Tuesday, March 28, 2017

MBUNGE AZINDUA UJENZI WA UZIO WA KITUO CHA AFYA



 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha shehena na saruji mifuko 500 kwa ajili ya uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani

 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa amebeba saruji ambayo itatumika kwenye ujenzi wa uzio wa kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani 







 Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizindua ujenzi wa uzio wa Kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani


Na John Gagarini, Kibaha

KITUO cha Afya cha Mlandizi kimeanza mchakato wa kuelekea kuwa Hospitali ya wilaya kwa kuanza ujenzi wa uzio ambapo Mbunge wa Jimbo la Kibaha 
Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani Hamoud Jumaa amewataka wafadhili mbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio huo ambao utagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 200.

Akizungumza na waandishi wa habari Mlandizi wakati akizindua ujenzi huo mbunge huyo alisema kuwa wameanza kuboresha huduma zinazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uzio huo ikiwa ni moja ya vigezo vinavyotakiwa kufikia hadhi hiyo.

Jumaa alisema kuwa Kituo hicho cha afya ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina wakazi 70,000 na wilaya jirani za Bagamoyo na miji ya Chalinze na Kibaha wanapata huduma hapo.

“Mpango huu nimeuanzisha kwa jitihada zangu binafsi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo hadi sasa nimepata mifuko 500 ya saruji, kokoto lori saba mchanga, mchanga na tani moja ya nondo ambavyo vitasaidia katika ujenzi wa uzio huu tunaomba wadau wengine waendelee kutusaidia,” alisema Jumaa.

Alisema kuwa kutokana na kituo hicho cha afya kuwa tegemeo kubwa kwa wameona kuna haja ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili waweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi watakaokuwa wanapata huduma hapo.

“Tumekubaliana vitongoji 26 na madiwani sita watoe 240,000 huku mfuko wa jimbo ukitoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya tofali za uzio ambao utasaidia kuondoa uingiaji holela wa watu bila ya sababu za msingi ndani ya eneo la Kituo cha afya,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mlandizi Eufrasia Kadala alisema kuwa wataungana na Mbunge huyo kuhakikisha wanafanikisha ujenzi huo ili kuboresha kituo hicho cha afya.

Kadala alisema kuwa kutokana na kutokuwa na uzio kumekuwa na mwingiliano wa watu kuingia kiholela hasa kutokana na kituo hicho kuwa jirani na makazi ya watu. 

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Mlandizi Tatu Jalala alisema kuwa waliupokea mkono mpango huo na kuupeleka kwa jamii kwa lengo la kumuunga mkono mbunge wao.

Jalala alisema kuwa wanaendelea kuihamasisha jamii ili iweze kuchangia ujenzi huo wa uzio ukamilike kwa wakati lengo likiwa ni kufanikisha harakati za kuwa Hosptali ya wilaya.

Mwisho. 

No comments:

Post a Comment