Thursday, March 23, 2017

MADEREVA SABA WAPORA FEDHA NA SIMU WAJERUHIWA

Na John Gagarini, Kibaha

MADEREVA saba wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kisha kuwapora fedha kiasi cha shilingi 920,000 baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kufunga barabara ya Kilwa kwa kutumia magogo.

Aidha watu hao licha ya kuwajeruhi na kuwapora fedha pia waliwaibia madereva hao simu saba na kutoweka kusikojulikana.

Kwa Mujibu wa taarifa zilizotolewa mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Onesmo Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 majira ya saa saba usiku katika kijiji cha Kitembo kata ya Mchukwi wilaya ya Kibiti.

Kamanda Lyanga amesema kuwa watu hao sita wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi walikuwa na silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga na marungu na walizitumia kuwajeruhi madereva hao.

Amesema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusina na tukio hilo na wanaendelea na msako kuhakikisha watu hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria waweze kujibu tuhuma hizo.

Aidha amewataja madereva waliojeruhiwa kwa mapanga kuwa ni Issa Juma (26) mkazi wa Jijini Dar es Salaam aliyejeruhiwa shavu la kulia, Badru Uwesu (31) mkazi wa Kisemvule Mkuranga aliyejeruhiwa shavu la kulia na mgongoni, Edward Safari (37) mkazi wa Morogoro.

Amewataja wengine kuwa ni Ramadhan Ally (34), Nasoro Mohamed (26), Kassimu Omary (36), Khalifa Mohamed wote wakazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam ambapo majeruhi wote walitibiwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mchukwi na kuruhusiwa kuondoka.

Katika tukio lingine ngombe 102 wamekufa baada ya kunywa maji ambayo yanasadikiwa kuwa hayafai kutumika kwa matumizi yoyote kwenye machimbo ya kokoto.

Kamanda Lyanga amesema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri kwenye Kijiji cha Pongwe Msungura Chalinze wilayani Bagamoyo.

Mwisho.  

  

No comments:

Post a Comment