Thursday, August 3, 2017

PICHA YA NDEGE WAPATA ENEO UJENZI SHULE YA SEKONDARI

Na John Gagarini,Kibaha

KATA ya Picha ya Ndege imepata eneo lenye ukubwa wa hekari 11 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ambapo kwa sasa wanafunzi wanaotoka kata hiyo wanasoma shule ya sekondari ya kata kwenye mtaa wa Mkuza.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata hiyo Robert Machumbe wakati wa mkutano wa kata uliofanyika kwenye shule ya Msingi ya Lulanzi na kusema kuwa eneo hilo limepatikana kutokana na jitihada zake na wananchi.

Machumbe alisema kuwa licha wanafunzi wanaotoka kwenye kata yake wanasoma kwenye mazingira magumu kwani darasa moja linawanafunzi 450 hali ambayo inafanya usomaji kuwa mgumu.

“Watoto wetu wanapata shida kwanza kule ni mbali na pia madarasa yao yamejaa wanafunzi hivyo hupunguza ari ya usomaji na ufaulu kuwa mdogo,” alisema Machumbe.

Naye Thomas Raymond alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo itakuwa mkombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye kata hiyo ambayo ni mpya ikiwa haina shule yake ya sekondari.
Raymond alisema kuwa wao wako tayari kuchangia ujenzi wa shule hiyo mara wakati utakapofika ili kuhakikisha shule hiyo inajengwa haraka kwenye kata yao.

Mwisho.


HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAOMBWA KUTENGA FEDHA KWA WATU WENYE ULEMAVU

Na John Gagarini, Kibaha

WADAU wa watu wenye ulemavu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wameiomba Halmashauri hiyo kutenga asilimia moja ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukabili changamoto za ulemavu.

Hayo yalisemwa na Methew Chungu mwezeshaji wa  mafunzo yaliyoandliwa na Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Kibaha Mjini kwa wadau wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu.

Chungu alisema kuwa mapato hayo yangesaidia kuwapatia huduma mbalimbali watu wenye ulemavu zikiwemo za kiafya, elimu, kiuchumi na huduma nyingine za kiutu.

Naye katibu wa SIVYAWATA Kibaha Mjini Happiness Matagi alisema kuwa kwa sasa changamoto za upataji huduma kwa watu wenye uelemavu zimepungua ambapo kumwona daktari kwa ni bure.

Matagi alisema kuwa kupitia kituo chao cha watu wenye ulemavu kilichopo Kwa Mfipa wanatoa huduma mbalimbali za kiafya hasa kwa wale walemavu wa viungo pamoja na shughuli za ujasiriamali.

“Pale watu wenye ulemavu wanafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuma, kushona nguo na mradi wa matofali ambao uko mbioni kuanza lengo kuwakwamua watu wenye ulemavu ili wasijione wanyonge na kuachana na tabia ya kuomba ambayo itawafanya washindwe kujitegemea,” alisema Matagi.

Kwa upande wake mwakilishi wa mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dk Mariamu Mgaya alisema kuwa watu wenye ulemavu wamekuwa wakisaidia ili kuhakikisha wanapata huduma za afya bila ya usumbufu kwa kuwapa kipaumbele.

Akijibu baadhi ya hoja ofisa mipango wa Halmashauri ya Mji Kibaha Amkauane Ngilangwa alisema kuwa katika bajeti iliyopitishwa watu wenye ulemavu wametengewa kiasi cha shilingi milioni 10.


Ngilangwa alisema kuwa pia wanapatiwa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuta ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi albino ili ngozi zao zisiharibike na fimbo kwa ajili ya wasioona. 

UCHAGUZI CHAMA CHA NETIBOLI PWANI

Na John Gagarini, Kibaha

CHAMA Cha Netiboli mkoa wa Pwani (CHANEPWA) kinatarajia kufanya uchaguzi wake Agosti 5 mwaka huu.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na ofisa michezo mkoa wa Pwani Grace Bureta na kusema kuwa uchaguzi huo utafanyika Tanita mjini Kibaha.

Bureta alisema kuwa mchakato wa uchaguzi huo unaendelea ambapo usaili unatarajiwa kufanyika wiki hii ili kuwapitisha wadau watakaogombea nafasi mbalimbali.

“Mchakato unaendelea na tunasubiri taarifa kutoka kwenye wilaya za mkoa wetu ili watuletee majina ya wagombea na baadaye tufanye usaili wiki hii ili kuwapata wale wenye sifa,” alisema Bureta.
Alisema kuwa fomu zilianza kutolewa tangu Aprili lakini baadye uchaguzi huo uliahirishwa kutokana na sababu mbalimbali ambapo sasa unafanyika kesho endapo taratibu zitakuwa ziko sawa.

“Fomu zote zinatakiwa zirejeshwe kwa maofisa michezo wa wilaya ambao nao wataziwasilisha mkoani kwa ajili ya taratibu za uchaguzi huo ambao utawaweka madarakani viongozi wapya kwa kipindi cha miaka minne,” alisema Bureta.

Aidha alisema kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kusimamiwa na kamati ya michezo ya mkoa na kuwataka wagombea hao kutimiza taratibu ili wawanie nafasi hizo.


Mwisho. 

MWIGULU ATAKATAARIFA ZA WATANZANIA ZIUNGANISHWE MTANDAONI


                                     Na John Gagarini, Kibaha

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba ametaka taarifa za Watanzania ziunganishwe kwenye mtandao tangu wanapozaliwa ili wasipate usumbufu wa kupata barua za utambulisho wanapotaka huduma mbalimbali.

Aliyasema hayo wakatia alipotembelea jengo jipya la kisasa la vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kusema hakuna haja ya mtu kila anapoomba huduma fulani awe na barua ya utambulisho toka kwenye mtaa anaoishi.

Nchemba alisema kuwa kwa sasa mifumo inakwenda kisasa na mtu anapotaka huduma fulani wanakwenda kwenye mtandao na kupata taarifa zote za muhusika.

“Mfano mtu anataka paspoti, leseni, kusajili biashara, laini za simu na huduma nyingine hapaswi kuwa na mabarua kwa kila huduma anayoitaka bali wanaangalia tu kwenye mifumo hii na kuzipata taarifa za mtu,” alisema Nchemba.

Alisema kuwa uunganishaji wa taarifa za wananchi na kuwa na utambulisho wa aina moja utasaidia kupata taarifa na itaonyesha kama ni dereva kujua ni makosa gani aliyokwisha kuyafanya hivyo ni rahisi kumdhibiti.

 “Mifumo hii ya kimtandao itasaidia sana kuhuisha huduma nyingi ambazo mtu anapaswa kwenda kwenye ofisi mbalimbali bali anaweza kutumia ofisi moja kupata taarifa zozote zinazotakiwa,” alisema Nchemba.

Aidha alisema kuwa taarifa hizo zitasaidia hata kupunguza kuwabaini raia wageni ambao wanaingia nchini kinyemela ambao hawaeleweki wako kwa ajili ya madhumuni gani.

Naye kaimu mkurugenzi wa uzalishaji wa Vitambulisho Alfonce Malibiche alisema kuwa ujenzi huo umefikia hatua za mwisho na wanatarajia utakamilika mwishoni mwa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao.

Malibiche alisema kuwa mara ujenzi huo utakapokamilika vitambulisho vya uraia vitakuwa vikizalishwa hapo ambapo kwa sasa ujenzi huo uko mwishoni.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka aliomba serikali ikitoa ajira izingatie wakazi wa wilaya hiyo na mkoa wa Pwani ili iwe manufaa kwa kujengwa ofisi hizo.

Koka alisema kuwa uzingatiaji wa kuajiri vijana na wataalamu kutoka kwenye eneo husika utaleta manufaa makubwa kwa mkoa huo ambao unainukia kwa kasi katika uwekezaji ukiwemo wa viwanda.

Mwisho.

KIJANA AIGIZA SAUTI YA KIKE AVAA DERA NA HIJABU BODABODA AINGIA MKENGE


Na John Gagarini, Kibaha

KIJANA mmoja anayekadiriwa kuwa na miaka (19) mkazi wa Mbagala Maji Matitu amejikuta yuko kwenye wakati mgumu baada ya kukutwa akiwa amevaa nguo za kike aina ya dera na kusababisha taharuki kwa wakazi wa Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Kibaha mwenyekiti wa mtaa wa Picha ya Ndege Joseph Zambo alisema kuwa kijana huyo alikuwa akiwasiliana na mtu akijifanya kuwa yeye ni mwanamke.

Zambo alisema kuwa kijana huyo alifika kwenye mtaa wake Agosti 2 majira ya sa 4:30 asubuhi akimfuata mtu waliokuwa wakiwasiliana naye kwa njia ya simu ambaye inadaiwa kuwa ni dereva bodaboda.

“Watu hawa walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na kijana huyo alikuwa akiigiza sauti ya kike na dereva bodaboda alijua fika kuwa aliyekuwa anawasiliana naye ni mwanamke,” alisema Zambo.

Alisema kuwa dereva bodaboda huyo alimwona kijana huyo kupitia ukurasa wake wa facebook ambapo ulipambwa na picha za msichana hali ambayo ilimfanya avutiwe naye.

“Mawasiliano yalianza kama siku tatu zilizopita na walikubaliana na ndipo bodaboda huyo alimwambia njoo Picha ya Ndege Kibaha lakini kijana huyo alipitiliza hadi Kongowe na ilibidi arudi ashukie Picha ya Ndege na alimwelekeza akishuka apande bodaboda ili aende kwake eneo la Sofu,” alisema Zambo.

Aidha alisema kuwa aliposhuka waendesha pikipiki walikuwa wakimfuatilia na wlimwona amevaa dira na usoni kajifunga kitambaa ambacho kiliacha wazi macho tu kama vile ninja akapandishwa kwenye pikipiki na kuanza safari ya kwenda kwa mtu wake.

“Wakiwa njiani upepo ulipuliza na dereva wa bodaboda akashangaa kuona miguu ya kiume lakini amevaa viatu vya kike akashtuka na kugeuza pikipiki kule alikotoka na ndipo madereva bodaboda walipojaa na kuanza kumzonga hali iliyowabidi wamlete ofisini kwangu na ilikuwa tafrani kubwa huku wengine wakitaka kumpiga wakidai ni mwizi wa pikipiki,” alisema Zambo.

Alibainisha kuwa baada ya kumfikisha walimfunua na kukuta kuwa ni mwanaume na kuanza kumhoji ndipo aliposema kuwa alikuja Kibaha kuja kuchukua hela na haikujulikana alikuja kuzichukua hizo fedha kwa njia gani.

“Zogo lilizidi pale huku bodaboda wakitaka kumpiga ndipo ikabidi tuchukue gari na kumpeleka polisi kwa ajili ya usalama wake na kueleza ni kwa sababu gani alijifanya mwanamke na fedha hizo anazichukua kwa njia gani,” alisema Zambo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa atalitolea taarifa tukio hilo baada ya kutoka kwenye msafara wa kiongozi.


Mwisho.   

Thursday, July 27, 2017

AKIMAMA WAFANYABIASHARA WALALAMIKA KUNYANYASWA


                                    Na John Gagarini, Kibaha

MTAA wa Maili Moja umesema utawafuatialia na kuwachukulia hatua mgambo ambao waliwadhalilisha akina mama wafanyabiashara ndogo ndogo kwa kuwadai rushwa ya ngono kwa madai kufanyabiashara kwenye eneo ambalo haliruhusiwi.

Akizungumza kwenye mkutano wa mtaa mwenyekiti wa Mtaa wa maili Moja Athuma Mkongota alisema kuwa baadhi ya akinamama walilalamika ofisini kwake kuwa walitakiwa watoe penzi ili wasitozwe faini kwa kudaiwa kufanya biashara kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Mkongota alisema kuwa jambo la kushangaza akinamama hao waliokuwa wakifanyabiashara nje ya eneo la Hifadhi ya Barabara ambapo waliondolewa kufuatia kubomolewa soko la zamani la Maili Moja.

“Hawa mgambo walifanya makosa kuwanyanyasa akinamama hawa hata kama walikuwa na makosa taratibu za wanaokiuka sheria sizipo kwanini wadai mapenzi pia walikuwa hawafanyibiashara kwenye eneo lililokatazwa hivyo tutawatafuta na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua,” alisema Mkongota.

Mkongota alisema kuwa baada ya wakinamama hao kuondolewa eneo lililokatazwa la hifadhi ya barabara ambalo liko jirani na stendi walienda kwenye barabara za mitaa na kuendelea kufanyabiashara lakini mgambo hao waliwafuata na kuwakamata huku wakimwaga vyakula na matunda waliyokuwa wakiyauza.

“Baadhi ya akinamama walifika ofisini na kudai kuwa baadhia ya mgambo walikuwa wakiwataka kimapenzi ili wasiwapige faini wakidai kuwa wanachafua mazingira jambo hili halikubaliki kwani tutawatafuta na wakibainika watepelekwa sehemu husika kwnai kuna baadhi wanajifanya mabwana afya,” alisema Mkongota.

Kwa upande wake Mwanahamisi Shomary ambaye ni muuzaji wa samaki alisema kuwa tangu waondolewe kwenye eneo la stendi na kuhamia kwenye barabara za mitaa wamekuwa wakisumbuliwa na mgambo hao.

Shomary alisema kuwa mgambo hao wamekuwa kero kubwa kwani wanatunyanyasa sana huku wakichukua bidhaa zetu na kuziharibu ambapo inabidi tujitafutie ili tuweze kurejesha mikopo tuliyokopa.


Mwisho.   

WAASWA KUTUMIA VITUO VYA MAFUNZO

                                      Na John Gagarini, Kibaha

WALIMU wakuu wa shule za msingi, sekondari na vyuo nchini wameshauriwa kuwapeleka wanafunzi wao kwenye vituo vya mafunzo badala ya kuwapeleka kwenye sehemu za starehe.

Ushauri huo umetolewa na makamu mwenyekiti wa wataalamu wasaidizi wa mifugo nchini Tavepa Ephrahim Masawe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Masawe ambaye pia ni mkurugenzi wa shamba darasa Kibaha akizungumzia juu ya kilimo cha kisasa alisema kuwa ziara za safari ni vema zikawa za kujifunza kuliko kujifurahisha.

“Kwenye mafunzo hujifunza mambo mengi kuliko kwenda kwenye sehemu ambazao hazina faida kwani ujuzi unaweza kumsaidia mtu kuliko kufanya vitu visivyo na faida,” alisema Masawe.

Naye moja ya wanafunzi kwenye shamba darasa mkazi wa Mbweni Jijini Dar es Salaam Hilda Ngowi akiezea kilicho msukuma kwenda hapo kujifunza ni kutaka kupata ujuzi wa ufugaji wa kuku.

Ngowi alisema ushauri juu ya shule na vyuo kuwapeleka wanafunzi kwenye sehemu za mafunzo kama hayo alisema kuwa sehemu za mafunzo ni muhimu kwa vijana.

Mwisho.