Monday, March 20, 2017

MLANDIZI QUEENS YAPONGEZWA KWA KUWA MABINGWA NCHINI

Na John Gagarini, Kibaha

SHIRIKISHO la Soka Nchini (TFF) limeombwa kuhamasisha uanzishwaji wa mashindano ya soka kwa wanawake kwa ukanda wa Afrika Mashariki ili kuendeleza vipaji vya wanawake kimataifa.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na mratibu wa timu ya Mlandizi Queens Florence Ambonisye wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa huo na kuwa mabingwa wa kihistoria wa kwanza kwa soka la Wanawake Tanzania.

Ambonisye alisema kuwa kwa kuwa kuna mashindano ya soka la wanawake ngazi ya nchi na nchi kuna haja ya kuwa na mashindano ya vilabu kama ilivyo kwa wanaume.

“Imefika wakati TFF kuhamasisha kuanzishwa mashindano ya vilabu vya soka la wanawake ili kuinua soka la wanawake hapa nchini kwani itasaidia kuwa na timu bora kutokana na kushindana na wenzao wa nchi zingine,” alisema Ambonisye.

Ambonisye ambaye pia ni katibu wa chama cha soka la wanawake mkoa wa Pwani alisema kuwa mashindano hayo pia yatasaidia kuimarisha timu ya soka ya Taifa ya wanawake Twiga Stars.

“Tukianzisha mashindano ya nchi za Afrika Mashariki tutakuwa na timu ya Taifa ya wanawake imara kwani watapata uzoefu mkubwa hivyo nchi itaweza kufika mbali kwenye mashindano ya Kimataifa,” alisema Ambonisye.

Aidha alisema kuwa washindi wa mashindano hayo watakuwa hawana mashindano yoyote hadi mwakani lakini wangekuwa na mashindano ya vilabu vya nchi nyingine ingewasaidia sana kuendeleza vipaji vyao ambapo kwa sasa watakaa muda mrefu bila ya kucheza.

Naye mgeni rasmi kwenye sherehe hizo Ivan Chenga ambaye ni katibu msaidizi wa chama cha soka wilayani Kibaha Ivan Chenga alisema kuwa timu hiyo haitakiwi kubweteka kwa kutwaa ubingwa huo.

Chenga alisema kuwa katika kipindi hichi wanapaswa kuendelea na mazoezi na kuachana na vitendo ambavyo vitasababisha kushusha viwango vyao.

Kwa upande wake mwakilishi wa chama cha soka mkoa wa Pwani COREFA Simon Mbelwa alisema kuwa timu hiyo imeleta mafanikio makubwa kwa kuweka historia kwa kuitoa Pwani kimasomaso kwa kutwaa ubingwa huo.

Mbelwa alisema kuwa timu za soka za wanaume za mkoa wa Pwani zimekuwa zikifanya vizuri kwenye ligi Kuu lakini hazijawahi kutwaa ubingwa lakini hii ya wanawake imeweza kuleta kombe na kuonyesha mfano mzuri.

Mwisho.

 Diwani wa Kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala akibusu kombe la soka la Wanawake lililotwaliwa na timu ya soka ya wanawake ya Mlandizi Queens wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo zilizofanyika Mlandizi hivi karibuni.

 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Mlandizi Queens wakiwa wamepozi wakati wa sherehe za kuwapongeza baada ya kufanikiwa kuwa mabingwa wa soka la wananwake nchini.

 Baadhi ya viongozi wa timu ya Mlandizi Queens wakiwa wametulia wakifuatilia wakati wa sherehe za kuipongeza timu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa soka la wanawake nchini hivi karibuni.

 Wachezaji wa timu ya Mlandizi Queens wakicheza wakati wa sherehe ya kuwapongeza kwa kuwa mabingwa wa soka la wanawake nchini.

 Wachezaji wa Mlandizi Queens wakicheza.

 Wachezaji wa Mlandizi Queens wakicheza pamoja na viongozi wao wakati wa sherehe ya kuwapongeza iliyofanyika Mlandizi hivi karibuni.

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha Ivan Chenga akipokea kombe toka kwa kepteni wa Mlandizi Queens Mwanahamis Gaucho katikati ni diwani wa kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala akishuhudia. 

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha KIBAFA Ivan Chenga akiongea wakati wa sherehe ya kuipongeza timu ya Mlandizi Queens kwa kuwa mabingwa wa soka la wanawake nchini

 Katibu Msaidizi wa Chama cha soka wilaya ya Kibaha KIBAFA Ivan Chenga akinyanyua kombe kama ishara ya pongezi kwa timu ya soka ya wanawake ya Mlandizi Queens kulia ni mjumbe wa Chama caha Soka mkoa wa Pwani COREFA Simon Mbelwa na wakwanza kulia ni Mwanahimis Gaucho Kapteni wa timu hiyo  


No comments:

Post a Comment