Na John Gagarini, Rufiji
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Mpalange Kijiji cha
Ikwiriri Kaskazini wilayani Rufiji mkoani Pwani Bakari Mpawane amenusurika kifo
baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika.
Mpawane alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 19
mwaka huu majira ya saa 2 usiku akiwa dukani kwake ambapo alipigwa risasi
mkononi na tumboni.
Alisema kuwa mtu aliyempiga alikuwa amepakizwa
kwenye pikpiki akampiga kisha wakatokomea kusikujulikana kwa kutumia pikpiki
hiyo ambayo namba zake hazikuweza kutambulika mara moja.
“Watu hao ambao walikuwa wamepakizana kwenye
pikipiki walifika hapo na mmoja wao kumwita jina lake mara nikashtukia napigwa
risasi ambazo hata hivyo namshukuru Mungu ziliniparaza tu na hazikuweza
kuniletea madhara makubwa ambayo yangehatarisha uhai wangu,” alisema Mpawane.
Aidha alisema kuwa anamshukuru Mungu na sasa
anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri hata hivyo ana hofu na
anafikiria atakaporudi kwake baada ya matibabu ataishije baada ya kunusurika
kwenye tukio kubwa na la uuaji kama hilo.
“Naomba serikali na jeshi la polisi liweke mikakati
kabambe ili kuvunja ngome za kiuhalifu na mtandao unaomaliza hasa viongozi bila
kujua chanzo ni masuala ya kisiasa ama nini,”alisema Mpawane.
Akizungumza
mara baada ya kwenda kumtembelea mwenyekiti huyo katika kituo cha afya cha Mchukwi
anapopatiwa matibabu Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo
alisema kuwa hilo ni tukio la tatu kwa mwezi mmoja likiwemo lililotokea machi
13 mwaka huu kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo wilayani hapa, Hemed
Njiwa (45) kuuwawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani na tukio lililohusisha
kifo cha OCCID.
Ndikilo alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watu hao
usiku na mchana hadi kuhakikisha wanawakamata ili waweze kuchukuliwa hatua za
kisheria kuhusiana na tukio hilo.
“Tutawasaka na hatafanikiwa kwa mipango
yao waliojiwekea tumejidhatiti na tutahakikisha tunategua mipango yao na
kurejesha amani kwa wananchi,”alisema Ndikilo.
Aidha aliwashukuru wahudumu wa afya katika kituo
cha afya cha Mchukwi kwa kuokoa maisha ya mwenyekiti huyo pamoja na kutoa
huduma nzuri kwa majeruhi na wagonjwa wengine wanaofikishwa hapo kupata
matibabu.
Naye Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga,aliomba
ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa polisi mara wanapopata wasiwasi wa watu
wanaoingia kwenye maeneo yao.
Kamanda Lyanga alisema ameletwa mkoa wa Pwani
kutoka Simiyu kwa ajili ya kufanya kazi na jambo kubwa analohitaji ni ushirikiano
na jamii ili waweze kupunguza matukio yanayotikisa ikiwemo la kuuwa wa
wenyeviti wa vitongoji,watendaji na wenyeviti wa vijiji.
Mwisho