Thursday, March 23, 2017

MWENYEKITI ANUSURIKA KIFO RISASI ZAMJERUHI

Na John Gagarini, Rufiji

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Mpalange Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini wilayani Rufiji mkoani Pwani Bakari Mpawane amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na watu wasiofahamika.

Mpawane alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 19 mwaka huu majira ya saa 2 usiku akiwa dukani kwake ambapo alipigwa risasi mkononi na tumboni.

Alisema kuwa mtu aliyempiga alikuwa amepakizwa kwenye pikpiki akampiga kisha wakatokomea kusikujulikana kwa kutumia pikpiki hiyo ambayo namba zake hazikuweza kutambulika mara moja.

“Watu hao ambao walikuwa wamepakizana kwenye pikipiki walifika hapo na mmoja wao kumwita jina lake mara nikashtukia napigwa risasi ambazo hata hivyo namshukuru Mungu ziliniparaza tu na hazikuweza kuniletea madhara makubwa ambayo yangehatarisha uhai wangu,” alisema Mpawane.

Aidha alisema kuwa anamshukuru Mungu na sasa anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea vizuri hata hivyo ana hofu na anafikiria atakaporudi kwake baada ya matibabu ataishije baada ya kunusurika kwenye tukio kubwa na la uuaji kama hilo.

“Naomba serikali na jeshi la polisi liweke mikakati kabambe ili kuvunja ngome za kiuhalifu na mtandao unaomaliza hasa viongozi bila kujua chanzo ni masuala ya kisiasa ama nini,”alisema Mpawane.

Akizungumza mara baada ya kwenda kumtembelea mwenyekiti huyo katika kituo cha afya cha Mchukwi anapopatiwa matibabu Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi  Evarist Ndikilo alisema kuwa hilo ni tukio la tatu kwa mwezi mmoja likiwemo lililotokea machi 13 mwaka huu kwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo wilayani hapa, Hemed Njiwa (45) kuuwawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani na tukio lililohusisha kifo cha OCCID.

Ndikilo alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watu hao usiku na mchana hadi kuhakikisha wanawakamata ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria kuhusiana na tukio hilo.

“Tutawasaka na hatafanikiwa  kwa mipango yao waliojiwekea tumejidhatiti na tutahakikisha tunategua mipango yao na kurejesha amani kwa wananchi,”alisema Ndikilo.

Aidha aliwashukuru wahudumu wa afya katika kituo cha afya cha Mchukwi kwa kuokoa maisha ya mwenyekiti huyo pamoja na kutoa huduma nzuri kwa majeruhi na wagonjwa wengine wanaofikishwa hapo kupata matibabu.

Naye Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Onesmo Lyanga,aliomba ushirikiano wa wananchi kutoa taarifa polisi mara wanapopata wasiwasi wa watu wanaoingia kwenye maeneo yao.

Kamanda Lyanga alisema ameletwa mkoa wa Pwani kutoka Simiyu kwa ajili ya kufanya kazi na jambo kubwa analohitaji ni ushirikiano na jamii ili waweze kupunguza matukio yanayotikisa ikiwemo la kuuwa wa wenyeviti wa vitongoji,watendaji na wenyeviti wa vijiji.


Mwisho 

No comments:

Post a Comment