Friday, April 1, 2016

SAKATA WAFANYAKAZI HEWA RC AWATAKA WAKURUGENZI KUBAINISHA WALIOKUWA WAKICHUKUA MISHAHARA PASIPO KUWA WAFANYAKAZI

Na John Gagarini, Kibaha
SAKATA la wafanyakazi hewa mkoani Pwani limeingia hatua mpya baada ya Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa huo kutakiwa kutoa taarifa zaidi juu ya wafanyakazi hewa 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini wamekuwa wakipokea mishahara kila mwezi.
Jumla ya wafanyakazi 42 kwenye mkoa huo majina yao yapo lakini wao hawapo kazini lakini walikuwa wakipokea mishahara kila mwezi hali ambayo imeisababishia hasara kubwa serikali kutokana na kulipa hewa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kiwake mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wafanyakazi hao hewa wamewekwa kwenye madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na hao 42 ambao hawapo kabisa kazini lakini walikuwa wanalipwa.
“Kutokana na hali hii nimewapa wakurugenzi hadi siku ya Jumatano Aprili 6 wawe wameniletea taarifa juu ya watu waliokuwa wakipokea fedha hizo kwani haiwezekani ni nani aliyekuwa akipokea fedha hizo licha ya kutokuwepo kabisa kwa wafanyakazi hao,” alisema Ndikilo.
Ndikilo alisema kuwa haiwezekani fedha zilipwe kwa wafanayakazi ambao hawapo kazini kwani ni jambo la kushangaza na lazima ajulikane ambaye alikuwa akipokea fedha hizo kwani kundi hili ni hewa kabisa.
“Kundi lingine ni la wafanyakazi 58 ambao wamesimamishwa kazi kwa tuhuma mbalimbali lakini wamekuwa wakipokea mishahara kama kawaida tunataka tujuea kwa undani ni tuhuma gani zinazowakabili na hatua zilizochukuliwa dhidi yao,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kundi lingine ni la wafanyakazi ambao wako kazini lakini ni watoro hawaendi kazini lakini mishahara wanachukua kama kawaida licha ya kwamba hawawajibiki kazini kama ilivyo taratibu za utumishi wa umma.
“Tunataka kila mkurugenzi atoe taarifa sahihi bila ya kuficha kwani endapo atabainika ameficha taarifa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake hivyo ni vema wakawea wazi taarifa za hao wafanyakazi hewa,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa juu ya hasara waliyoiingiza wafanyakazi hao hewa ambapo kwa mkoa wa Pwani ni 150 bado wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ni kiasi gani ambacho wameliingizia Taifa hasara na mara watakapokamilisha watatoa taarifa hizo.

Mwisho.

SELEMAN TALL ATWAA MKANDA WA TPBO

Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Said Seleman maarufu kama Tall juzi usiku alitwaa ubingwa wa taifa wa ngumi uzito wa kati kupitia shirikisho la ngumi la TPBO baada ya kumshinda kwa pointi Ambokile Chusa.
Pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye ukumbi wa Container wilayani Kibaha mkoani Pwani lilikuwa la vuta ni kuvute kutokana na umahiri wa mabondia hao ambao hata hivyo walikuwa wakicheza kwa kuogopana kwa hofu ya kupoteza ushindi.
Hata hivyo Tall alikuwa mjanja na kumzidi mbinu mpinzani wake ambaye muda mwingi alikuwa akijihami kwa kuficha uso ili kukwepa ngumi kali zilizokuwa zikirushwa na mpinzani wake.
Kwenye mapambano mengine Yasini Said alimpiga Julius Jackson, Emanuel Endrew alimpiga Ramadhan Keshi, Ramadhan Kamage alimtwanga Kassim Chuma, Salehe Muntari alimtwanga Aziz Pendeza, Hassan Mgosi alimtwanga Hemed Hemed, Said Chino alimtwanga Idd Mgwinyo kwa TKO, huku Alfred Masinda na Nurdin Mijibwa na Abdala Luwanje na Rajabu Mbena walitoka sare.
Akikabidhi mkanda huo kutoka TPBO mgeni rasmi katika pambano hilo Selina Wilson Diwani wa Viti Maalumu aliwapongeza waandaaji wa pambano hilo Butamanya Promotion kwa kuleta shindano hilo Kibaha.
Wilson alisema kuwa kuleta mchezo huo Kibaha ni kuibua vipaji vilivyopo mikoani na kuwapa uzoefu mabondia wa hapa kuweza kujifunza mbinu za ngumi.
“Mimi ni kijana na nimeona jinsi gani watu wanavyopenda mchezo huu hapa Kibaha na mkoa wa Pwani nitahakikisha naunga mkono mchezo huu na kupeleka halamashauri changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kuboresha mchezo huu,” alisema Wilson.
Kwa upande wake bondia wa zamani Habibu Kinyogoli alisema kuwa mabondia wa mkoa wa Pwani wameonyesha uwezo lakini walichokosa ni mbinu za mapigano hivyo atajitolea kuwafundisha mabondia wa mkoa wa Pwani.

Mwisho.

Wednesday, March 30, 2016

MABONDIA KUWANIA MKANDA TPBO KIBAHA

Na John Gagarini, Kibaha
MABONDIA Said Seleman Ambokile Chusa wajijini Dar es Salaam leo wanatarajia kupambana kwenye pambano la ngumi la kuwania ubingwa TPBO uzito wa kati pambano litakalo pigwa kwenye ukumbi wa Container Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha moja ya wasimamizi wa pambano hilo ambaye ni mwalimu wa ngumi Gordon Tambwe maarufu kama Mawe alisema kuwa pambano hilo litakuwa kali na la kuvutia.
Mawe alisema kuwa lengo la kufanya pambano hilo Kibaha ni kuhamasisha mchezo huo mikoani pia kuinua vipaji kwa mabondia wa mikoani ili nao waweze kuonyesha uwezo wao.
“Tumeleta pambano hili Kibaha ili kuhamasisha mchezo wa ngumi sehemu mbalimbali mikoani kwani michezo ni ajira na ngumi zimewasaidia vijana wengi kujiajiri kupitia mchezo huo,” alisema Mawe.
Aidha alisema kuwa mabondia hao watapigana raundi 10 na pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi ambayo yatausisha mabondia kutoka mkoa wa Pwani na wageni wao kutoka Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Seleman alisema kuwa amejiandaa ipasavyo na anatarajia kummaliza mapema mpinzani wake kwa KO kwani hatakuwa na muda wa kupoteza katika kumaliza pambano hilo.
Naye Chusa alisema kuwa amekwenda Kibaha kwa ajili ya kutafuta ubingwa na si kutalii na anatarajia kumpiga mpinzani wake ili kuwapa raha wapenzi wake hivyo wasiwe na wasiwasi. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa diwani wa Viti maalumu Selina Wilson.

Mwisho.

Saturday, March 26, 2016

MABASI YA MIKOANI 48 YAKUTWA NA MAKOSA MBALIMBALI

Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya mabasi 48 ya abiria ya kwenda mikoani yamekutwa na makosa mbalimbali kufuatia zoezi la ukaguzi lillofanywa kwa ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (SUMATRA).  
Zoezi hilo lilifanywa kwenye Stendi Kuu ya Ubungo, Maili Moja na Chalinze kwa lengo la kudhibiti ajali pamoja na madereva wanaokiuka taratibu za usalama barabarani kwa mabasi hayo yaendayo mikoani .
Akizungumza na gazeti hili Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini ACP Fortunatus Musilimu alisema kuwa zoezi hilo ambalo lilikuwa la kushtukiza litakuwa endelevu ili kuhakikisha ajali zinapungua na kuwaondolea usumbufu abiria.
Musilimu alisema kuwa waliyafanyia ukaguzi mabasi 169 na kuyabaini mabasi hayo 48 kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendokasi mabasi 24, kutofunga mikanda mabasi tisa, kuwazidishia nauli nane, ubovu basi moja, kukiuka ratiba basi moja na leseni basi moja.
“Pia tulimakamata dereva mmoja kwa kutumia kilevi ambapo alikuwa na kiwango cha juu cha ulevi cha 77.7 ambapo kwa kawaida kinatakiwa kuwa 00.8 kwa mujibu sheria hali iliyosababisha dereva huyo kushushwa na kupelekwa rumande,” alisema Musilimu.
Alisema kuwa ukaguzi huo unandelea kote nchi ambapo tayari makamanda wa usalama barabarani mikoani wameshapewa maagizo ya kufanya ukaguzi wa mabasi kwani ukaguzi hauwezi kuyakagua mabasi yote kutokana na eneo la ukaguzi kuwa dogo hali ambayo inawafanya wafanyie ukaguzi mabasi matano matano kwa wakati mmoja huku mengine yakiendelea na safari.
Aidha alisema kuwa mbali ya kukagua mabasi hayo pia walikagua malori ya mchanga 13 na kuyakuta na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mwendo kasi magari saba, mabovu matano, kuyapita magari mengine pasipo kuzingatia sheria.
Aliwataka abiria kutoa taarifa kwenye vyombo husika kwa madereva ambao wanaoendesha magari kwa mwendo wa kasi pia wasiwashabikie kwani ni moja ya vyanzo vya ajali za barabarani ambazo zinasababisha vifo vya watu wengi.
Mwisho.

Friday, March 25, 2016

RC AUNDA TUME KUCHUNGUZA KIWANDA JUU YA HAKI ZA WAFANYAKAZI

Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo ameunda Tume kutoka idara ya kazi ya mkoa huo kutembelea kiwanda cha Hong Yu Steel cha kuzalisha nondo kilichopo wilayani Kibaha kwa kushindwa kuzingatia masharti ya uendeshaji wa kiwanda na maslahi ya wafanyakazi.
Aliunda tume hiyo ya watu watatu itakayofanya kazi kwa wiki moja kufuatilia malalamiko hayo ya wafanyakazi kwa lengo la kuleta uwajibikaji kwa pande zote mbili katia ya wafanyakazi na wamiliki hao baada ya malalamiko kuzidi na kufanya ziara kujionea hali halisi.
Ndikilo alifikia hatua hiyo baada ya kupata malalamiko toka kwa wafanyakazi kuwa wamiliki wa kiwanda hicho hawajali usalama kazini kwa wafanyakazi wao kwa kushindwa kuweka vifaa vya kuwalinda kutokana na mazingira wanayofanyia kazi ambayo ni hatarishi kwa maisha yao.
“Tumesikia wafanyakazi na tumeona wafanyakazi wakifanya kazi huku wakiwa hawana vifaa vya kufanyia kazi kama vile baadhi yao hawajavaa kofia ngumu, gloves na mabuti kwa ajili ya kujikinga na hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa kufanya kazi,” alisema Ndikilo.
Alisema wafanyakazi wamelalamikia mambo mengi ikiwa ni pamoja na mshahara mdogo, kutokuwa na mikataba ya kazi, kutolipwa masaa ya ziada, kukatwa mishahara mara wanaposhindwa kwenda kazini kutokana na kuumwa au kuumia kazini, huduma ya kwanza kuchelewa pamoja na kutokuwa na mapumziko hata nyakati za sikukuu na mwisho wa wiki.
“Tumeona kuna matatizo mengi hivyo itaundwa tume kwa ajili ya kukaa na uongozi kwa ajili ya kurekebisha kasoro zilizopo kwa kuzingatia sheria za kazi kwani kila mtu anamtegemea mwenzake kati ya mwajiri na mfanyakazi hivyo hakuna sababu ya upande mmoja kumnyanysa mwenzake,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa tume hiyo itatembelea vitengo vyote kwa kuonana na viongozi wa vitengo husika na baadaye kukaa na uongozi ili kuangalia namna ya kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya wafanyakazi.
Kwa upande wake kaimu ofisa kazi wa mkoa Swalehe Njoma alisema kuwa haki nyingi za wafanyakazi zimevunjwa hivyo kuna haja ya kurekebisha na kuweka mazingira bora ya kazi ili haki iweze kupatikana kwani malalamiko ni mengi.
Njoma alisema kuwa moja ya haki za mfanyakazi ni kuwa na muda wa mapumziko na hata kama atafanya kazi kwa masaa ya ziada lazima alipwe na mfanyakazi anapoumwa au kuumia kazini hapaswi kukatwa fedha kutokana na kushindwa kwenda kazini kutokana na kujiuguza.
Naye ofisa mwajiri wa kiwanda hicho Asantemungu Filbert alikiri kuwepo na matatizo ambapo alisema kuwa yeye ni mgeni na hana muda mrefu ila kwa mtangulizi wake hakuweza kuweka mazingira mazuri ya wafanyakazi.
Filbert alisema kuwa tayari ameandaa utaratibu wa kushughulikia kero za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ili kukabiliana na changamoto zilizopo na kufanya utendaji kazi kuwa mzuri.
Mwisho.   

SUMATRA NA POLISI WAKAMATA MABASI

Na John Gagarini, Kibaha
MAMLAKA ya Usafirishaji Majini na nchi kavu SUMATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini wamefanya operesheni ya kushtukiza ya kukagua mabasi yaendayo mikoani na kubaini makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya madereva kutumia vilevi na kuwzidishia nauli abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha wakati wa zoezi hilo Mkurugenzi wa SUMATRA, Johnsen Kahatano alisema kuwa operesheni hiyo imefanywa ili kuwadhibiti wamiliki pamoja na madereva ambao wanakiuka sheria za usalama barabarani.
Kahatano alisema kuwa operesheni hiyo imefanikiwa kwani wameweza kukamata makosa kadhaa ambayo mengine ni ya barabarani na mengine ni ya kuwazidishia nauli abiria jambo ambalo ni kosa kisheria ambapo mabasi yaliyofanya makosa wamiliki wake watafikishwa mahakamani.
“Tumefanikiwa kumkamata dereva mmoja alikutwa akiwa ametumia kilevi na tulimkamata na kulizuia basi hilo hadi walipoleta dereva mwingine kwa ajili ya safari  jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wa abiria,” alisema Kahatano.
Alisema kuwa mabasi sita yalikamatwa yakiwa yamezidisha nauli ambpao abiria waliokuwa wakienda Moshi walkatiwa nauli ya kwenda Arusha ambayo ni shilingi 33,000 huku nauli halali kwa watu wanaoshukia Moshi ni shilingi 28,500.
“Mabasi yaliyowazidishia abiria walirudishiwa nauli zao kama taratibu zinavyoonyesha na hili ni kosa kisheria na abiria wanapaswa kulipa nauli halali ambazo zimepitishwa kisheria na wanapaswa kwenda kulalamika endapo watabaini wamezidishiwa,” alisema Kahatano.
Naye Kaimu Kamishna wa Usalama Barabarani Fortunatus Musilimu alisema kuwa abiria nao ni wadau muhimu katika vita ya kupambana na madereva au wamiliki wanaokiuka taratibu za usalama barabarani na kupunguza ajali hivyo wanapaswa kutoa taarifa kwao ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Musilimu alisema kuwa watu wanataka kuishi na maendeleo si kukatishwa uhai kutokana na ajali ambazo zinaweza kuzuilika na kutoa taarifa polisi kwa kutumia njia ya simu ambazo ziko kwenye mabasi yote lengo likiwa ni kupunguza ajali.
Mwisho.     


Thursday, March 24, 2016

WAWILI WASHIKILIWA KWA UTAPELI WAWILI WAKIMBIA

Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutaka kumtapeli mtu mmoja kiasi cha shilingi milioni tatu kwa kumuuzia madini aina ya Almasi ambayo ni bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao ambao walikuwa wanne wengine wawili walifanikiwa kukimbia walikamatwa baada ya kutaka kukimbia kutokana na mlalamikaji kupiga kelele ya kuomba msaada.
Mushongi alisema kuwa tukio hilo limetokea juzi eneo la CCM Mkoani wilayani Kibaha majira ya saa 3:30 asubuhi baada ya mlalamikaji kutoka kuchukua fedha kwenye benki ya NMB Tawi la Kibaha.
“Mlalamikaji mara baada ya kuchukua fedha alikutana na watuhumiwa hao ambapo waliongea naye na kumwambia kuwa wanauza madini aina ya Almasi ambapo walikubalina na akawakabidhi fedha hizo,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa watuhumiwa hao wakiwa kwenye gari aina ya Primio lenye namba za usajili T 668 DFY walianza kuondoka lakini mlalamikaji akagundua kuwa madini yale si halisi na kuanza kupiga kelele za wezi kuomba msaada ndipo waendesha pikipiki walipoanza kuwafukuza na baadaye polisi nao wakatokea na kuwakamata.
“Watuhumiwa hao baada ya kuona wamezingirwa walikimbia hata hivyo wawili walikamatwa na wengine wawili walifanikiwa kutokomea kusiko julikana nab ado tunaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ili kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma hizo,” alisema Mushongi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwantumu Juma maarufau kama Hawa, Fidelis Buberwa au Finas Barongo ambao wanashikiliwa kutokana na tukio hilo ambapo gari hilo linashikiliwa.
Kufuatia tukio hilo kamanda aliwataka wananchi kutokubali kuuziwa madini mikononi badala yake waende sehemu husika ambazo ziko rasmi kwa ajili ya uuzaji wa madini ili kuepukana na watu kama hao.
Mwisho