Monday, May 23, 2016

MABILIONI YATENGWA SEKTA YA ELIMU KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
KATIKA kukabiliana na changamoto za elimu  wilaya ya  Kibaha mkoani Pwani imetenga bajeti ya shilingi bilioni 1,789,828,891 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa shule za sekondari kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba na kusema kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kupunguza changamoto mbalimbali kwenye shule za sekondari wilayani humo.
Kihemba amesema kuwa kabla ya bajeti hiyo kupitishwa jumlaya shilingi milioni 640,424,679 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika shule za sekondari za Zogowale na Hosteli ya shule ya sekondari ya Pangani.
Amesema kuwa pia fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa matundu 20 ya vyoo, madarasa matano na nyumba moja ya mwalimu katika shule za sekondari za Pangani, Simbani na Ruvu Station.
Akizungumzia upande wa shule za msingi amesema kuwa katika bajeti hiyo zimetengwa kiasi cha shilingi milioni 943,144,394 kwa ajili ya miradi ya maendeleo  kwa elimu ya msingi.
Aidha amesema kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha ya 2015/ 2016 wilaya ilipokea kiasi cha shilingi milioni 140,254, 154 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mwalimu Kumba, vyumba 9 vya vya madarasa katika shule za Visiga, Lumumba, Bamba na Matuga.
Amebainisha kuwa fedha hizo pia zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo na ununuzi wa madawati 46, meza 4 na viti 6 kwa ajili ya shule ya Msingi ya Matuga.

VIONGOZI SIMBA WAWAJIBIKE


Na John Gagarini, Kibaha

UONGOZI wa Timu ya Soka ya Simba ya Jijini Dar es Salaam wametakiwa kuwajibika kutokana na matokeo mabaya ya timu kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Voda Com iliyomalizika mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha msemaji wa Tawi la Simba Kibaha maarufu kama “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa viongozi hao wamekuwa wakiwawajibisha wachezaji pale wanapofanya vibaya hivyo na wao lazima wawajibike kwa hilo.

Lardhi alisema kuwa timu hiyo imefanya vibaya kwenye misimu minne na kuifanya timu hiyo ishindwe kushiriki michuano ya kimataifa kutokana na matokeo mabaya ambapo kwa msimu huu imeshika nafasi ya tatu.

“Timu ina vitengo vingi na kamati mbalimbali hivyo kama kuna kiongozi ambaye alizembea kwenye kitengo chake na kufanya timu ifanye vibaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake anapaswa kuwajibika kwa kuachia ngazi,” alisema Lardhi.

Alisema kuwa inasikitisha kuona timu inafanya vibaya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu mwenendo wake haukuwa mzuri na kufanya timu kupata matokeo mabaya huku ikiwa imetambiwa na mtani wake Yanga kw akufungwa michezo yote.

“Tumechoka kusemwa vibaya na watani wetu hii ni fedheha kwetu tunaomba kiongozi yoyote ambaye alisababisha timu kufanya anapaswa kuwajibika kwa kuachia ngazi au kuondolewa,” alisema Lardhi.

Aidha alisema kuwa anawapongeza wanachama na wapenzi wa timu yao kwa kuwa na uvumilivu kwani kwa kipindi cha miaka minne timu yao imekuwa ikifanya vibaya lakini wametulia wakiamini kuwa timu itapata matokeo mazuri lakini imekuwa kinyume.

“Ligi imeshakwisha kila kiongozi atoe ripoti yake na kuonyesha uzaifu ulikuwa wapi ili kujipanga na msimu mwingine wa ligi ijayo ili timu ifanye vizuri na si kushika nafasi ambazo haiipi timu kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Lardhi.

Aliutaka uongozi kuwa makini katika usajili kwa kusajili wachezaji wenye uwezo na kuacha kusajili wachezaji wasio na uwezo kwani Simba inahitaji wachezaji wenye uwezo na si kila mchezaji anastahili kuichezea Simba kama ilivyokuwa kwa msimu huu kuwa na wachezaji wenye uwezo mdogo.

Mwisho.

VIJANA WAILILIA SERIKALI KUWAINUA KIUCHUMI

Na John Gagarini, Kisarawe

SERIKALI imeombwa kusaidia vikundi vya vijana vinavyopata mafunzo mbalimbali ya kuwainua kiuchumi ili waweze kujiajiri wakiwa Vijijini badala ya kukimbilia Mijini.

Akisoma risala ya wahitimu mbele ya mgeni rasmi ambaye ni kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima kwenye Kijiji cha Kibuta wilayani Kisarawe, Mariam Christopher alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kuweza kukabili mazingira wanayoishi huko huko waliko kuliko kukimbilia mjini kutafuta ajira.

Christopher alisema kuwa masomo waliyojifunza ni ya ufundi kwa vijana wa kata ya Kurui kupitia mradi wa kuwajengea uwezo vijana (YEE) unaosimamiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali Plan International wilaya ya Kisarawe.

“Tunashukuru wafadhili wetu kwani tumeweza kujifunza mambo mengi ya ufundi tunaamini yatatusaidia tukiwa huku huku bali kikubwa ni Halmashauri kutuwekea mazingira mazuri ya kufanya kazi ili tuisaidie jamii ya Kijijini hasa ikizingatiwa nako kuna hitaji maendeleo,” alisema Christopher.

Alisema kuwa mafunzo hayo wameyapata kwa kina katika fani mbalimbali za upambaji, mapishi, udereva, ushonaji na utengenezaji wa mapambo na wanatarajia kuboresha shughuli hizo Vijijini ili kuleta maendeleo kwa familia zao na wao binafsi.

Aidha alisema kuwa mafunzo hayo yanafadhiliwa na Eu, Vso, Uhiki, Veta na Plan International wilayani humo na yanatekelezwa kwenye kata Sita za Kibuta, Kisarawe, Manerumango, Msimbu, Kurui na Marumbo na yanatarajiwa kuwafikia vijana 1,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.

Kwa upande wa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa George Mbijima alisema kuwa Halmashauri inapaswa kuwatengenea vijana asilimia tano ya mapato yao kwa ajili ya kuwakopesha vijana kwani suala hilo liko kisheria na wanapaswa kutekeleza ili kuwajenga vijana kiuchumi, Mwenge huo leo unatarajiwa kukimbizwa wilaya ya Rufiji.

Mwisho. 





SERIKALI KUWAWEKEA MAZINGIRA MAZURI WAWEKEZAJI

Na John Gagarini, Kisarawe
SERIKALI itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje ambao watafuata taratibu za nchi ili kuongeza pato la taifa kupitia sekta ya uwekezaji ambayo kwa sasa inakuwa kwa kasi kwenye mikoa mbalimbali.
Hayo yalisemwa na kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwenye Bandari ya Nchi Kavu inayojengwa kwenye Kijiji cha Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani.
Mbijima alisema kuwa nchi kwa sasa iko kwenye kipindi cha utekelezaji  kwa vitendo sera ya uwekezaji ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi pamoja na serikali ili iweze kuwaletea maendeleo wananchi kupitia uwekezaji.
“Serikali inathamini mchango wa wawekezaji kwani wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na nchi lakini kikubwa ni kuwa wazi wakati wa kufanya taratibu za uwekezaji ili kuondoa malumbano yanayojitokeza baina ya wananchi na wawekezaji,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakikiuka taratibu za uwekezaji kwa kutokuwa wazi wakati wakufanya michakato ya uwekezaji kwani wanapaswa kuwa wazi kwa pande zinazohusika ili kuondoa mikanganyiko.
“”Wawekezaji wanapaswa kufuata sheria za nchi zilizowekwa ili faida inayopatikana iweze kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya uwekezaji hivyo wanapaswa kushirikiana na wananchi ili kuondoa migogoro isiyo na tija kwa uwekezaji”,  alisema Mbijima.
Aidha alisema kuwa serikali inatoa ushirikiano na wawekezaji kwnai mbali ya kutoa ajira kwa wananchi pia serikali inapata mapato yake kupitia sekta hiyo ili iweze kuendesha shughuli zake kupitia kodi na ushuru mbalimbali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Kampuni ya DSM Corridor Group  Sada Shaban alisema kuwa ujenzi huo wa Bandari kavu ulianza 2013 na kukamilika mwaka huu kwa baadhi ya vitengo ukiwa umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.5 ambapo gharama iliyobakia ni kiasi cha shilingi bilioni 38 hadi kukamilika kwake.
Shaban alisema kuwa eneo hilo litakuwa ni hifadhi ya bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na maghala ya mazao mbalimbali, madini na mizigo ya kila aina na itasaidia kupunguza msongamano barabarani kwani ikitoka hapo inapakizwa kwenye treni ambayo iko jirani na bandari hiyo. Mwenge huo ukiwa wilayani Kisarawe ulizindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 6.5 leo mwenge unakimbizwa wilayani Rufiji.
Mwisho.





Friday, May 20, 2016

WANANCHI KUEPUKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI

Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa Mitaa ya Viziwaziwa na Sagale wilayani Kibaha mkoani Pwani wataondokana na adha ya ukosefu wa Maji baada ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi 517,110,110 kuzinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima.
Mradi huo utakaohudumia wakazi 1,482 umekamilika baada ya Halmashauri kuomba maji kwenye bomba kuu la Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO) la Ruvu Juu baada ya majaribio ya kuchimba visima vya ardhini ambavyo havikupata maji.
Akielezea juu ya mradi huo katibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Ziwaziwa na Sagale (SAVI) Abdulrahman Mango alisema kuwa mradi huo ni moja ya miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira ni moja wapo ya mitaa minne iliyopo kwenye kata ya Viziwaziwa ambako katika Halmashauri kwenye miradi hiyo kuna jumla ya mitaa 13.
“Kabla ya kuwa na mradi huu tulikuwa tunategemea maji ya visima vya asili ambavyo ni vya msimu ambapo maji tuliyokuwa tukiyatumia yalikuwa siyo safi wala salama na inapofikia wakati wa kiangazi tunakwenda kuchota maji kwenye mtaa jirani wa Kwa Mfipa uliopo kilomita saba na kuwachukulia wananchi muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Mango.
Mango alisema kuwa mradi huo una husisha ujenzi wa tanki la chini lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa chumba kwa ajili ya kuweka pampu, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba, tanki la juu lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na ujenzi wa mifumo matanki ya uvunaji wa maji ya mvua.
“Ujenzi wa miundombinu ya umekamilika na kwa sasa vituo tisa kati ya 10 vinatoa huduma ya maji kwa mgao wa DAWASCO siku mbili kwa wiki na unasimamiwa na SAVI na jamii huchangia shilingi 100 kwa ndoo ya lita 20 ambapo fedha hupelekwa benki na hadi sasa kuna akiba ya shilingi 950,000 na fedha zinazopatikana hutumika kwa ajili ya kulipia bila ya umeme, kufanya ukarabati mdogomdogo, uendeshaji wa ofisi na kulipa bili ya DAWASCO,” alisema Mango.
Aidha alisema kuwa mradi huo umechangiwa na wananchi kiasi cha shilingi milioni 12 kwa kutoa maeneo yao na kupitisha mabomba na kujenga vituo vya maji vya jamii na kutekeleza azma ya Rais Dk John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mbijima alisema kuwa azma ya serikali ni kuwapunguzia kero wananchi kwa kupata huduma za kijamii karibu ili wapate muda mwingi wa kufanya shughuli za maendeleo na si kutumia muda mwingi kutafuta huduma.  

Mwisho.

MWENGE HAUNA ITIKADI

Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa dhana ya Mwenge wa Uhuru si itikadi ya chama au watu wa aina fulani bali ni kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia miradi ambayo imetokana na nguvu zao.
Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima alipokuwa akizindua bweni la wasichana kwenye Shule ya Sekondari ya Zogowale wakati mwenge huo ukikimbizwa wilayani humo.
Mbijima alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya maendeleo katika nchi ambapo mwasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliutumia kama ishara ya maendeleo.
“Mwenge ni alama muhimu katika maendeleo ya nchi kwani kila mahali ulipopita umeacha alama ya maendeleo na lengo lake ni kuhamasisha watu kuwa wanapaswa kuwajibika ili kuleta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa jumla,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa watu wanaobeza Mwenge hawajui historia ya nchi na umuhimu wa mwenge ambacho umezindua na kufungua miradi mingi ya maendeleo ambayo imewaletea watu mafanikio.
“Sehemu yoyote ambayo mwenge umepita umeleta mafanikio kutokana na miradi iliyopo na kufunguliwa au kuzinduliwa na mbio hizi ambazo hufanyika kila mwaka,” alisema Mbijima.
Aliwaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza kwenye mambo ambayo yatawaharibia masomo yao ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya au kushiriki kwenye vitendo vya ngono ambavyo mwisho wake ni kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ukimwi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mwalimu mkuu wa shule hiyo tatu Mwambala alisema kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2015 na kukamilika mwaka mwaka huo huo na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 230,814,608.
Mwambala alisema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kuongeza ufaulu ambapo bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 86 na lina miundombinu yote. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na ilipata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita mwaka 2014 na ina wanafunzi 408.
Mwenge huo ukiwa wilayani Kibaha ulitembelea miradi mbalimbali yenye tahamani ya shilingi zaidi ya bilioni nne leo unakimbizwa wilayani Mkuranga kuendelea na mbio zake.

Mwisho.          

ASKARI POLISI AUWAWA KWA RISASI

Na John Gagarini, Kibaha

ASKARI wa jeshi la  polisi kikosi cha usalama barabarani mwenye namba F.1839 sajent (SGT) Ally Salum maarufu Kinyogori ameuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika akiwa nyumbani  kwake.
>
> Tukio hilo limetokea may 19,majira ya saa 1.30 usiku huko katika kijiji cha Chatembo kata ya Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
>
> Kamanda wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi,amesema katika hali isiyo ya kawaida watu wawili wakiwa wamevalia makoti meusi na nyuso zao wakiwa wamezificha kwa mask walifanya mauaji hayo na kutokomea.
>
> Amesema watu hao waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya askari huyo wakitumia usafiri wa pikipiki aina ya boxer na baada ya kushuka kwenye pikipiki waliingia ndani na kumfyatulia risasi askari huyo kichwani pamoja na ubavuni na kumpotezea maisha yake.
>
> Kamanda Mushongi amesema katika tukio hilo wauaji hao hawakuchukua  kitu chochote zaidi ya funguo wa gari la  marehemu ambapo waliondoka nalo.
>
> Amesema msako mkali wa kuwasaka waliohusika  na tukio unaendelea  na ameomba  ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa wale wenye taarifa zitakazosaidia kuwapata  wahusika hao.
>
> Mwili  wa marehemu umehifadhiwa  katika hospital ya Temeke na utakabidhiwa  kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi mara  baada ya kufanyiwa uchunguzi .
>
> Mwisho