Friday, May 20, 2016

WANANCHI KUEPUKANA NA ADHA YA UKOSEFU WA MAJI

Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa Mitaa ya Viziwaziwa na Sagale wilayani Kibaha mkoani Pwani wataondokana na adha ya ukosefu wa Maji baada ya mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi 517,110,110 kuzinduliwa na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima.
Mradi huo utakaohudumia wakazi 1,482 umekamilika baada ya Halmashauri kuomba maji kwenye bomba kuu la Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO) la Ruvu Juu baada ya majaribio ya kuchimba visima vya ardhini ambavyo havikupata maji.
Akielezea juu ya mradi huo katibu wa Jumuiya ya Watumiaji Maji wa Ziwaziwa na Sagale (SAVI) Abdulrahman Mango alisema kuwa mradi huo ni moja ya miradi ya Maji na Usafi wa Mazingira ni moja wapo ya mitaa minne iliyopo kwenye kata ya Viziwaziwa ambako katika Halmashauri kwenye miradi hiyo kuna jumla ya mitaa 13.
“Kabla ya kuwa na mradi huu tulikuwa tunategemea maji ya visima vya asili ambavyo ni vya msimu ambapo maji tuliyokuwa tukiyatumia yalikuwa siyo safi wala salama na inapofikia wakati wa kiangazi tunakwenda kuchota maji kwenye mtaa jirani wa Kwa Mfipa uliopo kilomita saba na kuwachukulia wananchi muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo,” alisema Mango.
Mango alisema kuwa mradi huo una husisha ujenzi wa tanki la chini lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa chumba kwa ajili ya kuweka pampu, uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba, tanki la juu lenye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa vituo 10 vya kuchotea maji na ujenzi wa mifumo matanki ya uvunaji wa maji ya mvua.
“Ujenzi wa miundombinu ya umekamilika na kwa sasa vituo tisa kati ya 10 vinatoa huduma ya maji kwa mgao wa DAWASCO siku mbili kwa wiki na unasimamiwa na SAVI na jamii huchangia shilingi 100 kwa ndoo ya lita 20 ambapo fedha hupelekwa benki na hadi sasa kuna akiba ya shilingi 950,000 na fedha zinazopatikana hutumika kwa ajili ya kulipia bila ya umeme, kufanya ukarabati mdogomdogo, uendeshaji wa ofisi na kulipa bili ya DAWASCO,” alisema Mango.
Aidha alisema kuwa mradi huo umechangiwa na wananchi kiasi cha shilingi milioni 12 kwa kutoa maeneo yao na kupitisha mabomba na kujenga vituo vya maji vya jamii na kutekeleza azma ya Rais Dk John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani.
Kwa upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Mbijima alisema kuwa azma ya serikali ni kuwapunguzia kero wananchi kwa kupata huduma za kijamii karibu ili wapate muda mwingi wa kufanya shughuli za maendeleo na si kutumia muda mwingi kutafuta huduma.  

Mwisho.

MWENGE HAUNA ITIKADI

Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa dhana ya Mwenge wa Uhuru si itikadi ya chama au watu wa aina fulani bali ni kuhamasisha maendeleo ya wananchi kupitia miradi ambayo imetokana na nguvu zao.
Hayo yalisemwa wilayani Kibaha na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa George Mbijima alipokuwa akizindua bweni la wasichana kwenye Shule ya Sekondari ya Zogowale wakati mwenge huo ukikimbizwa wilayani humo.
Mbijima alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya maendeleo katika nchi ambapo mwasisi wake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliutumia kama ishara ya maendeleo.
“Mwenge ni alama muhimu katika maendeleo ya nchi kwani kila mahali ulipopita umeacha alama ya maendeleo na lengo lake ni kuhamasisha watu kuwa wanapaswa kuwajibika ili kuleta mafanikio kwa mtu mmoja mmoja na jamii nzima kwa jumla,” alisema Mbijima.
Alisema kuwa watu wanaobeza Mwenge hawajui historia ya nchi na umuhimu wa mwenge ambacho umezindua na kufungua miradi mingi ya maendeleo ambayo imewaletea watu mafanikio.
“Sehemu yoyote ambayo mwenge umepita umeleta mafanikio kutokana na miradi iliyopo na kufunguliwa au kuzinduliwa na mbio hizi ambazo hufanyika kila mwaka,” alisema Mbijima.
Aliwaasa wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha kujiingiza kwenye mambo ambayo yatawaharibia masomo yao ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kulevya au kushiriki kwenye vitendo vya ngono ambavyo mwisho wake ni kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwemo ukimwi.
Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi mwalimu mkuu wa shule hiyo tatu Mwambala alisema kuwa ujenzi huo ulianza mwaka 2015 na kukamilika mwaka mwaka huo huo na kugharimu kiasi cha shilingi milioni 230,814,608.
Mwambala alisema kuwa lengo la ujenzi huo ni kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kujifunzia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita ili kuongeza ufaulu ambapo bweni hilo lina uwezo wa kulaza wanafunzi 86 na lina miundombinu yote. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007 na ilipata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita mwaka 2014 na ina wanafunzi 408.
Mwenge huo ukiwa wilayani Kibaha ulitembelea miradi mbalimbali yenye tahamani ya shilingi zaidi ya bilioni nne leo unakimbizwa wilayani Mkuranga kuendelea na mbio zake.

Mwisho.          

ASKARI POLISI AUWAWA KWA RISASI

Na John Gagarini, Kibaha

ASKARI wa jeshi la  polisi kikosi cha usalama barabarani mwenye namba F.1839 sajent (SGT) Ally Salum maarufu Kinyogori ameuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika akiwa nyumbani  kwake.
>
> Tukio hilo limetokea may 19,majira ya saa 1.30 usiku huko katika kijiji cha Chatembo kata ya Mwandege wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
>
> Kamanda wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi,amesema katika hali isiyo ya kawaida watu wawili wakiwa wamevalia makoti meusi na nyuso zao wakiwa wamezificha kwa mask walifanya mauaji hayo na kutokomea.
>
> Amesema watu hao waliingia ndani ya uzio wa nyumba ya askari huyo wakitumia usafiri wa pikipiki aina ya boxer na baada ya kushuka kwenye pikipiki waliingia ndani na kumfyatulia risasi askari huyo kichwani pamoja na ubavuni na kumpotezea maisha yake.
>
> Kamanda Mushongi amesema katika tukio hilo wauaji hao hawakuchukua  kitu chochote zaidi ya funguo wa gari la  marehemu ambapo waliondoka nalo.
>
> Amesema msako mkali wa kuwasaka waliohusika  na tukio unaendelea  na ameomba  ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa wale wenye taarifa zitakazosaidia kuwapata  wahusika hao.
>
> Mwili  wa marehemu umehifadhiwa  katika hospital ya Temeke na utakabidhiwa  kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi mara  baada ya kufanyiwa uchunguzi .
>
> Mwisho

Thursday, May 19, 2016

MKURANGA MBIONI KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI

Na John Gagarini, Kibaha
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani limechonga madawati 5,043 ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato akisoma taarifa ya wilaya hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo wakati wa ziara yake kutembelea wilaya hiyo kukagua shughuli za maendeleo.
Kihato alisema kuwa wilaya hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 5,131 hivyo kubakiwa na upungufu wa madawati 500 ambayo wanatarajia kukamilisha utengenezaji muda mfupi ujao.
“Tatizo la upungufu wa madawati kwa wanafunzi wa shule za Sekondari tatizo hilo hakuna ila tatizo kubwa liko kwa wanafunzi wa shule za Msingi kutokana na uwingi wao na hata wale wa darasa la kwanza ambapo kwa mwaka huu walioandikishwa ni wengi sana,” alisema Kihato.
Alisema kuwa hawana wasiwasi kwani hadi ule muda uliowekwa wa Juni 30 kwa wilaya zote kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha kabisa kwani wanashirikiana na wadau mbalimbali kutengeneza madawati.
“Tunawahimiza watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanakamilisha zoezi hilo ili kuwaondolea adha wanafunzi kukaa chini na kuwafanya washindwe kujifunza vizuri masomo yao,” alisema Kihato.
Aidha aliwaomba wadau wa maendeleo ndani ya wilaya hiyo kuwaunga mkono katika kufanikisha zoezi hilo la uchongaji wa madawati kwa wanafunzi kwenye wilaya hiyo.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa anaipongeza wilaya hiyo kwa kuweza kufanikisha kuchonga madawati hayo ambayo sasa yanaenda kuondoa tatizo hilo la upungiufu wa madawati.
Ndikilo alisema kuwa mkoa huo ulikuwa una upungufu wa madawati 43,047 kwa shule za msingi lakini kwa jitihada hizo zitakuwa zimepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu huo.

Mwisho.

MKURANGA YAZUIA MALIPO YA MISHAHARA YA WATUMISHI 15

Na John Gagarini, Mkuranga
WILAYA ya Mkuranga mkoani Pwani imewasimamishia malipo watumishi 15 ambao wameondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ya taarifa kwa mwajiri wake ambaye ni Halmashauri.
Hayo yalisema na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Abdala Kihato alipokuwa akisoma taarifa ya wilaya wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Pwani kutembelea shughuli za maendeleo kwenye wilaya hiyo.
Kihato alisema kuwa mishahara hiyo ilizuiliwa kutokana na watumishi hao kutotoa taarifa walipoondoka kwenye vituo vyao vya kazi wakati wa uhakiki watumishi katika zoezi la kutambua watumishi hewa.
“Tulifanya uhakiki wa watumishi 179 na kubaini kuwa watumishi 85 walikuwa ni watoro ambapo 51 wamehamia kwenye vituo vingine vya kazi 10 hawakujitokeza na 15 ndiyo walioondoka kwenye vituo vya kazi bila ya taarifa na watano ni watoro kabisa,” alisema Kihato.
Alisema kuwa zoezi hilo ni endelevu na linaendelea kwani linaoneka lina changamoto nyingi katika kubainisha watumishi hewa na wale ambao wako kisheria.
“Hatua tuliyoichukua kwa wale ambao waliondoka kwenye vituo vyao vya kazi bila ya taarifa ni kusimamisha mishahara yao ili wasije wakwa wanachukua fedha pasipo kufanya kazi,” alisema Kihato.
Kwa upande wake Ndikilo alisema kuwa maofisa utumishi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa serikali katika kuhakikisha watumishi hewa wanapatikana na itawachukulia hatua kali wale watakaowaficha watumishi hewa.
Ndikilo alisema kuwa zoezi hilo litakapokamilika mkoa utatoa taarifa juu ya zoezi hilo ambalo lina lengo la kuondoa watumishi hewa ambao wamekuwa wakijipatia fedha pasipo kufanya kazi.

Mwisho.

MWENGE KUPITIA MIRADI YENYE THAMANI YA BILIONI 66.3

Na John Gagarini, Bagamoyo
MWENGE wa Uhuru jana ulianza mbio zake mkoani Pwani baada ya kumaliza kuzunguka mkoa wa Dar es Salaam ambapo utakimbizwa kwenye Wilaya Sita za mkoa huo na kupitia miradi 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 66.3.

Akizungumza mara  baada ya kukabidhiwa mwenge  wa uhuru kutoka wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam  mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, alisema miradi hiyo imetekelezwa kwa ushirikiano wa serikali kuu na wananchi.

Ndikilo alisema kuwa kati ya miradi hiyo 47, miradi 14 itawekwa mawe ya msingi, 11 itazinduliwa,11 itafunguliwa na miradi mingine 11 itakaguliwa na mwenge huo utakapokuwa mkoani hapa.

 “Miradi mingine  imetekelezwa na Halmashauri, wahisani wa kitaifa na kimataifa pamoja na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambapo ujumbe wa mwenge  mwaka huu unasema vijana ni nguvu kazi ya taifa na shirikisho la kuwezeshwa hivyo tupige vita matumizi ya madawa ya kulevya,” alisema Ndikilo.

Alisema kuwa kwa kutambua changamoto za vijana mkoa umejipanga katika kutatu  changamoto za vijana kwa ushirikiano na vijana wenyewe ambao katika mkoa huu wapo vijana 379,646 kati ya watu milioni 1.9.

“Mkoa umejipanga kutekeleza ujumbe huo kwa vitendo kwani  msingi mkubwa wa ujumbe ni vijana ndio nguzo na ni chachu kubwa ya maendeleo katika taifa hivyo lazima tuwape nafasi,” alisema Ndikilo.

Aidha aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zilizopo ili kujibu changamoto hususan za ajira walizonazo na ni wakati wa vijana kujitokeza kutumia fursa mbalimbali zikiwemo kujiajiri na kuwajibika ili kukabiliana na changamoto walizonazo kwa kuzigeuza kuwa fursa za ajira kwenye maeneo yao.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paulo Makonda akimkabidhi Ndikilo mwenge huo wa Uhuru alishukuru kukabidhi mwenge  huo kwa mkoa wa Pwani huku ukiwa umetembea mkoani kwake bila ya tatizo lolote na Mwenge leo  utakimbizwa katika wilaya ya Kibaha.

Mwisho


WANANCHI WALILIA DARAJA

Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wa mtaa wa Mkombozi wilayani Kibaha mkoani Pwani umeiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwajengea kivuko au daraja kwenye mto Mpiji kwa ajili ya kuvuka kwenda Majohe wilaya ya Kinondoni kupata huduma za kijamii ambako ni jirani na ikilinganishwa na Maili Moja wilaya ya Kibaha umbali wa kilometa zaidi ya 10.
Akizungumza na waandishi wa habari mkazi wa mtaa huo Malaki Lakibuka alisema kuwa  huduma hizo wanazipata Majohe kutokana na ukaribu uliopo wa kilometa mbili ukilinganisha na Kibaha ambako ni mbali kwa zaidi ya kilometa 10, lakini tatizo lililopo ni kukosa kivuko au daraja.
Lakibuka alisema kuwa wako kwenye wakati mgumu kuvuka mto huo kutokana na kuwa na mamba wengi jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao ambapo kwa miaka ya nyuma watu walikuwa wakiliwa na mamba.
“Tunapata taabu sana kuvuka hapo mtoni kwani mamba ni wengi na pia endapo utapita vibaya unaweza kuchukuliwa na maji hasa wakati wa mvua hivyo kuhatarisha maisha yetu na ikizingatiwa kuwa watumishi wanaofanya kazi Majohe,” alisema Lakibuka.
Naye mweneykiti wa mtaa huo ambao ni mpya Moshi Mhagama alisema kuwa kutokuwa na kivuko ni changamoto kubwa kwa wananchi ambao wanategemea  hali inakuwa mbaya kipindi cha mvua ambapo mto huo unakuwa umejaa maji.
Moshi alisema kuwa wanategemea Majohe kama ni sehemu ya kupata mahitaji yao ya kawaida ambako ni jirani ikilinganishwa na Kibaha ambako ni mbali sana hivyo tungeomba Halmashauri iwasaidie ujenzi huo ambapo nao tayari walishaanza kuchangishana fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko.
“Kwa wagonjwa au mama wajawazito ni taabu kwani wanajifungulia wakiwa njiani lakini pangekuwa na daraja wangepita kwa urahisi na kuwawahisha wagonjwa kupata matibabu pia kuna wafanyakazi wanafanya kazi ngambo ya pili ni shida sana kuvuka mvua zinapokuwa nyingi,” alisema Moshi.
Naye diwani wa kata hiyo Agustino Mdachi alisema kuwa jambo hilo alilipeleka Halmashauri lakini alijibiwa kuwa uwezo wa kujenga daraja hilo haupo kutokana na gharama za ujenzi kuwa kubwa sana kiasi cha zaidi ya bilioni mbili.
Mdachi alisema kuwa changamoto kwenye eneo hilo ni kubwa sana kwani mbali pia kuna mamba ambao ni hatari kwa watu wanaovuka hapo hivyo kuhatarisha maisha yao.
“Mbali ya Halmashauri kusema kuwa hawana uwezo wa kujenga daraja kwa sasa pia walisema hawawezi kujenga kivuko cha muda kwani gharama itakuwa mara mbili wao wanataka wajenge kitu cha kudumu ambapo ni ujenzi wa daraja,”alisema Mdachi.
Mwisho.