaji mifugo kinapaswa kuwa makini ili kuepuka uingizwaji wa mifugo ambayo haijachanjwa.



Masawe alisema kuwa mifugo inayo ingizwa bila ya kuchanjwa ina hatari ya kuingiza magonjwa ambayo ni ya hatari kwa mifugo pamoja na afya za walaji.

Mwisho.




Friday, October 27, 2017

MIILI MIWILI YA WATU WALIOSOMBWA NA MAJI YAPATIKANA


Na John Gagarini, Kibaha

WATU wawili wamefariki dunia kufutaia mvua iliyonyesha juzi mkoani Pwani ambapo miili yao imeweza kugundulika baada ya maji kupungua kwenye mto Mpiji unaotenganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Akithibitisha kuokotwa kwa miili hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Blasius Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilikutwa kando kando ya mto huo ambao ulikuwa umejaa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi.

Chatanda alisema kuwa miili hiyo ilokotwa maeneo tofauti ambapo mwili wa kwanza ulipatikana majira ya saa 2:30 eneo la Muheza kata ya Pangani alitambuliwa kwa jina la Simon Ramadhan mwenye umri kati ya miaka (25) na (30) uliokotwa eneo la mto Mpiji na marehemu alikufa alipokuwa akijaribu kuvuka.

“Mwili wa pili wa Issa Ally (28) ambaye ni mgambo uliokotwa eneo la Kiluvya na inadaiwa kuwa marehemu alisombwa na maji alipokuwa akijaribu kumwokoa mtoto aliyetaka kusombwa na maji na kukutwa kilometa nne toka sehemu aliyozama,” alisema Chatanda.

Alisema kuwa miili yote ya marehemu imehifadhiwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa ajili ya kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

“Nawaomba wananchi kuwa makini wakati wa kuvuka kwenye mito kuwa na subira ili maji yapungue waweze kuvuka na kuendelea na safari zao kwani wasidaharu maji kama ni madogo ambapo yanaweza kuwaletea madhara,” alisema Chatanda.

Mwisho.   
  


SABA WASOMBWA NA MAJI WANUSURIKA


Daraja linalounganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam likiwa limejaa maji

 Baadhi ya wananchi wakifuatilia zoezi la uokoaji watu waliosombwa na maji ambao walipanda kwenye miti

 Moja ya kijana aliyenusurika Silas Moshi baada ya kusombwa na maji mara baada ya kuokolowa

 Dada ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja baada ya kuokolewa akiwa amepoteza fahamu akipakiwa kwenye gari la polisi kwa ajili ya huduma ya kwanza.



 Kijana Mohamed Kitindi aliyenusurika baada ya kusombwa na maji 

 Furaha Mwaipopo moja ya watu walionusurika baada ya kusombwa na maji na kupanda kwenye mti


 Moja ya watu walionusurika akihojiwa na polisi baada ya kunusurika 

 Kened Meshaki ambaye alishika nguzo ya bango huku mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa zaidi ya masaa matatu akiwa ameshikwa mkono na polisi kwa ajili ya kwenda kupatiwa huduma ya kwanza


Na John Gagarini,Kibaha

WATU saba wamenusurika kifo baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka huku wakiwa wameshikana mikono ambapo walijinusuru kwa kupanda kwenye miti kabla ya kuokolewa na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani.

Aidha kati ya watu hao mmoja alikuwa akininginia kwa kujishika kwenye bomba la bango la matangazo huku mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa masaa zaidi ya huku akiwa anaomba msaada wa kuokolewa bila mafanikio.

Watu walionusurika ni pamoja na Kened Meshaki, Mohamed Kitindi, Silas Moshi Henry Francis na mwanamke mmoj ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja ambao wote walikimbizwa hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Pwani.

Tukio hilo lilitokea jana eneo la Maili Moja wilayani Kibaha kwenye daraja linalotenganisha kati ya mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Pwani na kusababisha daraja kujaa maji na kusababisha magari na watu kushindwa kuvuka upande wa pili.

Daraja hilo ambalo linapita kwenye mto Mpiji lilikuwa halipitiki na kusababisha watu na abiria kushindwa kuvuka upande wa pili kutoka Maili Moja wilayani Kibaha na upande mwingine Kiluvya wilaya ya Ubungo.

Kutokana na daraja hilo kushindwa kupitika abiria wa mabasi wameshindwa kuendelea na safari zao za kwenda mikoani na maeneo mengine yanayopita kwenye barabara ya Morogoro.

Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la tukio hilo ofisa habari na uhusiano wa Jeshi la uokoaji Harison Mkonyi alisema kuwa zoezi la ukoaji limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wameweza kuwaokoa watu hao wakiwa salama.

Mkonyi alisema kuwa wamefanikiwa kuwaokoa watu hao kwa kushirikiana na wadau wengine ambao walijitosa kwenye maji hayo ambayo yalikuwa mengi na kulifunika kabisa daraja hilo na kusababisha kushindwa kupitika.

“Tunawashukuru wadau mbalimbali vikiwemo vikosi vya majeshi ya Polisi, Magereza, JWTZ na wananchi ambao walionyesha ushirikiano wa hali ya juu kuwanusuru watu hao akiwemo mwanamke mmoja,” alisema Mkonyi.

Mwisho.